Na Kija Elias, Moshi
WANAFUNZI wa kike wa ngazi ya stashahada wilayani Moshi, wanalazimika kufanya biashara ya ngono kupata fedha za kujikimu baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kukataa kuwakopesha fedha wanafunzi wa ngazi hiyo.
Tatizo hilo pia linawakumba wanafunzi wa shahada ya kwanza ambao kwa mujibu wa Bodi hawana sifa za kukopeshwa.
Katibu wa Ofisi ya Rais katika serikali ya wanafunzi wa chuo cha ushirika na biashara Moshi (MUCCoBS), David Waryoba, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu, ngazi ya stashahada.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi wa ngazi ya stashahada ni kunyimwa mikopo hali inayowasukuma kuuza miili yao ili kupata fedha za kujikimu vyuoni.
Bodi ya wanafunzi ya elimu ya juu inatoa kipaumbele zaidi kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza.
Alisema chuo cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS), ambacho kina zaidi ya wanafunzi 700 wengi wa ngazi ya stashahada, wamekosa fursa ya kupata mikopo kutokana na serikali kutowapa kipaumbele.
“Tatizo liliko katika bodi ya mikopo ni kuwa ubaguzi mkubwa unaofanywa na bodi hiyo, mfano hapa MUCCoBS kuna zaidi ya wanafunzi 700 wa stashahada na shahada ambao wamekosa fursa ya kupata mikopo kutokana na serikali kutowapa kipaumbele, hili ni tatizo kubwa sana, linawafanya dada zetu kuwa makahaba,” alisema.
Alisema ipo haja kwa serikali kuliangalia suala hilo, kabla halijaleta athari kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho, Prof. Faustin Bee, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa tayari chuo kimeshakaa chini na uongozi wa serikali ya wanafunzi.
Prof. Bee alisema wanafunzi wote wanapata mikopo isipokuwa wa stashahada, ambao wanatakiwa baada ya kumaliza masomo yao kujiunga na shahada ya kwanza.
Akizungumzia suala la wanafunzi hao kujihusisha na biashara ya ngono, Prof. Bee alikiri kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu lakini akasema suala la kujiuza kwa wanafunzi hao halihusiani na tatizo la kukosa mikopo.
No comments:
Post a Comment