Habari za Punde

SMZ kujenga kiwanda cha kusarifu mwani


Na Asya Hassan, Hafsa Golo
WIZARA ya Biashara,Viwanda na Masoko Zanzibar inafanya mazungumzo na Shirika la Viwanda Vidogo la Umoja wa Mataifa (UNIDO) ili kujenga kiwanda cha kusarifu zao la mwani, kitakachosaidia wakulima kuwa na soko la uhakika la zao hilo.

Waziri wa wizara hiyo, Nassor Ahmed Mazrui aliyasema hayo wakati akijibu hoja za Wawakilishi waliochangia bajeti ya wizara ya Uvuvi na Mifugo.

Alisema jopo la wataalamu kutoka UNIDO wapo nchini kufanya mazungumzo na wizara, yatakayotoa nafasi ya kiwanda hicho kujengwa.

Mazrui aliwataka wakulima wa mwani wawe wastahamilivu wakati serikali yao ikiendelea na mikakati madhubuti ya kumaliza kilio chao.

Alisema ujenzi wa kiwanda hicho utatoa nafazi kwa Zanzibar kutosafirisha mwani ghafi nchi za nje badala yake itasafirisha mazao yanayotokana na mwani.

Akizungumzia suala la kuku kutoka Brazil, Waziri huyo alisema sheria za biashara za kimataifa zinawabana kupiga marufuku uingizaji wa kuku hao lakini pia uzalishaji wa ndani bado ni mdogo na haukidhi mahitaji ya soko ikiwemo sekta ya utalii.

Aidha alisema kwa kuwa Zanzibar ni kivutio cha utalii, watalii wengi wanaokuja nchini huhitaji kuku, hivyo iwapo kuku hao watapigwa marufu kutakuwa na upungufu mkubwa na hao wanaozalishwa ndani watapanda bei mara dufu kiasi kwamba wananchi watashindwa kuwanunua.

Wajumbe wa Baraza hilo wamekataa kupitisha bajeti ya Wizara ya mifugo na uvuvi wakiilazimisha serikali kupiga vita uingizwaji wa kuku hao nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.