Habari za Punde

Spika akutana na Naibu Mkurugenzi Mkaazi wa UNDP


Na himid Choko, BLW

SPIKA  wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Pandu Ameir Kificho amesema Wajumbe wa Baraza hilo hivi sasa  wako makini zaidi baada ya kujengewa uwezo mkubwa wa kiutendaji  chini ya Ufadhili  wa Shirila la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Amesema kwa kipidi kirefu  UNDP kupitia miradi tofauti ya Kusaidia Mabunge , imeweza kusaidia kutoa taaluma  ya utendaji wa vyombo hivyo hapa nchini.

Amesema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, chini ya miradi hiyo  limekuwa likifaidika kwa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa Wajumbe wa Baraza hilo  pamoja na watendaji .

Aidha  amesema UNDP kwa kiasi kikubwa  imesaidia  vitendea kazi  ndani ya Baraza hilo ikiwemo Usafiri.

Spika Kificho amesema hayo leo wakati akizungumza  na  Naibu Mkurugenzi  Mkaazi wa UNDP hapa nchini Bibi Mandisa  Mashologu  huko ofisi kwake Chukwani .


Amesema kutokana na mafunzo hayo  hivi sasa anaridhishwa  na utendaji wa wajumbe hao,  jambo ambalo limejenga  heshima na  imani kubwa kwa wananchi  kuhusiana na Maendeleo ya chombo chao cha Kutunga Sheria.

“ Wajumbe wangu hasa wale wa  upande wa Back Benchers’  (wasiokuwa Mawaziri /Manaibu Mawaziri) hivi sasa wako  makini, na wanafanya hivyo  kuibana serikali kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji  ambapo  nguvu hizi wanazipata kutokana na uwezo wanaojengewa  kupitia Ufadhili wa UNDP” Alisema Spika.

Akitoa mfano Spiika Kificho amesema  Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  tayari wamejengewa Uwezo  katika masuala ya uchambuzi wa Bajeti  na Miswaada ya Sheria  na mafanikio yake yameanza kuonekana.

Amesema kutokana na mafunzo hayo  wajumbe wa Baraza hilo hivi sasa  wamekuwa makini zaidi  wakati wa uchambuzi wa Bajeti ya Serikali  na  Miswaada ya Sheria  kitendo ambacho mara nyengine  kinawaweka katika wakati mgumu  baadhi ya Mawaziri na watendaji wa serikali kwa ujumla.

Amesema  hali hiyo inapelekea uwajibikaji mzuri  wa wajumbe wa Baraza hilo  pamoja na Mawaziri  suala ambalo ni zuri kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.

Spika kificho amemueleza Naibu Mkurugenzi huyo wa UNDP kuwa hata katika utendeji wa Kamati za Baraza hilo, umeimarika  ambapo hivi sasa kamati zimekuwa zikiibua mambo mengi  yanayohususiana na udhaifu au mafanikio ya  utendaji wa serikati na taasisi zake.

Hivyo Spika Kificho amelishukuru shirika hilo kwa misaada yake kwa Baraza la Wawakilishi na Taifa kwa ujumla  na kuahidi  kuendelea kuitumia vyema fursa  inayotolewa na shirika hilo.

Kwa upande wake Bibi Mandisa  Mashologu  amesema anaridhishwa na matumizi ya misaada  inayotolewa  na shirika hilo kwa Baraza la Wawakilishi  nha kuahidi kuendelea  kufanyakazi kwa karibu zaidi na Ofisi hiyo.

Amesema UNDP iko tayari  kuendelea kusaidia  vyombo vya kutunga sheria  lengo likiwa ni kuimarisha  kuongeza uwazi wa utendaji wa taasisis hizo.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kufahamu kwa uwazi  kinachotendeka  ndani ya vyombo hivyo  ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza demokrasia na utawala bora  hapa nchini.

1 comment:

  1. Kificho huna hataaibu kwamda wa miaka yamapinduzi mnasaidiwa vitendeakazi vya barazani?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.