Na Kunze Mswanyama, DSM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
Kisutu, imemwachia huru kwa masharti Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislam,
Sheikh Issa Ponda Issa na wenzake 49, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la
kuingia kijinai katika eneo la ardhi linalodaiwa kumilikiwa na Kampuni ya
Agritanza Limited.
Ponda na wenzake 49
walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya shilingi
milioni 59.6 , uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na kampuni
ya Agritanza Ltd na kujimilikisha isivyo halali.
Wakati Ponda akitiwa
hatiani na kuachiwa kwa masharti ya kutokutenda kosa lolote katika kipindi cha
mwaka mmoja, washatakiwa wenzake, wote 49 waliachiwa huru bila masharti baada
ya mahakama hiyo uwaona hawana
hatia kwa mashtaka hayo yaliyokuwa yakiwakabili.
Mahakama iliwaachia huru
baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha
mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Hakimu Mkazi wa mahakama
hiyo, Viktoria Nongwa aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, pia alimtaka Ponda awe
ni kiongozi wa kutunza amani katika jamii na asijichukulie sheria
mkononi.
Hakimu Nongwa alisema kwa
kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda mrefu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) kuzuia dhamana yake ni haki kuangalia muda huo.
“Hivyo mahakama chini ya
kifungu cha kifungu cha 25(g) cha kanuni za adhabu, mshtakiwa unaachiwa kwa
masharti ya kutokutenda kosa kwa miezi 12, unatakiwa ulinde amani na kuwa na
tabia njema katika jamii. Ukishindwa hiyo utarudi hapa kwa adhabu nyingine
inayokufaa,” alisema.
Awali Hakimu Nongwa
alichambua ushahidi wa mashahidi wote 16 wa upande wa mashtaka na ushahidi wa
mashahidi 53 wa utetezi akasema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha
mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Alifafanua kuwa upande wa
mashtaka umeshindwa kuthibitisha katika kosa la kwanza, la tatu na nne,
yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa wote na katika shtaka la tano lilolikuwa
likimkabili Ponda na mshtakiwa wa tano, Mukadamu Swalehe, ambaye ni kiongozi wa
taasisi na jumuiya za kiislam.
Katika shtaka la pili,
Hakimu Nongwa alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya
mshtakiwa wa kwanza tu, Ponda na kwamba kwa upande wa washtakiwa wengine
umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Alisema hakuna ushahidi
unaoonesha ni jinsi gani washtakiwa hao walivyohusika katika kosa hilo na kwamba hata kwa upande wa
mshtakiwa wa tano japo kuna maelezo ya onyo yanayoonesha kuwa alikiri, lakini
akasema maelezo ya onyo tu ya mshtakiwa hayatoshi kumtia hatiani ni lazima
upande wa mashtaka utoe ushahidi zaidi.
Alisema upelelezi
hakukufanyika kwa umakini kiasi kwamba kuna mambo ambayo hayakuwa wazi
yaliyoibuliwa na upande wa utetezi, ambayo kama upelelezi ungefanyika kwa
umakini basi washtakiwa wote wangetiwa hatiani.
“Katika kesi hii ni dhahiri
upelelezi haukuwa mzuri kwani kuna mambo mengi yaliyoibuliwa na upande wa
utetezi ambayo kama upelelezi ungefanyika vizuri, washtakiwa wote wangetiwa
hatiani,” alisema Hakimu.
Pia aliionya Jamhuri
kujiepusha na mashtaka ya kula njama ambayo hata yenyewe inajua kuwa ni vigumu
kuyathibitisha na kuishauri iwe inajikita katika mashtaka yanayoweza
kuthibitika kwa urahisi.
Ponda na wenzake
walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 18, 2012 na kusomewa mashtaka
manne wote kwa pamoja, huku yeye akikabiliwa na kosa lingine zaidi pekee yake.
Mashtaka hayo ya pamoja ni
kula njama, kuingia kwa jinai katika eneo la ardhi, kulikalia kwa nguvu eneo
hilo, na wizi wa vifaa vya ujenzi mali ya kampuni ya Agritanza.
Shtaka la ziada kwa Ponda
lilikuwa ni kushawishi kutenda kosa.
No comments:
Post a Comment