Habari za Punde

Dk. Shein: Jiandaeni kutumia fursa miradi ya China.

Ataka watendaji wabadilike kufanikisha maendeleo

Na Mwantanga Ame
SERIKALI imewataka watendaji wake kujiandaa kufanikisha mradi mkubwa wa maendeleo,baada ya serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kukubali kusaidia Zanzibar miradi saba itakayoweza kusaidia kuchangia maendeleo katika sekta mbali mbali nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, baada kuwasili nchini akitokea China kwa ziara ya siku saba ya kiserikali.

Dk. Shein alisema Zanzibar na China, zimetiliana saini mikataba hiyo ambayo itabadili baadhi ya sekta ili kufikia malengo ya maendeleo ya nchi za uchumi wa kati, lakini ni lazima kutahitajika kuwepo mabadiliko kwa waliopewa jukumu la kusimamia shughuli za serikali.

Alisema rasimu hiyo ni ya kwanza kwa serikali ya Zanzibar kutoka China, ambayo itaifanya serikali kuandaa miradi itayosaidiwa na nchi hiyo kwa kila mwaka kupitia ubalozi mdogo wa China uliopo nchini.

Alisema makubaliano ya rasimu hiyo, haitaweza kuwa na maana ikiwa watendaji wa serikali watashindwa kujiandaa namna ya kutekeleza wajibu wao na ni lazima kuanzia sasa waone haja ya kubadilika.

Alisema katika hatua ya awali, Zanzibar itaweza kufaidika na mradi wa kuendeleza ZTEC, kwa kuimarisha miundombinu yake, mfumo wa E-gov afya, Zanzibar Smart, ambao utaifanya Zanzibar kuingia katika ramani ya nchi zenye maendeleo ya kati, ujenzi wa ICU na kitengo cha mfumo wa njia za chakula.

Miradi mingine aliyotaja ni pamoja na kuanzisha utafiti wa uvuvi wa bahari kuu na mifugo ambapo pia itawawezesha wavuvi kuvua katika bahari kuu na pia wawekezaji katika sekta ya utalii.

Alisema pia serikali hiyo inakusudia kusaidia eneo la kuimarisha kilimo, afya na kuunda udugu ambao utawawezesha viongozi wa baraza la manispaa kupata ujuzi wa namna ya kuendesha mji.

Kuhusu eneo la biashara, Dk. Shein, alisema nalo litaweza kupata msukumo baada ya baadhi ya wawekezaji kuonesha nia ya kutumia fursa za kuwekeza nchini, ambapo serikali inatarajia kupokea ujumbe wa watu 20 watakaoweza kuangalia maeneo watakayotumia kufanya uwekezaji wao.

Alisema pia kampuni ya Fujian Construction, imekubali kujenga nyumba za bei nafuu.

Alisema kuja kwa miradi hiyo kwa kiasi kikubwa kutaweza kuifanya serikali kuwa na mabadiliko katika maeneo tofauti ya kisekta.

Akizungumzia juu ya majengo ya historia, alisema ni kweli eneo hilo hivi sasa linahitaji kufanyiwa mabadiliko yatakayoweza kuifanya Zanzibar kukuza utalii wake pamoja na kuinua shughuli za wajasiriamali kutumia amajengo ya historia.

Dk. Shein, aliishukuru serikali ya China kutokana na mchango inayoendelea kuitoa kwa Zanzibar na kuahidi kushirikiana vyema na watendaji wanaoletwa nchini wakiwemo wa sekta ya afya.

Katika ziara hiyo Dk. Shein, alifuatana na mkewe mama Mwanamwema Shein, pamoja na baadhi ya Mawaziri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.