Habari za Punde

Washauri kuwepo Mahakama ya Ardhi

 Mkuu wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo akifungua warsha ya sera ya Taifa ya Ardhi iliyowashirikisha Masheha wa Wilaya hiyo. Kushoto ni Mratibu wa Mradi wa SMOLE Saleh Kombo na kulia ni mkufunzi wa warsha Mlenge Hassan.
Masheha wa wilaya ya kusini wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya Haji Makungu Mgongo (hayupo pichani) alipokuwa akifungua warsha ya sera ya ardhi katika afisi ya Wilaya Makunduchi. (Picha na Ramadhani Ali- Maelezo Zanzibar)
 
Na Ramadhani Ali – Maelezo                      
 
Masheha wa Wilaya mbili za Mkoa wa Kusini Unguja wameshauri kuwepo Mahakama ya Ardhi na kitengo cha usajili wa Ardhi kuanzia ngazi ya wilaya katika Sera mpya ya ardhi inayoandaliwa ili kupunguza migogoro mingi inayoikabili sekta hiyo.
 
Ushauri huo wameutoa katika Warsha ya kuelimisha na kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya sera ya Taifa ya Ardhi iliyoandaliwa na Mradi wa usimamizi endelevu wa ardhi na Mazingira (SMOLE) awamu ya pili Afisi ya Wilaya Kusini Makunduchi na  Halmashauri ya Wilaya ya Kati Dunga.
 
Wamesema matatizo ya ardhi hasa vijijini yamekuwa makubwa na ufumbuzi wake huchukua muda mrefu kutokana na kukosa vitengo vinavyoshughulikia ardhi na Mahamakama ya ardhi katika ngazi za Wiaya.
 
“Kesi zinazohusu ardhi ni nyingi na mahakama ya ardhi ipo mjini hili ni tatizo kubwa hivyo sera mpya inayoandaliwa ifikirie kuanzisha mahakama za ardhi kuanzia ngazi ya Wilaya,” alisema Sheha wa Chwaka Msaraka  Pinja.
 
Katika Sera mpya ya Ardhi  inayotayarishwa, Masheha wa Wilaya ya Kusini  na Kati wamependekeza sheria za ardhi ambazo hivi sasa zinasimamiwa na  taasisi  tano ziwekwe katika taasisi moja ili kupunguza urasimu katika kuzitekeleza.
Taasisi hizo ni Idara ya Ardhi na Usajili,  Idara ya Misitu na Mali  zisizohamishika,Idara ya  Mipango miji na vijiji, Idara ya upimaji na ramani na Idara ya   Mazingira.
 
Sheha wa shehia ya Mzuri Khamis Ramadhani ameshauri sheria za ardhi  zilizopo zifanyiwe mapitio upya na ikiwezekana zipunguzwe kwani hivi sasa ni nyingi na utekelezaji wake unapelekea kuwa  mgumu.
 
Aidha viongozi hao wa shehia wametaka sera ya ardhi iweke wazi idadi ya Eka ambazo mtu mmoja anatakiwa azimiliki kwa shughuli za  maendeleo na  watu wanaojikusanyia maeneo makubwa ya ardhi yachukuliwe na kupewa watu ambao hawana ardhi.
 
“Kuna baadhi ya watu wanamiliki mashamba makubwa kila sehemu na wala hawayatumii, wakati umefika yachukuliwe na serikali na wapewe wananchi wengine  kwa shughuli za kilimo na maendeleo mengine,” alipendekeza sheha Mumeangu.
 
Aidha wameishauri Serikali kuanzisha majengo ya ghorofa na tabia ya kuuziwa ardhi wageni  ama kukodishwa kwa miaka mingi iachwe na wamependekeza kipindi cha kukodishwa  ardhi kisizidi miaka 20.
 
Mratibu wa mradi wa SMOLE  Saleh Kombo amewaeleza viongozi wa Wilaya hizo mbili kwamba serikali kwa kushirikiana na serikali ya Finland  imo katika mchakato wa kutayarisha Sera  rasmi ya ardhi katika kusimamia ardhi ndogo iliyopo  ikiwa ni  juhudi  za kupunguza umaskini kupitia MKUZA awamu ya pili na amewashauri kushiriki kikamilifu katika mchakato huo.
 
Amesema Serikali imechukua uwamuzi huo kwa kujua kuwa  ardhi  ni rasilimali kubwa katika nchi na ardhi ya  Zanzibar imekuwa ikipungua kwa kasi kutokana na mmongonyoko wa fukwe wakati idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi. 

1 comment:

  1. Tatizo la migogoro ya ardhi Z'bar linasababishwa na uzembe wa watendaji wa serikali.

    Z'bar ni ndogo, watu wote wanajuana tokea enzi na enzi, nani kwao wapi na eneo lao ni lipi.

    Baada ya mapinduzi serikali ikaamua kufanya mambo ya ajabu kwa kuigawa ardhi kienyeji bila ya kuiwekea kumbu kumbu.

    Siku moja nilimuuliza mdau mmoja juu ya kumbu kumbu za nyumba, viwanja na mashamba ya serikal i yakiwemo yale ya 'eka'..akaniambia "Hakuna kumbukumbu ya mpaka kati ya Z'bar na tanganyika, wewe unaliza eka?..kwa mara ya kwanza michoro ya mpaka kabla ya muungano ililetwa na al-marhum ALI NABWA"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.