Habari za Punde

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria

                                     HOTUBA YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA


MHE. ABUBAKAR KHAMIS BAKARY (MBM) KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA

                                                                             2013/2014

UTANGULIZI
1. Mhe. Spika, sasa naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako tukufu likae kama Kamati ya Matumizi ili liweze kupokea, kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2013/14.

2. Mhe. Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu aliyetuwezesha kukutana tena leo hii, kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yanayohusu mipango yetu ya maendeleo. Tunamuomba atupe hekima na uwezo wa kuyafanikisha hayo kwa faida ya nchi yetu, Amin!

3. Mhe. Spika, kabla ya kuwasilisha taarifa za Wizara yangu naomba nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wake makini, ambao umeleta heshima kubwa kwa nchi yetu.

4. Mhe. Spika, naomba pia kutumia nafasi hii kuwapongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, kwa utendaji wao makini na ushauri wanaompa Mheshimiwa Rais, ambao bila shaka unasaidia kuleta ustawi wa nchi yetu. Napenda pia niwashukuru viongozi hawa kwa kutupa muongozo mzuri pamoja na maagizo yao ya busara ambayo yamesaidia sana katika Wizara yangu kutekeleza vizuri zaidi majukumu yake.

5. Mhe. Spika, naomba pia ruhusa yako ili nikupongeze wewe binafsi kwa kuliongoza Baraza letu kwa upeo na uwezo mkubwa, ambao umelijengea hadhi kwa wananchi. Vile vile, napenda kuwapongeza Wajumbe wa Baraza hili kwa kutekeleza vyema majukumu yao. Aidha, nawapongeza watendaji wa Baraza kwa kufanya kazi zao kwa umahiri.

6. Mhe. Spika, baada ya pongezi hizo, naomba ruhusa yako ili nitoe shukurani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Kamati zote za Baraza kwa kutekeleza majukumu yao kwa umakini. Aidha, naomba kutoa shukurani maalum kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala iliyomaliza muda wake chini ya uongozi wa Mhe. Ali Abdalla Ali, kwa kuishauri vizuri Wizara yangu. Aidha, nachukua fursa hii kuikaribisha Kamati mpya ya Katiba, Sheria na Utawala, inayoongozwa na Mheshimiwa Ussi Jecha Simai. Vile vile, napenda kuishukuru Kamati ya PAC iliyomaliza muda wake kwa kufanya kazi nzuri kwenye Wizara yangu, na tunaikaribisha kwa dhati PAC mpya chini ya uongozi uliokomaa wa Mheshimiwa Omar Ali Shehe. Tunatarajia Kamati hizo na nyengine, zitaendelea kutushauri ipasavyo katika kipindi kinachofuata. Mimi pamoja na watendaji wa Wizara yangu tunawaahidi ushirikiano wa dhati.

7. Mhe. Spika, pamoja na shukrani hizo naomba niwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Mgogoni kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha majukumu yangu ya uwakilishi katika jimbo letu, na kwa kunivumilia wakati wote ninapokosekana jimboni kutokana na majukumu ya kitaifa. Natumai tutaendelea kushirikiana ili kuharakisha maendeleo ya jimbo letu.

HALI YA UPATIKANAJI WA FEDHA

8. Mhe. Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara ya Katiba na Sheria iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 7,591,000,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 4,393,130,052.00 zilipangwa kulipia mishahara na stahiki mbali mbali za watumishi na Shilingi 3,197,869,948.00 kwa matumizi mengineyo. Hadi kufikia mwezi Machi 2013 Shilingi 4,909,058,935.00 zilikuwa zimepatikana. Kati ya fedha hizo, Shilingi 3,051,545,020.00, ambazo ni 76%, ni kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi, Shilingi 1,373,038,809.00 (47%) kwa matumizi mengineyo, na 484,475,106.00 (71%) ni Ruzuku. Kwa kazi za maendeleo, Shilingi 6,682,200,000.00 ziliidhinishwa. Kati ya hizo, Shilingi 3,455,000,000.00 ni mchango wa Serikali na Shilingi 3,227,200,000.00 ni msaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kufikia Machi 2013, Shilingi 1,657,552,527.00 zilikuwa zimepatikana, ambapo Shilingi 1,468,913,527.00 sawa na 43% ni mchango wa Serikali na Shilingi 188,639,000.00 (6%) zilitoka kwa Washirika wa Maendeleo. Wizara pia ilikadiria kukusanya Shilingi 447,000,000.00 ili kuchangia mapato ya Serikali. Hadi Machi 2013, fedha zilizokusanywa ni Shilingi 288,708,060.00, sawa na asilimia 65%. Angalia Viambatanisho nam. 1&3.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA 2012/13

