Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Afunguwa Mkutano wa Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini


 Kiongozi wa Mkutano wa Viongozi Waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeywo akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuufungua Mkutano huo unaofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
 Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hayupo Pichani kwenye Mkutano wao unaoendelea hoteli ya Sea Cliff iliyopo Mtaa wa Kama Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini mara baada ya kuufungua mkutano huo hapo Hoteli ya Sea Cliff Kama.
:- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Kiongozi wa Mkutano wa Viongozi waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeywo mara baada ya kuufungua mkutano wao.(Picha na Hassana Issa wa - OMPR – ZNZ.



                                                          Press Release:-

Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kusaidia mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Sudan pamoja na Sudan ya Kusini ambayo imejitenga ili kuona pande hizo mbili zinadumisha utulivu katika eneo la kati ya Bara la Afrika.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunguwa Mkutano maalum wa Viongozi waandamizi wa Mataifa hayo mawili wanaokutana katika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif aliwaambia Viongozi hao waandamizi wa Sudan zote mbili kwamba Dunia inaangalia Mikutano ya pande hizo huku ikijenga matumaini ya kupatikana kwa ufumbuzi unaotokana na migogoro inayotikisa Nchi hizo hasa lile suala la umiliki wa mafuta.

Balozi Seif alisema Jamii za Kimataifa zilikuwa zikishuhudia maelfu ya raia wa Sudan wasiokuwa na hatia wakiyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao kufuatia mivutano ya kisiasa kati ya Sudan na Sudan ya Kusini.

Alisema mivutano hiyo ilipelekea kuendelea kuzaa kwa vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopelekea kupoteza maisha ya watu hasa watoto na wanawake pamoja na mali zao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba wakati umefika kwa viongozi wa pande hizo mbili kumaliza kabisa tatizo hilo ili kutoa fursa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili kuelekeza nguvu zao katika maendeleo badala ya mivutano.

Alieleza kuwa Mataifa hayo bado yana fursa nzuri ya kulinda amani iliyoanza kujichomoza kati ya mahasimu hao kufuatia msingi uliowekwa tokea mwaka 2005 chini ya usimamizi wa rais wa zamani wa Marekani Bwana Jimmy Carter kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Kimataifa.

Balozi Seif alisisitiza kwamba msingi huo ulibuniwa makusudi ili kurejesha hali ya kuaminiana, kuvumiliana katika kuona utulivu na amani inaimarika katika Mataifa hayo yaliyopo kati kati mwa Bara la Afrika.

“ Kamwe haitawezekana hata kidogo jamii yoyote kupata maendeleo wakati Jamii hiyo imezunguukwa na migogoro ya kisiasa iliyoshamiri ndani ya harakati zao za Kimaisha “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Mapema Kiongozi wa Mkutano huo wa Viongozi waandamizi wa Mataifa ya Sudan na Sudan ya Kusini Bwana Lazaro Sumbeywo alisema Viongozi hao wameamua kufanya mkutano wao hapa Zanzibar kutokana na historia ndefu yiliyopo ya ukarimu waliyonayo Wazanzibari kwa wageni.

Bwana Lazaro aliupongeza Muungano uliopo Tanzania uliounganisha Mataifa mawili huru ya Zanzibar na Tanganyika ambao bado unaonekana kuleta faraja ya amani miongoni mwa wananchi wake.

Alifahamisha kwamba Muungano huu wa Jamuhuri ya Tanzania wanauchukulia kama kielelezo kwao kitakachowapa muongozo utakaowasaidia kuelekea kwenye mfumo wa amani wanaouhitaji katika mashirikiano ya pande zao mbili.

Wakitoa matumaini yao baadhi ya Viongozi hao waandamizi wa Sudan na Sudan ya Kusini wamesema mtazamo wao hivi sasa umelenga kuangalia hatma njema ya kizazi chao ambacho kilikuwa katika mazingira ya kubahatisha kufuatia mizozo ya kisiasa.

Walisema licha ya Sudan kuwa nchi ya mwanzo kujipatia uhuru wake Barani Afrika ikifuatiwa na Ghana lakini Taifa hilo lilikumbwa na migogoro ya kisiasa ya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka 66.

“ Tumefikia wakati hivi sasa kwa Wasudani kuhitaji kuishi kwa amani na matumaini bila ya kujali mtu anatoka sudan au Sudan ya Kusini “. Alisisitiza mmoja wa Viongozi hao waandamizi wa Sudan zote mbili Bwana Lual Deng.

Viongozi hao wameelezea faraja yao kutokana na uamuzi wa Rais Omar Al- Bashir wa Sudan kufanya ziara ya kihistoria Nchini Sudan ya Kusini tokea Mataifa hayo yalipojitenga miaka ya hivi karibuni.

Wananchi wa Sudan ya Kusini wakuamua kupiga kura ya maoni ya kutaka kujitenga na Sudan ambapo zaidi ya asilimia 70% ya wananchi hao walipinga kuendelea kuongozwa na utawala wa rais Omar Al-Bashir.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
14/4/2013.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.