Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi - Miundombinu kuyafanyia tathmini matuta yasiyo viwango

 
WIZARA ya Mawasiliano na Miundombinu, imesema imo katika mpango wa kufanya tathmini ujenzi wa matuta yaliowekwa barabarani bila ya kuzingatia taratibu kutokana na baadhi yao kuchangia ongezeko la ajali.

Waziri wa Wizara hiyo Rashid Hemed, aliyasema hayo jana wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani ya kuweka matuta katika bara bara ya Muungoni, Muyuni, Kitogani, Bwejuu na Pete.

Waziri huyo alisema ni kweli kuna barabara zinazohitaji matuta lakini kuna baadhi ya wananchi wameamua kuweka matuta bila ya ruhusa ya taasisi husika jambo ambalo tayari limeanza kuleta athari kutokana na baadhi yao kujengwa chini ya kiwango.

Alisema kazi ambayo wizara hiyo inajiandaa kukabailiana nayo ni kuangalia wapi wataweza kuweka matuta hayo ili kupunguza ongezeko la ajali.

Lakini alisema tatizo kubwa ni baadhi ya madereva kuzidaharau alama za barabarani.

Kutokana na hali hiyo,alisema wiki ijayo wizara itaandaa mkamkati kabambe wa kukabiliana na hali hiyo baada ya kuzindua wiki ya nenda kwa usalama, katika hoteli ya Bwawani.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi huyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Issa Haji Gavu, alisema serikali inaweka alama nyingi za barabarani lakini jambo la kusikitisha baadhi ya watu huamua kuzing’oa.

Alisema kutokana na hali hiyo wizara hiyo, imeamu kuchukua hataua za kuweka matuta katika maeneo ambayo yameonekana ni ya msingi yakiwemo maeneo ya skuli, masoko na vituo vya afya.

Alisema licha ya serikali kuweka matuta hayo kwenye maeneo hayo lakini bado kumekuwa na tatizo ya kuongezeka ajali kwa kila mwaka.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo ni vyema jamii ikazingatia kutii sheria zausalama barabarani ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
Alisema serikali itahakikisha inaendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii ili kupunguza matatizo hayo.




 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.