Na Mwantanga Ame
SIKU chache baada ya wauguzi kusherehekea siku yao, imebainika kuwepo viashiria vipya vya maradhi hatari vinavyoanza kujitokeza.
Hali hiyo imebainika baada ya wizara ya afya nchini kufanya uchunguzi wa kiafya katika wilaya mbali mbali za Unguja na Pemba.
Uchunguzi huo ulihusisha maradhi ya kansa ya shingo ya kizazi, kansa ya matiti, shinikizo la damu, kisukari na maradhi yasiyopewa kipaumbele.
Uchunguzi huo umegundua watu wenye matatizo mbali mbali ambayo yalikuwa bado hayajabainika.
Kati ya watu 380 waliofanyiwa uchunguzi huo kwa wilaya sita za Unguja, 18 walibainika kuwa na dalili za ugonjwa wa kansa ya shingo ya kizazi ikiwa ni sawa na asilimia 4.7.
Pia uchunguzi umebaini kuanza kuwepo dalili za ugonjwa wa kansa ya matiti, baada ya watu wanne ambao ni sawa na asilimia 1.0, kuonekana na ugonjwa huo ambao walilazimika kupelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.
Kwa wilaya ya kusini Unguja, uchunguzi huo ulifanywa kwa maradhi ya kifua kikuu na ukoma, ambapo uliwahusisha watu 94 ambapo 75 walionekana kuwa na matatizo mbali mbali ya kiafya, ikiwemo maradhi ya ngozi.
Waliobainika kuwa na maradhi ya ukoma ni watu saba, ambao ni sawa na asilimia 7.4 na kwa kifua kikuu ni watu 17 ambao ni sawa na asilimia 18.1, na watu wawili ambao ni sawa na asilimia 2.1 wamegundulika na dalili za ugonjwa wa moyo.
Muuguzi Mkuu wa hospitali kuu ya Mnazimmoja, Wanu Khamis Bakari, akizungumzia hali hiyo, alisema ni kweli kumekuwa na dalili za ongezeko la viashiria vya maradhi mapya ambayo ni hatari kwa binadamu.
Alisema uchunguzi uliofanywa, umeonesha ni kiasi gani umeweza kusaidia kugundua matatizo kwa watu ambao wanajisikia kuwa ni wazima huku wakiwa tayari wameathiriwa na ugonjwa mbali mbali.
Alisema ongezeko hilo la maradhi linaweza kumalizikia ikiwa jamii itapewa elimu zaidi juu ya umuhimu wa kupima afya zao.
Alisema ni vyema jamii ikajenga tabia ya kupenda kupima afya hatua ambayo inaweza kuwasaidia kupunguza ukali wa matatizo ya kiafya.
No comments:
Post a Comment