Na Rajab Mkasaba, Beijing China
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping katika siku yake ya pili ya ziara yake ya siku saba nchini China.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Wananchi mjini Beijing Dk. Shein na Rais Jinping walikubaliana kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano ulipo kati ya Zanzibar na China.
Katika kufanya hivyo viongozi hao wametaka nchi zao zitilie mkazo maeneo zaidi ya ushirikiano hasa biashara na uwekezaji, sekta ya uvuvi ambayo itajumuisha masuala ya utafiti, mafunzo na ufugaji wa samaki, sekta za elimu na afya pamoja na maeneo mengine yanayogusa ustawi wa watu wa nchi zao.
Rais wa China Xi Jinping ameeleza matumaini yake kuwa ziara ya Dk. Shein nchini China itaongeza msukumo na ari ya nchi mbili hizo kuwa karibu zaidi na kwamba anaamini kuwa Dk. Shein ni rafiki mkubwa wa watu wa China.
Amesema Serikali na wananchi wa China wana kila sababu ya kuuenzi na kuthamini uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar ambao ni sehemu ya ushirikiano wake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameishukuru Serikali na Wananchi wa China kwa misaada yao mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kwa Zanzibar.
Dk. Shein alimshukuru pia Rais Xi Jinping kwa kumualika kufanya ziara nchini mwake ziara ambayo sio tu imempa fursa ya kukutana na viongozi na wananchi wa China bali pia kujifunza kutoka kwao kutokana na uzoefu waliopata katika kujiletea Maendeleo.
Amesema ziara yake nchini China imekusudia kuimarisha na kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliodumu kwa miaka mingi kati ya China na Zanzibar ambao umejengwa katika misingi ya usawa na haki.
Alieleza kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano wake na China na kwamba makubaliano ya kupanua maeneo zaidi ya ushirikiano ni kielelezo halisi cha mahusiano mazuri kati ya nchi mbili hizo.
Katika mazungumzo hayo Shein alimueleza Rais wa China kuwa hivi sasa Serikali ya Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekuwa ikitekeleza vyema majukumu yake ya kuwatumikia wananchi na kwamba kumekuwapo na mafanikio katika nyanja mbalimbali.
Alibainisha kuwa hali ya utulivu wa kisiasa iliyopo Zanzibar hivi sasa imewezesha Serikali kutekeleza kwa umakini mipango ya Maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini- MKUZA na Ilani ya Uchagazi.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Li Yuanchao huko katika nyumba ya wageni wa Serikali mjini Beijing.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao wawili walizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Zanzibar.
Mazungumzo ya Dk. Shein na Rais Xi Jinping pamoja na Makamu wa Rais yalihudhuriwa na Mawaziri aliofuatana nao ambao Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Ardhi, Mkazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillah Jihad Hassan na Balozi Philip Marmo.
Rais anaendelea na ziara yake kesho ambapo atashiriki uzinduzi wa Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Biashara ya Beijing na baadae atasafiri kwenda Nanjing.
No comments:
Post a Comment