Habari za Punde

Makampuni ya Hoteli ya Misali Pemba na Ocean View Zanzivar vyakabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu ya Taswa Zanzibar FC

UMOJA wa Makampuni ya hoteli za Zanzibar Ocean View, ambao ni wadhamini wakuu wa timu ya TASWA Zanzibar FC, jana ulikabidhi vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni tatu na laki nne, ili kuzidi kuiimarisha timu hiyo.

Vifaa vilivyotolewa katika hafla iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini Zanzibar, ni seti mbili za jezi, mipira miwili, soksi, nyavu za magoli pamoja na vizibao vya mazoezi (bibs).

Wakizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa hoteli hiyo Jacob Makundi na Mkurugenzi Michezo wa makampuni ya hoteli hizo Said Omar Kwimbi, walieleza matumaini yao kuwa mbali na kuijenga timu hiyo, vifaa hivyo vitakuwa njia ya kujitangaza zaidi na kuleta maendeleo ya michezo yote nchini.


Walieleza kuwa, waandishi wa habari za michezo, wana nafasi kubwa kusaidia harakati za kurejesha hadhi ya mpira wa miguu na michezo yote iliyoiletea sifa Zanzibar ambayo sasa ama imefifia au imekufa kabisa.

Walisifu wazo la kuundwa kwa timu hiyo, na kusema kama itasimama vyema, itaweza kufanya mambo makubwa siku zijazo, huku wakiahidi kuendelea kuiunga mkono ili iwe taasisi endelevu na yenye manufaa kwa wanamichezo na jamii ya Zanzibar kwa jumla.

Wakitoa shukurani zao, Mwenyekiti wa TASWA Zanzibar Mwinyimvua Nzukwi, nahodha wa timu Is-haka Omar na Mjumbe wa Bodi Emmanuel Magazi, walisema msaada huo ni muhimu katika jitihada zao za kujenga timu imara pamoja na dhamira ya kuimarisha michezo nchini.

1 comment:

  1. naona hapa kwetu znz tumekumbwa ba wimbi la mpira ili kuwapoteza watu kifikra , kuna mambo mengi ya kuchangia ya muhimu katika jamii yetu lakini kila unayemuona anachangia mpira, jee mnafikiri matakapokufa na kukutana na Mungu mtaulizwa kuhusu mipira?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.