Habari za Punde

Skuli za Wakulima ziwe mkombozi kilimo chenye tija.

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasaili Zanzibar Affan Othman Maalim, akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu kilimo cha mpunga, mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
 Mkulima wa Migomba katika kijiji cha Kangani, Makame Kombo, akitoa maelezo ya kilimo hicho, mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wakulima wa mpunga katika bonde la Mfubaha Vitongoji, wakati wa ziara yake kwa Wizara ya Kilimo Kisiwani Pemba. (Picha na OMKR).
 
 
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Dhana ya “Mapinduzi ya kilimo” iliyoasisiwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein, inazidi kupata umaarufu na mafanikio baada ya serikali kupitia Wizara ya kilimo na maliasili, kuamua kuanzisha skuli za wakulima wa mazao na mifugo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
 
Lengo kuu la kuanzishwa kwa skuli hizo ni kuwapa ujuzi wakulima na wafugaji ili waweze kuendeleza kilimo na mifugo kwa ufanisi zaidi na kuongeza kipato chao, sambamba na kuipunguzia serikali mzigo wa kuagiza mchele kutoka nje ya nchi.
 
Katika ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kwa Wizara ya Kilimo na Maliasili Kisiwani Pemba mwisho mwa mwezi wa Mei, 2013, ilibainika kuwa jumla ya skuli 532 zimeanzishwa kisiwani Pemba, 280 kati ya hizo zikiwa za mazao na 252 za mifugo.
 
Miongoni mwa mazao yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na mpunga, muhogo, migomba, viazi na uatikaji wa miche ya mikarafuu. Kwa upande wa mifugo iliyopewa kipaumbele ni pamoja na ng’ombe, mbuzi na kuku.
Skuli hizi zinakwenda sambamba na kile watendaji wa Wizara ya Kilimo na Maliasili wanachokiita “utafiti shirikishi” ambao huanzia katika vituo vya kilimo kwa majaribio, na baadae kuwashirikisha wakulima katika maeneo yao kwa lengo la kuendeleza utafiti huo katika maeneo tofauti ya kilimo na mifugo.
 
Utafiti wa haraka haraka unaonesha kuwa utafiti shirikishi kwa wakulima unaleta manufaa makubwa, baada ya wakulima wenyewe kukiri na kuthibisha juu ya ubora za mbegu na huduma zitolewazo na Wizara ya kilimo ikilinganishwa na zile mbegu za asili.
 
Katika kituo cha Gombeume Mchangamdogo kwa mfano, ilibainika mbegu ya mpunga wa “nerika” nambari 1, 4, na 7 zinakua vizuri zaidi ikilinganishwa na mbegu za asili. Katika kituo hicho mbegu hizo za utafiti zinatarajiwa kuvunwa katika kipindi cha miezi mitatu, huku zile mbegu za asili zikitazamiwa kavunwa katika kipindi cha miezi mitano hadi sita.
 
Mbali na kipindi kifupi cha mavuno kwa mbegu za kisasa, mazao pia huwa mazuri na mengi ikilinganishwa na kilimo cha zamani, ambapo hata soko lake linakuwa la uhakika zaidi.
 
Wanafunzi wa skuli ya wakulima wa mpunga katika kituo cha Kichokochwe Kambini Wilaya ya Wete, walibainisha kuwa mafunzo wanayopatiwa ni mazuri na yamekuwa yakiwasaidia sana katika kuendeleza kilimo cha mpunga.
 
Wanasema wamekuwa wakipatiwa mafunzo kuanzia namna ya kuchagua mbegu bora, upandaji, utumiaji wa pembejeo na mchakato mzima wa kuendeleza kilimo hicho hadi kufikia wakati wa mavuno. “Kwa kweli mafunzo haya yanatusaidia sana na hata upaliliaji wake ni rahisi, tofauti na tulivyokuwa tukilima hapo awali ambapo tulikuwa tukilazimika kung’oa jani moja baada ya jengine, lakini sasa tunaweza kupatililia hata kwa kutumia jembe dogo kwa kilimo hiki cha kitaalamu”, alisema mkulima mmoja wa eneo hilo wakati wa ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
 
Hata hivyo alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni kutopatikana mbolea kwa wakati, ambapo Wizara ya Kilimo ilikiri juu ya tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi, ili mbolea ya kutosha iweze kupatikana kwa wakati katika misimu ijayo ya kilimo.
 
“Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais, ni kweli msimu huu tulichelewa kidogo kuwapatia mbolea wakulima. Hii ilitokana kuchelewa kwa makampuni tunayoyatumia kutuletea mbelea hiyo, lakini hivi sasa ninavyokwambia mbolea tayari ipo katika maghala yetu ambayo itatumika kwa msimu ujao, lakini pia tumeanza kutayarisha tenda    na kuzitangaza mapema iwezekanavyo, ili mbolea iweze kufika mapema zaidi”, alisema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Affan Othman Maalim.
 
Affan alisema katika muktadha wa “Mapinduzi ya Kilimo” Wizara imekuwa ikitekeleza kwa vitendo azma ya serikali ya kuwawezesha wakulima kwa kuwapunguzia gharama za pembejeo ambapo bei ya mfuko wa mbolea imepunguzwa kutoka shilingi 70,000 hadi 10,000.
 
Katika ziara hiyo pia ilibainika kuwepo kwa maendeleo mazuri ya kilimo cha migomba, muhogo, viazi vitamu na uatikaji wa miche ya mikarafuu ambapo Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali kuangalia kilimo hicho, na kuelezea kufurahishwa na maendeleo yaliyopatikana.
 
Maalim Seif alifika Makangale kuangalia kilimo cha viazi vitamu, Kangani kuangalia kilimo cha Migomba, Mjimbini kukagua vitalu vya miche ya mikarafuu, bonde la Mfubaha Vitongoji kuangalia kilimo cha mpunga na Mfikiwa kukagua kilimo cha muhogo.
 
Mafanikio ya wazi yalionekana kwa mfugaji Hamad Juma Hassan wa Kinyasini Pemba ambaye sasa ananufaika na mradi wa gesi “biogas” itokanayo na kinyesi cha ng’ombe awafugao yeye mwenyewe. Gesi hiyo anaitumia kwa shughuli mbali mbali zikiwemo kupikia na kuonea, na hivyo kuepukana kabisa na matumizi ya kuni na vibatari.
 
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, sasa nimepata nishati mbadala ambayo ninatumia kwa kupikia vyakula vyote pamoja na kuonea, ni nishati nzuri na inawezekana kuipata na kuitumia, nawaomba wafugaji wenzangu wafuatilie utaratibu huu ili watumie nishati hii mbadala isiyoharibu mazingira”, alisema Hamad Juma, mfugaji wa ng’ombe katika eneo la Kinyasini.
 
Kupitia ziara hiyo Maalim Seif pia alijionea jinsi wakulima walivyohamasika kuatika miche ya mikarafuu na baadae kuiuzia serikali kwa bei ya shilingi 1000 hadi 1500 kwa mche. Baada ya serikali kuuziwa miche hiyo huigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa kukuza na kuendeleza kilimo cha mikarafuu ambacho kilionekana kupoteza hadhi.
 
Kwenye majumuisho ya ziara hiyo yaliyofanyika kituo cha mafunzo ya amali Vitongoji, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, aliwasisitiza wakulima kuzingatia na kuyatumia vyema mafunzo wanayopatiwa kupitia skuli za wakulima, ili waweze kujikomboa na kuipunguzia serikali mzigo wa kuagizia mchele kutoka nje.
 
Alisema licha ya kuwepo na upungufu mkubwa wa mabwana na mabibi shamba, lakini iwapo wataalamu waliopo watatumika vizuri, mafanikio makubwa zaidi ya kilimo yanaweza kupatikana Zanzibar.
 
“Utafiti shirikishi na mashamba darasa yote yana lengo la kumpa utaalamu mkulima na mfugaji wa Zanzibar, kwa hivyo itumieni vyema taaluma munayoipata kuendeleza kilimo ambacho ndio kitakuwa mkombozi wetu” alisisitiza Maalim Seif na kuhitimisha ziara yake kwa kuiagiza Wizara ya Kilimo pamoja na mambo mengine kufanya utafiti kwa kila shehia ili kujua mahitaji wa pembejeo kwa shehia husika.
 
Uanzishwaji wa Skuli za wakulima ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dhana ya “Mapinduzi ya Kilimo” na itafanikiwa zaidi ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.