Habari za Punde

Maalim Seif aiagiza Wizara ya kazi kusimamia utaratibu wa waajiri binafsi

Na Hassan Hamad OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameiagiza Wizara ya Kazi kusimamia utaratibu wa waajiri binafsi, ili kuhakikisha kuwa wanawapatia zote wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na malipo ya muda wa ziada.
 
Amesema serikali kwa upande wake imekuwa ikiendeleza utaratibu wa kuwapa malipo hayo wafanyakazi wake, lakini malalamiko mengi yamekuwa yakijitokeza kwa taasisi binafsi.
 
Maalim Seif ameeleza hayo viwanja vya Amaan mjini Zanzibar, wakati akifungua maonyesho ya nne ya biashara na huduma, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani “Mei day”, yanayotarajiwa kufikia kilele chake kesho.
 
Kuhusu maonyesho hayo Maalim Seif amesema ni muhimu katika kujifunza mbinu za kibiashara na kubadilishana uzoefu kwa wajasiriamali.

“Maonyesho ya biashara na huduma yana faida kubwa sana kwa wanaoonesha bidhaa, lakini pia yana faida kubwa kwa wateja ambao wanahitaji kujua bidhaa au huduma za aina gani zinapatikana wapi. Pia ni nafasi ya wateja kupata kujua na kulinganisha unafuu wa upatikanaji wa huduma hizo, kati ya watoaji tofauti”, alisisitiza Maalim Seif.
 
Amefahamisha kuwa katika maonyesho kama hayo ya biashara, watu hupata fursa ya kipekee ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika shughuli za uzalishaji, ununuzi na biashara kwa jumla, nahatimaye kuondoka wakiwa na mawazo na upeo mkubwa zaidi wa kibiashara na kiuchumi kutokana na mawazo na uzoefu walioupata kwa wengine.
 
Hata hivyo amesema jambo la muhimu kwa wazalishaji na watoa huduma ni kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa za viwango vya juu na kutoa huduma bora zitakazokwenda sambamba na ushindani wa kibiashara uliopo.
 
Katika hatua nyengine, Maalim Seif amezishauri taasisi za Umma kujipanga ili ziweze kushiriki kikamilifu katika maonyesho kama hayo kuanzia mwakani, 2014.
 
Mapema akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kazi, Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haji Omar Kheir, amesema lengo la maonyesho hayo ni kukuza ajira kupitia vyama vya ushirika.
 
Katika risala yao ya maonyesho, wafanyakazi hao wamesema wanakabiliwa na tatizo la sehemu maalum ya kufanyia maonyesho, na kuiomba serikali kuwasaidia kupata sehemu hiyo.
 
Maonyesho hayo yamevishirikisha vikundi 48 vya wajasiriamali kutoka Unguja na Pemba.

2 comments:

  1. Maalim umesema lakinivitendo hakuna kwani uliahidi mishahara yawafanyakazi wa Zanziba itakuwa mikubwa kuliko kwa wenzetu Tanganyika sasa kwanini humshauri huyu DR shen aboreshe hali ya maisha hapapetu inatisha

    ReplyDelete
  2. Maali..maalim, wale wale tu!
    Hana mpya yoyote, hebu muulize mamilioni wanayopata wabunge wake kila mwezi(kama mfuko wa jimbo)na milioni 200 za ruzuku ya chama zinatumiakaje?...kama hatowaambia wafuasi wake(Ba nchicha) kwamba unatumiwa kukihujumu chama.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.