Kuwait kugharamia upembuzi yakinifu ujenzi bandari ya Maruhubi.
Pia kusaidia upatikanaji maji Mjini
Na Mwandishi maalum
Pia kusaidia upatikanaji maji Mjini
Na Mwandishi maalum
TANZANIA itanufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete nchini Kuwait.
Manufaa hayo kwa Tanzania yametangazwa katika mazungumzo rasmi na kati ya Rais Kikwete na Kiongozi wa Kuwait, Emir Sheikh Sabah Al Ahmad Al Jaber Al Sabah na katika mazungumzo na Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Kuwait wa Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (Kuwait Fund) Ghanim Sulaiman Al-Ghaniman.
Katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye kasri ya Bayan kabla ya kumwandalia dhifa ya kitaifa Rais Kikwete, kiongozi wa Kuwait aliahidi kuwa nchi yake itaisaidia Tanzania katika miradi yote ya maendeleo ambayo serikali ya Tanzania imeomba kuungwa mkono wakati wa ziara ya siku mbili ya kiserikali ya Rais Kikwete.
Emir alimwambia Rais Kikwete kuwa nchi yake tayari imetoa fedha za kufanyia upembuzi yakinifu wa ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahua katika mikoa ya Singida na Tabora na inafikiria kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo yenye kilomita 90 katika kiwango cha lami.
Ujenzi wa kipande hicho cha barabara ni sehemu ya barabara ya kilomita 700 ya kuunganisha Manyoni, mkoa wa Singida na Kigoma na ujenzi wake utakuwa umekamilisha kwa asilimia kubwa barabara hiyo muhimu kwa mawasiliano ya kutoka magharibi kwenda mashariki mwa Tanzania.
Mradi mwingine ambao Kuwait imekubali kufikiria kugharimia ni ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay ambayo ujenzi wake utakamilisha barabara ya Mtwara Corridor kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na hivyo kufungua eneo hilo la Tanzania kwa maendeleo.
Sehemu nyingine za Mtwara Corridor zinaendelea kujengwa, sehemu kubwa ikiwa inajengwa chini ya mradi wa Millenium Challenge Account (T) ambao unagharimiwa na serikali ya Marekani.
Kuwait pia imekubali kuchangia mradi mkubwa wa maji wa Mwanga-Same-Korogwe ambao unagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 56.
Mfuko wa Kuwait wa Maendeleo ya Nchi za Kiarabu utashirikiana na Mfuko wa Opec na Benki ya BADEA kutoa dola za Marekani milioni 20.4 kugharamia mradi huo wa kumaliza shida kubwa ya maji katika maeneo hayo.
Kuwait pia imekubali kugharimia upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya Maruhubi Zanzibar na kufikiria uwezekano wa kugharimia hatua kama hiyo ya mradi mkubwa wa kuongeza upatikanaji wa maji katika mji wa Zanzibar na maeneo yanayozunguka mji huo. Mfuko wa Kuwait ulianza shughuli zake rasmi katika Tanzania mwaka 1975, miezi sita tu baada ya sera ya mfuko huo kupanuliwa na kuruhusu mfuko huo kufanya shughuli zake nje ya nchi za kiarabu kama ilivyokuwa mwanzo na Tanzania ilikuwa moja ya nchi saba za mwanzo kunufaika na sera hiyo.
Tokea wakati huo, mfuko huo umegharimia miradi 12 ya maendeleo nchiniTanzania ukiwamo ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam-Kibiti hadi kwenye daraja la Mkapa ambalo pia liligharamiwa na mfuko huo.
Kuwait Fund inaendelea kuchangia ujenzi wa barabara ya Nyamwage-Somanga ambao ujenzi wake umebakiza kilomita chache kukamilika.
No comments:
Post a Comment