9. Mhe. Spika, Wizara ya Katiba na Sheria inatekeleza miradi ya maendeleo ifuatayo:- (i) Programu ya Mabadiliko ya Sekta ya Sheria; (ii) Mradi wa Kuimarisha Taasisi za Wizara unaohusisha Utafiti wa Matumizi ya Sheria za Zanzibar, Utafiti Kuhusu Uwezekano wa Kuanzisha Kituo cha Utamaduni cha Kiislamu, na Utayarishaji wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini; (iii) Mradi wa Marekebisho ya Mfumo wa Usajili wa Biashara na Uimarishaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali; (iv) Mradi wa Marekebisho ya Mfumo wa Usajili wa Matukio ya Kijamii; (v) Mradi wa Mapitio ya Sheria za Zanzibar; (vi) Mradi wa Matengenezo ya Majengo ya Mahkama; (vii) Mradi wa Kuanzisha Mahkama ya Biashara; (viii) Mradi wa Kuimarisha Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka; (ix) Mradi wa Ujenzi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; na (x) Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Katiba na Sheria. Utekelezaji wa miradi hii ni kama ifuatavyo:-

10. Mhe. Spika, kazi ya kuandaa Mkakati wa Mabadiliko katika Sekta ya Sheria imefikia hatua ya kutayarishwa rasimu ya mwanzo ambayo inatarajiwa kupelekwa kwa wadau. Kazi hii inaratibiwa na Kamati Simamizi inayohusisha wajumbe 10 kutoka katika baadhi ya taasisi za Sheria Zanzibar. Vile vile Wizara kwa kushirikiana na UNDP imo katika hatua za kumpata Mratibu wa Programu ya Mabadiliko katika Sekta ya Sheria, ili kazi ya kukamilisha matayarisho ya mkakati na utekelezaji wake vifanyike kwa ufanisi zaidi. Washirika wengine katika Programu hii ni UNICEF, na Jumuiya ya Ulaya.

11. Mhe. Spika, Utafiti wa Matumizi ya Sheria za Zanzibar umefanyika ili kubainisha Sheria zilizopitwa na wakati miongoni mwa Sheria za Zanzibar. Utafiti huo unafanywa na wataalam wa ndani na rasimu ya mwanzo ya utafiti huo iko tayari na inatarajiwa kujadiliwa na wadau hivi karibuni. Vile vile matayarisho ya Mfumo wa Ufatiliaji na Tathmini yamefanywa kwa kutumia wataalamu wa ndani. Hatua iliyofikiwa ni kupata ripoti ya mwanzo ambayo tayari imekwishajadiliwa. Mtaalam bado anaendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wahusika ili kujiandaa na kuwasilisha ripoti ya mwisho ya kazi hiyo. Mfumo huu utakapokamilika utarahisisha upatikanaji wa taarifa zitakazowezesha kupima ufanisi wa kiutendaji wa Idara na Taasisi za Wizara. Kwa upande mwingine, Utafiti wa Kuanzisha Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu unatarajiwa kuanza wakati wowote zitakapokamilika taratibu za kumpata mtaalamu na fedha.

12. Mhe. Spika, Mradi wa Marekebisho ya Mfumo wa Usajili wa Biashara una lengo la kurekebisha mfumo wa usajili wa taasisi za biashara na tasnia ya mali za ubunifu (Industrial Property Automation System - IPAS) na kufanya marekebisho ya sheria zinazosimamia usajili. Sheria zinazohusika ni Sheria ya Kampuni (Companies Decree Cap. 153) na Sheria ya Ufilisi (Insolvency Decree Cap. 20). Rasimu ya Sheria mpya ya Kampuni tayari imejadiliwa kwenye vikao vinavyohusika, ikiwemo Baraza la Mapinduzi. Matayarisho ya Rasimu ya Sheria mpya ya Ufilisi yanaendelea. Vile vile, Kanuni za Sheria ya Tasnia za Mali za Ubunifu imekamilika na itawasilishwa kwa Shirika la Kimataifa la Mali za Ubunifu (World Intellectual Property Organization (WIPO) na Shirika la Mali za Ubunifu la Afrika (Africa Regional Intellectual Property Organization’ (ARIPO), kwa ajili ya kupata maoni.

13. Mhe. Spika, Mradi wa Uimarishaji Usajili wa Matukio ya Kijamii ulianza mwaka 2010, na unagharamiwa na Serikali pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNFPA. Chini ya Mradi huu, Mfumo wa Usajili wa Kielektroniki umeanzishwa na matayarisho ya kutunga Sheria ya Usajili wa Matukio ya Kijamii yanaendelea. Rasimu hiyo imejadiliwa kwenye vikao vinavyohusika ikiwemo Baraza la Mapinduzi.

14. Mhe. Spika, Mradi wa Matengenezo ya Majengo ya Mahkama, kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, ulihusisha kuendelea na matengenezo ya sehemu ya nje ya Jengo la Mahkama Kuu Vuga, kazi ambayo inaendelea. Jengo la Mahkama ya Kadhi Mwanakwerekwe limefanyiwa matengenezo kwa kuongezwa urefu wa kuta zake, kuezekwa na kutiwa umeme. Kwa upande mwingine, matengenezo ya Mahkama ya Chake Chake na Makunduchi hayakuweza kufanyika kutokana na upungufu wa fedha.

