Na Masanja Mabula,Pemba
KESI 42 za makosa ya udhalilishaji wa wanawake na watoto yametokea katika wilaya ya Wete na kuripotiwa ofisi ya Dawati za jinsia na watoto la jeshi la polisi mkoa wa kaskazini Pemba kwa kipindi cha mwaka 2012.
Makosa hayo yanajumuisha vitendo vya utoroshaji, ubakaji na utelekezaji ambapo kati ya makosa hayo 21 yamefikishwa mahakamani huku matano yakiondolewa kutokana na sababu mbali mbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hizi ofisini kwake,Mkuu wa dawati la jinsia na watoto wa jeshi la polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Haji ametaja sababu zilizopelekea kesi hizo kuondolewa ni kukosa ushahidi na jamii kukubaliana kufanya suluhu.
Alisema kwamba, licha ya elimu inayotolewa kuhusiana na vitendo hivyo, lakini bado baadhi ya jamii inashindwa kuipokea kwa mtazamo chanya jambo ambalo linasababisha kuendelea kuwepo vitendo hivyo.
"Katika kipindi cha mwaka 2012, sisi kama dawati tulipokea kesi 42 na kesi 21 tulizifikisha mahakamani, lakini cha kushangaza baadhi ya jamii ilikubaliana kufutisha kesi huku baadhi ya nyingine zikikosa ushahidi kwani jamii haijawa tayari kushiriki katika kutoa ushahidi," alisema.
Naye Salama Juma Salum akifafanua juu ya masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto alisema dawati litaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuona kwamba vitendo vya aina hiyo vinapatiwa ufumbuzi.
Alisema tayari wameshafanya mikutano katika maeneo ya skuli ya mjini Wete na kupata mafanikio na sasa wanaelekeza nguvu zao katika sehemu za mashamba ambapo wanatarajia kuwatumia watu maarufu na viongozi wa dini ili kufanikisha suala hilo.
Aidha alitaja badahi ya mambo yanayochangia vitendo hivyo ni pamoja na masula ya utandawazi, kuporomoka kwa maadili pamoja na kukosekana malezi ya pamoja katika jamii.
Kwa upnde wake Mariam Abdalla Salim mwanaharakati kutoka Jumuiya ya wanawake Mkoa wa Kakskazini Pemba ameitaka jamii kuondoa muhali na kuwa tayari kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria pindi unapohitajika.
Alisema rushwa muhali ndiyo inayopelekea wanawake na watoto kudhalilishwa baada ya wao kukosa kujiamini.
No comments:
Post a Comment