Habari za Punde

Bulembo:Viboko lazima

Na Kija Elias, Hai
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Abdallah Bulembo ameagiza kuendeleza adhabu ya viboko kwa wanafunzi wote wanaosoma katika shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo nchini ili kurudisha nidhamu mashuleni.

Bulembo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Wari iliyoko katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na kusema suala la viboko katika shule za wazazi ni lazima.

Alisema malezi kwa vijana hivi sasa yameporomoko kutokana na wazazi kutowajibika ipasavyo hali ambayo imemesababisha vijana wengi kutowaheshimu walimu na wakati mwingine mzazi amekuwa akidiriki kumwadhibu mwalimu eti kisa kampiga mtoto wake.

“Suala la viboko kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za wazazi lazima ili kumweka katika malezi mazuri, maana hata sisi tulichapwa viboko ndiyo maana leo hii mnapotuona hapa ni kutokana na malezi tuliyolelewa na wazazi wetu na ndio maana tumefika hapa tulipo hivi sasa,”alisema Bulembo.

“Sisi wazazi tunasema huwezi kuendelea kuwalea wanafunzi kama ambavyo wazazi wao wanavyotaka, na kama mzazi anaona kuwa mwanae hawezi kuchapwa viboko amwondoe hapa,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya wanafunzi hawalipi ada na akatoa agizo kwa wanafunzi wote ambao hawajalipa karo ya shule kuondoka katika maeneo ya shule hizo ili kutafuta shule ambazo zinapokea wanafunzi wasiokuwa na ada.

“Katika hili nitakuwa mkali kweli mwanafunzi asiyelipa ada aanze kufungasha mizigo yake akatafute shule ambayo wanasoma bure, mwalimu anayefundisha hapa kama hajalipwa mshahara wake wamekuwa wakija makao makuu na kudai mishahara yao na hata wakati mwingine wamekuwa wakitushitaki kwa nini leo hii mwanafunzi anayesoma hapa asilipe ada,” alihoji.

Bulembo yuko mkoani Kilimanjaro katika ziara ya kukagua uhai wa chama na jumuiya zake sambamba na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM.

1 comment:

  1. viboko sio dawa ya kuleta nidhamu ndugu yangu , nidhamu inapatikana kwa tabia nzuri na uadilifu wa mwalimu na wazazi wenyewe , kwani mtoto ni sawa na kompyuta ambayo ni tupu haijatiwa softwares , kwa hio mtoto huchukua tabia kutokana na wazazi na walimu na wale wanaomzunguka.Hakuna anazaliwa mwizi au mtoro ila ni mazingira humfanya mtoto kuwa mwizi iwapo mahitaji muhimu hapewi , kwanini kwa mfano umpige mtoto kama amekula chakula chako ulichopika kumwekea mumeo? kwa nini yeye mtoto hana haki? na kama kaiba ni kwa ajili ya njaa sio kwa ajili anapenda kuiba , hii ni asili ya kibinadamu ambayo inatuwezesha tuishi , njaa ni tatizo kubwa kwa watoto wetu , hutoroka shule kwenda kujitafutia vipato au riziki , viboko sio dawa ya nidhamu ndugu yangu wee , na kama ingeukwa hivyo tusingekuwa na haja ya kuwa na maegereza , kila mhalifu apigwe viboko aachiwe

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.