Habari za Punde

Balozi Seif Akutana na Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini

 Kiongozi wa Timu ya Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeiywo akiwasilisha muhtasari wa Ripoti ya Azimio lao waliofikia kwenye Mkutano wao wa Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini waliokutana hapa Zanzibar kuzungumzia hatma ya amani ya Mataifa yao mawili.
Kiongozi wa Timu ya Viongozi waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeiywo akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Ireland Nchini Tanzania Bibi Fionnuala Gilsenan aliyefika Ofisini kwake Vuga kusalimiana naye.(Picha na Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ.


Press Release:-
Mataifa ya Sudan na Sudan ya Kusini yanapaswa kuendelea kuvumiliana na kuaminiana katika masuala ya Uchumi na Utamaduni ili kusaidia kupunguza au kuondosha kabisa wimbi la kisiasa lililoyakumba Mataifa hayo kwa miongo kadhaa iliyopita na kusababisha Sudan ya Kusini kujitenga.


Hayo yamo katika Azimio la Zanzibar lililofikiwa mara baada ya kukamilika kwa Mkutano wa kwanza wa Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini waliokutana siku mbili katika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Kiongozi wa Mkutano huo wa Viongozi waandamizi wa Mataifa ya Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeiywo Kutoka Nchini Kenya alisema hayo wakati akitoa muhutasari wa ripoti ya Azimio hilo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Lazaro akiambatana na Mwakilishi wa Sudan Bwana Rabi Hassan , Profesa Pouline Riah wa Sudan ya Kusini, pamoja na Balozi David Kapya kutoka Ofisi ya Rais Mstaafu wa Tanzania alisema mafanikio makubwa yameanza kuchomoza kufuatia Mkutano huo.


“ Tumejaribu kuweka msingi madhubuti katika mkutano wetu utakaokuwa na muelekeo wa kujenga hali ya kuaminiana na kuvumiliana katika masuala ya kisiasa kwa pande zote mbili “. Alisisitiza Bw. Lazaro.

“ Mambo matatu ya msingi tuliyoyapendekeza katika ripoti ya Azimio letu la Zanzibar ni masuala ya Uchumi, Utamaduni na kuvumiliana katika siasa. Mipango yote tumependekeza yakubalike kufanywa kwa pamoja “. Alifafanua Bwana Lazaro Sumbeiywo.

Kiongozi wa Mkutano huo wa Viongozi waandamizi wa Mataifa ya Sudan na Sudan ya Kusini alimueleza Balozi Seif kwamba Mataifa hayo yanaweza kupiga hatua kubwa ya mafanikio iwapo jamii yao itaridhia kushirikiana katika masuala hayo hadi kwa wananchi wa kawaida.

Alisema Mkutano wa Pili wa Viongozi hao Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini mwezi ujao wa Mei Mjini Nairobi Nchini Kenya.

Nao Wawakilishi wa Pande hizo mbili za Sudan na Sudan na Kusini Bwana Rabi Hassan na Profesa Pouline Riah walisema Mkutano huo wa Zanzibar umejenga Histori mpya ya kuelekea kwenye mafanikio ya kudumu ya Kisiasa kati ya pande hizo mbili.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wamefarajika kuona Mkutano huo umemalizika kwa mafanikio makubwa.

Balozi Seif alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na fursa nzuri ya kuridhia Sudan kujiunga na Jumuiya hiyo kufuatia maamuzi ya mwanzo ya kuzitaka Sudan zote mbili kuondoa hitilafu zao kwanza.

“ Sisi Viongozi iwapo tutakosa kuwa na utulivu na uvumilivu wa kisiasa tutawezaje kuwaongoza wananchi wetu katika kuelekea kwenye maendeleo ? “. Aliuliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi wa Ireland Nchini Tanzania Bibi Fionnuala Gilsennan hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Viongozi hao wamezungumzia masuala mbali mbali ya uhusiano uliopo kati ya pande hizo mbili ambapo Balozi Fionnuala alieleza kwamba Zanzibar ina fursa nzuri ya kujifunza kwa Ireland mfumo wa uendeshaji wa serikali yenye muundo wa Umoja wa Kaitaifa.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisena Zanzibar hivi sasa imepata utulivu wa kisiasa baada ya uamuzi wake wa kufuata mfumo huo ambao bado ni mgeni miongoni mwa wananchi wake.

Alisema kumekuwa na mashirikiano mazuri ya uendeshaji Serikali miongoni mwa Mawaziri kutoka vyama vikuu viwili vilivyopata nafasi ya kuunda Serikali baada ya uchaguzi mkuu kufuatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyotoa fursa ya kuendesha Serikali yenye mfumo huo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/4/2013.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.