JESHI la Polisi Zanzibar limesema ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi unasababisha kurejesha nyuma juhudi za kupambana na biashara haramu za dawa.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam wakati akitoa hali halisi ya dawa za kulevya na hatua zinazochukuliwa na polisi katika kukabiliana na tatizo hilo.
Aliyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku nya upigaji vita matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya duniani iliyofanyika Sogea mjini hapa.
Alisema pamoja na jitihada za makusudi zinazochukuliwa na jeshi hilo lakini zimekuwa hazifii malengo kutokana na changamoto kadhaa.
Alisema jeshi la polisi linakabiliwa na tatizo la vifaa vya mawasiliano kama gari za kufanya doria, boti za doria bandarini, pikipiki na radio za mawasiliano.
Hata hivyo, alisema mazingira ya bandari ya Zanzibar ni tatizo katika kufanikisha kupunguza uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya sambamba na hali halisi ya kijografia ya visiwa vya Unguja na Pemba ambapo zaidi ya bandari 500 za kienyeji zipo.
Hivyo alisema kutokana na tatizo hilo polisi wanapata wakati mgumu kufikia maeneo ambayo yanahitajika kuangaliwa mara kwa mara.
Aidha alisema watendaji wa uwanja wa ndege wamekuwa na utaratibu mbaya wa kuwazuia maafisa wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya kufikia baadhi ya maeneo na kusema kitendo hicho hakiisaidii taifa katika vita hivyo.
Aidha alisema wapelelezi,waendesha mashtaka na mahakimu hawana elimu itakiwayo katika kusimamia kesi za dawa za kulevya kwa mujibu wa matakwa ya mikataba ya kimataifa.
Kamanda huyo alipendekeza kuanzishwa mahakama maalum ikiwa na mahakimu wake ambao watashughulikia tatizo hilo.
Pamoja na kuwepo changamoto hizo Kamanda alisema mwaka 20013 kuanzia Januari hadi Aprili wameweza kukamata kesi 24 za dawa ya kulevya zikiwemo kesi nane za bangi.
Hata hivyo alisema takwiwimu hizo hazihusishi kesi zinazokamatwa katika mikoa yote.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej alisema serikali kwa kushirikiana na tasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha tatizo hilo linaondoka au kupungua.
Aidha alisema miongoni mwa jitihada hizo ni kama vile marekebisho ya sheria namba 9 ya mwaka 2009.
Waziri Fereji katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema wakati umefika kwa jamii kuelewa kwamba dawa hizo ni sumu hivyo ni vyema kushirikiana kuwafichua wale wote waonahusika kwa njia moja au nyengine.
No comments:
Post a Comment