Habari za Punde

UNFPA yawafunda vijana ujasiri

Na Salum Vuai, Maelezo
ILI vijana waweze kupata mustakbali mzuri wa maisha, wametakiwa kuepuka vishawishi, kujitambua, kujiamini na kuwa na malengo.

Nasaha hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Islam Seif Salum, alipokuwa akizungumza na vijana wa taasisi mbalimbali, katika warsha ya siku moja iliyofanyika hoteli ya Chavda mjini Zanzibar.

Katika warsha hiyo iliyolenga kuwapatia elimu vijana walio katika rika la mpito majaribu, Dk. Islam alisema, lazima vijana wajitoe muhanga wakati wakiwa maskuli na vyuoni, ili waweze kufikia ngazi za juu kielimu.

Alisema, elimu ndio ufunguo wa mafanikio, hivyo ni lazima itafutwe kwa kila hali, kwani bila ya hivyo, familia na jamii zitashindwa kujikomboa na umasikini, ambao unazidi kulipa taifa changamoto mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.

Alifahamisha kuwa, kijana akitambua kuwa familia yake ni masikini, ndipo pahala pazuri na kujifunga mkaja ili achimbe hazina ya elimu, kwa lengo la kuikomboa familia yake.

“Familia inapokuwa katika hali ya umasikini, na baadhi ya ndugu wakashindwa kwenda mbali kielimu, lazima atokee mmoja ajifunge na apige moyo konde, ili awe mkombozi na mfano kwa ndugu zake wengine,” alifafanua.

Aidha, alisema kutafuta elimu ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu na dhamira ya dhati ili kufikia malengo mtu anayokusudia.

Akitoa mada kuhusu mambo yanayowahusu vijana katika ngazi ya kimataifa na kikanda, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) Dorothy Temu, alisema iko haja kwa vijana kupatiwa elimu juu ya namna bora ya kufanya maamuzi wanapokwazwa na mambo tafauti.

Alisema zaidi ya thuluthi moja kwenye tatu (1/3) ya idadi ya watu wanaoishi katika nchi za kusini kwa jangwa la Sahara ni vijana hasa kuanzia miaka kumi hadi 24, ambao wanatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 420 mwaka 2025, kufikia 650 ifikapi mwaka 2050.

Alieleza kuwa asilimia 60 ya watoto wa eneo hilo, ni vigumu kwenda skuli, kutokana na familia zao kuishi katika mazingira magumu ya umasikini, na kujikuta wakilazimika kujiingiza kati ajira za watoto ili kupata mahitaji yao na familia zao.

Baadhi ya vijana walioshiriki warsha hiyo, ambao ni kutoka Unguja na Pemba, waliitaka serikali kuweka sheria zaidi za kuwalinda watoto na vijana, na kuzitekeleza ipasavyo, ili vijana na watoto waweze kupata haki zao pale wanapotendewa vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Walieleza masikitiko yao kwamba, baadhi ya watendaji waliopewa dhamana ya kuzisimamia sheria, ndio wa kwanza kuzipinda na kuwatetea watu waovu wanaowafanyia watoto udhalilishaji wa kijinsia, na hivyo kuwafanya waishi katika hali ya kukata tamaa na kutengwa na jamii.

Warsha hiyo iliyokuwa na mada mbalimbali, imefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani na kushirikisha vijana kutoka asasi mbalimbali Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.