Habari za Punde

Mgombea huru ruksa

Rais apate asilimia 50+1
Ruksa kupinga ushindi
Umri wa rais miaka 40
Wananchi kumng’oa Mbunge asipowajibika
Mambo ya muungano yapunguzwa
Mawaziri kuthibitishwa na Bunge


Na Mwandishi wetu, DSM
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imependekeza mfumo wa serikali tatu nchini, ambazo ni Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na serikali Shirikishi.

Pia Tume hiyo imependekeza mfumo wa mgombea huru katika nafasi zote.

Akizungumza katika sherehe za unzinduzi wa rasimu ya katiba mpya yenye ibara 240 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba, alisema suala la muundo wa Muungano limechukua muda mrefu kujadiliwa na kuchambua maoni ya wananchi wote na kamwe halikuwa jambo rahisi.

Alisema hoja ya Muungano ilizungumza na wananchi wengi; wako waliotoa maoni ya serikali nne, serikali ya mkataba, serikali mbili, serikali tatu na wengine walisema Muungano uvunjwe kabisa.

Jaji Warioba alisema wananchi waliotoa maoni ya kuwepo muungano wa serikali moja hawakuwa wengi, lakini walitoa sababu za msingi za kuunga mkono hoja zao lakini baada ya kutafakari Tume iliona huu si wakati muafaka wa kupendekeza mfumo huo.

“Wapo waliopendekeza serikali nne (Unguja, Pemba, Tanganyika na Muungano) walikuwa na sababu zao lakini Tume haikuona uzito wa sababu walizotoa,” alisema.

Aidha alisema wapo waliopendekeza muungano wa mkataba na sababu zao zilikuwa na uzito lakini, wajumbe wa Tume waliridhika kwamba kabla ya kuingia kwenye muungano wa mkataba, muungano uliopo sasa lazima uvunjwe kwa kuwa haiwezekani kuwa muungano wa mkataba bila ya kuwa serikali mbili huru.

Tungefanya hivi, athari zake zinaweza kuvunja muungano uliopo sasa na kwa kuwa waliopendekeza mfumo huu (mkataba) walisisitiza muungano uwepo, hatukuwa na sababu ya kupendekeza hilo,” alisema Jaji Warioba.

Kuhusu mfumo wa serikali mbili, alisema pamoja na sababu nzuri zilizotolewa na kwa kuwa mfumo huo unahitaji ukarabati mkubwa ambao kamwe usingewezekana kufanywa, Tume imeona mfumo huo haufai.

Akizungumzia mfumo wa serikali tatu, alisema Tume imeangalia uzuri wake na changamoto zake na kusema ilichukua muda kwa wajumbe kuamua.

Alisema baada ya kufikiria na kugundua kuwa mfumo wowote una changamoto zake, Tume imependekeza mfumo wa serikali tatu.

Jaji Warioba alisema pia Tume imependekeza mambo ya Muungano yapunguzwe hadi kufikia saba, ambayo ni Katiba na Mamlaka ya Muungano, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu, Benki Kuu, Mambo ya Nje, Ushuru wa bidhaa zisizotokana na Muungano.

Aidha alisema serikali ya Muungano Tume imependekeza isiwe na Mawaziri wasiozidi 15.

Alisema Rais ataendelea kuchaguliwa na wananchi kwa kura na ili atangazwe kuwa mshindi lazima apate asilimia 50+1 ya kura badala ya utaratibu wa sasa ambapo mshindi anapatikana kwa kushinda wingi wa kura.

Kama itashindikana mshindi kupatikana katika duru ya kwanza, Tume Huru ya Uchaguzi itaitisha uchaguzi wa marejeo ndani ya siku 30 kwa wagombea wawili waliopata kura za juu.

Akizungumzia kupinga ushindi wa Rais, Jaji Warioba alisema Tume imependekeza ushindi wa Rais uhojiwe katika mahakama ya juu (Supreme Court) chombo kipya kilichopendekezwa na Tume hiyo, lakini atakaeruhusiwa kuhoji ni mtu aliegombea nafasi hiyo pekee na si vyenginevyo.

Chombo hicho (Supreme Court) kitakuwa chini ya Jaji Mkuu.

Kuhusu umri wa mtu kugombea urais, Tume imependekeza umri wa sasa uliomo kwenye katiba ubakie kama ulivyo, ambapo mgombea lazima awe na umri kuanzia miaka 40.

Akigusia madaraka ya Rais, alisema Tume imependekeza Rais abaki na madaraka yake ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, lakini kwa ngazi ya chini kazi hiyo itafanywa na Tume ya Utumishi wa umma.

Hata hivyo, baada ya kufanya uteuzi wa Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu, lazima uteuzi wao uthibitishwe na Bunge.

Kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Tume imependekeza Rais afanye uteuzi huo kwa kushauriana na chombo kipya kilichopendekezwa (Baraza la Ulinzi na Usalama) na uteuzi wa Makatibu Wakuu lazima ashauriane na Tume ya Utumishi wa Umma, ukiachilia mbali uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi ambae atathibitishwa na Bunge.

Jaji Warioba alisema, hata hivyo Rais ataendelea kuwa na kinga aliyonayo sasa lakini Bunge litaendelea kuwa na mamlaka ya kumuondoa madarakani.

Kuhusu Bunge, alisema Tume imependekeza Bunge liwe dogo lenye wajumbe 75 pekee, ambapo 50 watatoka Tanzania Bara na 20 watatoka Zanzibar na watano watateuliwa na Rais ambao watatoka kundi la watu wenye ulemavu.

Alisema wapiga kura watachagua wabunge wawili; mwanamke na mwanamme kutoka kila jimbo, hivyo Tume imendekeza kufutwa utaratibu wa sasa wa kuwepo Wabunge wa viti maalum.

Kuhusu ukomo wa Mbunge, alisema wamependekeza ukomo wa mtu kuwa Mbunge uwe vipindi vitatu, lakini kama wananchi hawaridhiki na uongozi wa Mbunge, wawe na mamlaka ya kumuondoa.

Alisema iwapo Mbunge atafariki, Tume imependekeza Tume Huru ya Uchaguzi isiitishe uchaguzi mdogo badala yake, kilichotoa Mbunge kiruhusiwe kuteua mtu wa kujaza nafasi hiyo, isipokuwa kama Mbunge huyo ni huru.

Kuhusu kiongozi wa Bunge, Jaji Warioba alisema Tume imependekeza Spika na Naibu Spika wasiwe viongozi wa vyama vya siasa wala wasiwe wanasiasa.

Lakini alisema Bunge litabaki na madaraka yake katika mihimili mitatu ya dola, na litaendelea kuwa na kinga ili Wabunge wawe huru wakiwa bungeni.

Kwa upande wa Tume ya Uchanguzi, Jaji Warioba alisema Tume imependekeza tume ya uchaguzi ibadilishwe na badala yake iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.

Alisema ya Tume Huru ya Uchaguzi yaunganishwe na majukumu ya Msajili wa Vyama vya Siasa huku sifa za wajumbe wa Tume hiyo ziwekwe kwenye katiba.

Alisema wananchi wanaotaka kuwa wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi, watawasilisha maombi yao kwa chombo maalum walichokipendekeza ambacho ni Kamati ya Uteuzi itakayoongozwa na Jaji Mkuu, ambayo ndio itachuja majina ya waombaji.

Kuhusu mahakama ya Kadhi, alisema Tume imeliondoa suala hilo kwenye katiba ya Muungano badala yake nchi washiriki wa Muungano wanaweza kulishughulikia hilo.

“Mahakama ya Kadhi inaweza kuwepo, lakini lisiingizwe kwenye katiba, Zanzibar wana mahakama ya Kadhi lakini haiko kwenye katiba yao,” alisema.

Kuhusu misingi mikuu ya taifa, Jaji Wariomba alisema taifa lolote lazima liwe na misingi na katiba ya sasa misingi hiyo iko kwenye utangulizi na kwamba misingi hiyo ni muhimu ibaki kwenye katiba.

Hata hivyo, misingi hiyo imependekezwa kuongezwa ambapo sasa itakuwa ni usawa, umoja, mshikamano, uhuru, haki, udugu na amani.

Kuhusu maadili ya viongozi, alisema maadili na miiko ya viongozi yawekwe kwenye katiba na kiundwe chombo maalum chenye madaraka ya kuchunguza maadili yao.

Hivyo, Tume imependekeza Sekretari ya Maadili ya Viongozi ibadilishwe iwe Tume yenye mamlaka kamili.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliipongeza Tume hiyo kwa kutekeleza kazi hiyo ngumu kwa uadilifu mkubwa.

Aidha aliwashukuru wananchi wa kutoa maoni yao kwa uwazi, yaliyochangia kupatikana rasimu ya katiba mpya.

Karibu watu milioni 1.3 walishiriki kutoa maoni yao nchi nzima pamoja na viongozi walio serikalini na waliostaafu 47.

1 comment:

  1. mmh huu ni ujanja wa wantanganyika , kujidai serikali tatu , sisi tunataka kuwa na serikali yetu huru na tanganyika serikali huru , halafu tushirikiane kwenye mambo yatayokubaliwa pande zote , sio kuungana tafadhali, kushirikiana na kuungana ni vitu tofauti. Halau ujanja wao mambo yote muhimu wameyaweka kwenye serikali ya muungano . Kama ni hivo basi serikali ya muungano iwe na wizara zifuatazo : kilimo , utalii , utamaduni, mifugo , afya , michezo , ustawi wa jamii na watoto .

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.