Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jaji Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
(Jumatatu, Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid. (Picha
na Tume ya Katiba)
Mwenyekiti wa kamati ya uwasilishaji wa
mapendekezo ya muundo wa mabaraza ya Katiba kwa jamii ya watu wenye ulemavu,
Bw. David Nyendo (kushoto) akiwasilisha maoni yake ya kamati hiyo kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika mkutano baina yao uliofanyika ofisi za Tume Jijini Dar es Salaam tarehe 13
Feb mwaka huu (2013). Kulia ni Mjumbe wa Tume, Dkt. Salim Ahmed Salim. (Picha
na Tume ya Katiba)
Na Mwandishi Wetu
Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.
Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa
walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia
kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba
itakayotolewa na Tume.
Hatua hii inafuatia ombi la
Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa
Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.
Chaguzi
za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia
mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote
hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa,
vijiji, vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba,
tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji
katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa
na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.
“Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa
na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri
mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya
Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa
Mwongozo,” amesema Jaji Warioba.
Changamoto
Akizungumzia kuhusu changamoto
zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na
mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa
na misimamo ya kisiasa na kidini
“Katika baadhi ya maeneo mikutano
ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na
mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi
kufangamanisha chaguzi za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya
kisiasa na kidini,” amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto
nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya
rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya
katiba.
“Tumepokea pia malalamiko ya
vitendo vya rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume
cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo
zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.
Aina
na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika mkutano huo uliofanyika
katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya
aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume
katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.
“Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba
ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba
itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa
wananchi,” alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama
mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao
kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.
Hatujajua maslahi ya Taifa lipi anayoyalinda huyu Warioba Wazanzibar washamwambia hawautaki wanataka kupumua yeye kashikamaslahi yaTaifa mbona hatumuelewi
ReplyDelete