JIJI LA XIAMEN KUTUMA UJUMBE WA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA ZANZIBAR
Na Sauid Ameir, China
Meya wa jiji la Xiamen katika jimbo la Fujian nchini China Bwana Liu Keqing ameahidi, kabla ya mwisho wa mwaka huu, kupelekea Zanzibar ujumbe mzito wa wawekezaji na wafanyabishara kuangalia maeneo ya uwekezaji nchini.
Bwana Liu ametoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye yuko katika jiji hilo akimalizia ziara yake ya siku saba katika Jamhuri ya Watu wa China.
“Tutapeleka ujumbe mzito utakaojumuisha serikali, wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta ya viwanda vya kuunganisha bidhaa, samani, uvuvi na viwanda vya samaki, utalii ambapo watakuwemo makampuni ya kusambaza watalii na mahoteli na wengine”alieleza Bwana Liu.
Aliongeza kuwa atatumia uzoefu walioupata katika jiji hilo kushirikiana na Zanzibar kuinua sekta mbalimbali za uchumi zikiwemo za uvuvi, usafirishaji na utalii ambao kwa jiji la Xiamen ni sekta muhimu kwa kuwa kuwaingizia watalii wengi kwa mwaka.
“Mwaka jana tuliingiza watalii milioni 40”alieleza na kubainisha kuwa wengi wa watalii hao ni wa shughuli za mikutano na mafunzo pamoja na wale wanaokuja kuangalia vivutio vua kihistoria katika jiji hilo.
“Tulikuwa na mikutano 150 mwaka jana; tuna wastani wa mikutano 2 kwa siku huku tukiendesha semina na warsha zipatazo 2200 hivyo tunakuwa wageni wa namna hiyo”alisema Bwana Liu.
Meya huyo wa jiji la Xiamen alimueleza Rais wa Zanzibar kuwa uongozi wa jiji lake utahakikisha inaimarisha ushirikiano na Zanzibar kwani hilo ni jukumu lao kwa kuwa Rais Xi Jinping amesisitiza nchi yao kuimarisha ushirikiano na Zanzibar.
“Rais Xi Jinping alibainisha maeneo ya kushirikiana na nanyi (Zanzibar) kwa hiyo ni wajibu wa jiji la Xiamen kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais” alisisitiza.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimueleza Meya Liu kuwa ana matumaini makubwa kuwa ziara yake katika jiji la Xiamen itakuwa imeweka misingi madhubuti ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Xiamen kwa miaka mingi ijayo.
“Nimefurahishwa sana na mazungumzo yangu na watu mbalimbali niliokutana nao jana na leo asubuhi kwa kuwa yamenipa matumaini ya kuwa ziara yangu imeweka msingi bora wa ushirikiano katika Zanzibar na Xiamen”alisema Dk. Shein.
Halikadhalika alimueleza Meya Liu kuwa alipokuwa Benjing alikutana na Rais Xi na Makamu wa Rais Li Yuanchao na kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na China na kwamba yaliyofana sana.
“Nilipokuwa Beijing tulisaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya Uvuvi ambapo tunataka tuanzishe kituo cha kisasa cha utafiti wa masuala ya bahari na maliasili zake hivyo hili ni eneo ambalo Xiamen tunaweza kushirikiana”aliongeza
Dk.Shein amemueleza Meya huyo kuwa sekta ya utalii kwa Zanzibar ni sekta mama hivyo ni sekta ambayo angependa nayo kupewa nafasi muhimu katika ushirikiano na jiji la Xiamen hasa kwa kuzingatia jiji hilo lina uzoefu mkubwa kwenye sekta hiyo.
Baada ya mkutano na Meya wa Xiamen Rais na Ujumbe wake ulitembelea kisiwa cha utalii cha Gulangyu na kujionea shughuli za utalii katika kisiwa hicho pamoja na kutembelea makumbusho ya muziki wa Piano.
Kabla ya kwenda kisiwani humo wajumbe wengine katika msafara wa Rais wakiongozwa na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yusuf Mzee walitembelea ukumbi wa manesho wa Xiamen uliopo katikati ya jiji la Xiamen ambamo walijifunza historia ya maendeleo ya jiji hilo.
Wajumbe wengine walikuwa ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillah Jihad Hassan, Msaidizi wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa,Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Balozi wa Tanzania China Balozi Philip Marmo, Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji. Alikuwepo pia Balozi Mdogo wa China Zanzibar Bibi Chen Qiman.
No comments:
Post a Comment