Habari za Punde

Dk. Shein aipa rungu ZECO • Ataka taasisi za umma zisizolipa zikatiwe huduma

Na Hafsa Golo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amelitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kufanya kazi bila hofu katika kufuatilia madeni ya wateja wao katika sekta mbali mbali zikiwemo Wizara na taasisi za serikali.

Dk. Shein alitoa kauli hiyo wakati akizindua mradi wa uimarishaji miundombinu ya ndani ya umeme katika kituo kikuu cha umeme Mtoni Wilaya ya Magharibi Unguja jana.

Dk.Shein alisema shirika hilo linapaswa kuhakikisha linadai madeni yake kwa kutumia busara na sheria zilizopo huku likihakikisha kutohofia kuzikatia huduma hiyo taasisi za serikali zanazoshindwa kulipa madeni.

Alisema haiwezekani kwa taasisi za serikali kushindwa kulipia huduma wakati zinapatiwa fedha za kulipia umeme.

Aidha aliwataka watendaji wa shirika hilo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata miongozo iliyopo ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.

Alisema sekta ya umeme ni muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote hivyo kufanikiwa kwa sekta hiyo ni dhahiri kuwa Zanzibar itaweza kuyafikia malengo ya mpango wa kupunguza umaskini (MKUZA) pamoja na Dira ya Maendeleo ya 2020.

Aidha alisema kuimarika kwa sekta hiyo kutaongeza idadi ya wawekezaji wa ndani na nje kama inavyoeleweka kuwa hivi sasa dunia ipo katika karne ya sayansi na teknolojia inayotegemea mahitaji ya umeme katika nyanja zake nyingi.

Dk.Shein alisema kumalizika kwa mradi huo kutaondosha tatizo la kukatika umeme mara kwa mara jambo lililokuwepo kwa muda mrefu kufuatia uchakavu wa miundombinu ya umeme iliyokuwepo awali.

Akitoa mfano Dk.Shein alisema mwanzoni mwa miaka ya 1980 matumizi ya umeme kwa Unguja yalikuwa ni megawati 3.5 tu ambapo jumla ya watumiaji wa huduma hiyo walikuwa ni 13,500.

Lakini kufikia mwaka 1989 matumizi hayo yaliongezeka hadi kufikia megawati 10 ambapo watumiaji walikuwa 24,500.

Dk.Shein alisema matumizi ya sasa kwa Unguja ni megawati 52 ambapo idadi ya watumiaji imefikia 94,000.
Nae Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada alisema serikali yake itaendelea kusaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali.

Alisema Japan na Zanzibar zimekuwa na uhusiano kwa takriban miaka 50 sasa hivyo uhusiano huo utaendelea kwa kusaidiana katika maendeleo ya wananchi wake.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema kukamilika kwa mradi huo kutaliondoshea lawama za mara kwa mara Shirika la Umeme kutoka kwa wateja.

Akitoa taarifa za mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Ali Khalil Mirza alisema mradi huo umegharimu shilingi bilioni 57 ambazo zilitolewa kwa pamoja kati ya Serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi walihudhuria.



1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.