Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa sensa ya watu na makazi Waziri Mkuu Pizengo Pinda akiwa pamoja na Kamishna wa Sensa ya watu na Makazi Tanzania Bara Hajat Amina Mrisho wakiangalia Ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya Utawala hapo Hyatt Legency Kilimanjaro Hoteli Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa sense ya watu na makazi Waziri Mkuu Pizengo Pinda akizindua Ripoti Ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya Utawala hapo Hyatt Legency Kilimanjaro Hoteli Jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa sensa ya watu na makazi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na uongozi wa Juu wa Kamati ya Sensa nje ya Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Legency Kilimanjaro Jijini Dar es salaam.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Waziri Mkuu Mh. Mizengo Piter Pinda alisema Serikali yeyote haitaweza kutoa huduma za Elimu, Afya sambamba na miundo mbinu bila ya kuwa na takwimu sahihi ya idadi ya wananchi wake.
Mh. Pinda alisema hayo wakati akizindua Ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya utawala ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 hapo katika ukumbi wa Hyatt Regency Hoteli ya Kilimanjaro Jijini Dar es salaam.
Aliitahadharisha jamii kuelewa kwamba kasi iliyopo ya ongezeko la idadi ya watu Nchini Tanzania ya asilimia 2.7 ina muelekeo wa kuashiria Taifa hili kuwa na ongezeko kubwa la mara mbili katika kipindi cha miaka 26 ijayo.
Alifahamisha kwamba wakati umefika kwa baadhi ya wananchi Nchini kuondoa dhana potovu waliyonayo ya kuona fahari ya kujipatia umaafuru wa kuwa na idadi kubwa ya watoto jambo ambalo ni hatari kwa hatma yao ya baadaye.
Waziri Mkuu Pinda aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya Nchini kote kuhakikisha kwamba Taarifa za sensa zinawafikia Viongozi wote kuanzia Wabunge,Wawakilishi hadi shina.
Alieleza kwamba Serikali Kuu imeanza kuimarisha miundo mbinu mbali mbali katika kuwasogezea huduma muhimu Wananchi kwa kuangalia vigezo vya Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi.
“ Ipo mipango tuliwahi kuitumia katika kipindi kilichopita kupitia taasisi ya uzazi wa Mpango Tanzania { UMATI } ambayo ilitusaidia kupanga uzazi katika mazingira bora ya kukabiliana na mfumko wa ongezeko kubwa la idadi ya watu. Sasa ipo haja ya kuifufua mipango hii katika kukabiliana na hili ”. Alisisitiza Mh. Pinda.
Mwenyekiti huyo wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Tanzania aliwashukuru washirika wa maendeleo wa kitaifa na kimataifa kwa michango yao ya kitaalamu na uwezeshaji iliyosaidia kufanikisha maradi wa sense Nchini.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi alisema Serikali zote mbili hazina budi kujipanga katika kubuni mipango na kuchukuwa hatua za muda mfupi na mrefu ilikukabiliana na changamoto zilizoibuliwa ndani ya ripoti hiyo.
BaloziSeif ` aliunga mkono utaratibu wa kusambazwa kwa ripoti hiyo kwa washirika mbali mbali iliziweze kutumika katika kupanga mipango yao ya maendeleo, kufanya maamuzi sahihi na kufanya tathmini ya miradi katika ngazi mbali mbali za utawala.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Wataalamu kupitia Ripoti hiyo wanaweza kuendesha mijadala itakayosaidia kuimarisha sera na mipango ya Taifa.
Alifahamisha kwamba hatua hiyo itachangia kuyafanya maisha ya Watanzania kuwa bora zaidi na hilo ndio lengo kuu la Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendesha Sensa ya Watu na Makazi.
“ Leo ni siku pekee kwa Watanzania na washirika wetu wamaendeleo ambao kwa pamoja tumeweza kuona matunda ya uwekezaji tulioufanya katika mchakato mzima wa mradi wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Albina Chuwa alisema idadi ya watu Tanzania imeongezeka mara tatu kutoka watu Milioni 12.3 mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012.
Dr. Albina Chuwa alisema Mkoa wa Dar es salaam pekee una watu Milioni 4.36 sawa na asilimia 10 kwa upande wa Tanzania Bara wakati Mkoa Mjini Magharibi una watu laki 593,678 sawa na asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar.
Alifahamisha kwamba Idadi ya watu kwa kilomita moja ya mraba Tanzania ni watu 51 kukiwa na tofauti kimkoa hali inayotoa sura halisi ya msongamano wa watu katika Mikoa ya Dar es salaam na Mjini Magharibi.
No comments:
Post a Comment