15. Mhe. Spika, Mradi wa Kuanzisha Mahkama ya Biashara ulihusisha matengenezo ya jengo na kutungwa kwa Sheria. Hadi kufikia sasa Sheria imepitishwa Baraza la Wawakilishi. Hata hivyo, Mahkama ya Biashara haitaweza kuanza kazi katika mwaka wa fedha 2013/14 kutokana na ukosefu wa bajeti. Tunatarajia Mahkama hiyo itasaidia kupunguza mzigo wa kesi kwenye Mahkama za kawaida, na pia kuyashughulikia kwa haraka na umakini zaidi mashauri yanayohusu biashara.

16. Mhe. Spika, Mradi wa Kuimarisha Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mwaka 2012/13 ulikusudia kuwapatia makaazi Waendesha Mashtaka wanaopelekwa kufanya kazi kwenye Mahkama za Wilaya ili wawe karibu na vituo vyao vya kazi. Hivi sasa Mradi huo unakamilisha ujenzi wa nyumba iliyopo Madungu Pemba na umeanza ujenzi wa nyumba ya Makunduchi ambayo imefikia hatua ya kuezekwa. Maandalizi ya nyumba ya Mkokotoni yameanza katika hatua ya kupata kiwanja na kutayarisha michoro.

17. Mhe. Spika, Mradi wa Ujenzi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu ulikusudia kuipatia Afisi ya Mwanasheria Mkuu jengo jipya kwa ajili ya shughuli za Ofisi. Ujenzi umefikia hatua za kazi za kumalizia, zikiwemo kuweka mifumo ya usalama, udhibiti wa moto na mawasiliano. Matarajio ni kukamilisha ujenzi na kuhamia katika mwaka wa fedha 2013/14.

18. Mhe. Spika, Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Wizara ulianza April 2012 katika eneo la Mazizini Unguja. Mradi huu una lengo la kuiwezesha Wizara kuwa na Jengo la kisasa litakalotosha kwa matumizi ya Ofisi za Wizara na taasisi zake. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Novemba 2013, ikiwa fedha za ujenzi zitapatikana kama tulivyokubaliana. Kama hilo litawezekana jengo hili litakuwa ni moja ya miradi itakayofunguliwa kwenye Sherehe za Mapinduzi yetu matukufu ya 1964 kufikia miaka 50, na kuwa moja ya vielelezo vya mafanikio ya Mapinduzi hayo. Ujenzi huo umefikia ghorofa ya tano na jumla ya Shilingi 2,513,832,424.00 zimetumika kumlipa mjenzi.

UTEKELEZAJI WA IDARA NA TAASISI ZA WIZARA

19. Mhe. Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba nitoe maelezo ya utekelezaji wa shughuli za Wizara yangu kwa mwaka 2012/13 kwa kuangalia maendeleo ya taasisi moja moja kama ifuatavyo:-

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI

20. Mhe. Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu Mipango, Sera na Utafiti, pamoja na kutekeleza shughuli za kila siku. Katika mwaka wa fedha wa 2012/13, Idara imetekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

21. Mhe. Spika, Idara imeratibu maandalizi ya ripoti na taarifa mbali mbali za utekelezaji na kuziwasilisha kunakohusika. Idara pia imeratibu maandalizi ya Bajeti ya Wizara pamoja na maandiko ya miradi sita na kuyawasilisha Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Angalia Kiambatanisho Nam. 4.

22. Mhe. Spika, Miongoni mwa majukumu ya Idara hii ni kuratibu shughuli za NGOs. Katika mwaka wa fedha 2012/13 Idara imefanya mapitio ya Sheria ya Jumuiya Zisizo za Serikali (Nam. 6 ya 1995). Rasimu ya Sheria hiyo imejadiliwa kufikia ngazi ya Kamati ya Uongozi ya Wizara. Mapendekezo ya Kamati ya Uongozi yamezingatiwa na sasa rasimu hiyo inatarajiwa kurejeshwa tena kwenye Kamati kwa maamuzi. Aidha, Idara imeanza kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Sera ya NGO’s ya mwaka 2009 kwa kuanza uhakiki wa NGOs zilizosajiliwa Zanzibar. Kazi hiyo imefanyika katika Wilaya nne za Unguja ambapo jumla ya NGOs 43 zimehakikiwa. Katika mwaka ujao wa fedha, kazi hiyo itaendelea Mkoa wa Mjini Magharibi na Kisiwani Pemba. Lengo la uhakiki huo ni kujua kwa usahihi Jumuiya zilizo hai ili kuziondoa zile ambazo haziwajibiki ipasavyo kwa mujibu wa sheria, na kuweka mikakati ya kuziimarisha Jumuiya zinazofanya kazi zake vizuri na zinazowajibika kisheria.

23. Mhe. Spika, katika kuimarisha uwezo wa Wizara kiutendaji, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imetoa mafunzo kwa njia ya Semina kwa Maafisa Mipango na Wahasibu wa Taasisi za Wizara, ili kuwajengea uwezo katika utengenezaji wa malengo na shabaha za kibajeti. Kwa upande mwengine, katika kujiimarisha, Idara imewapatia mafunzo watumishi wake watatu.

24. Mhe. Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iliidhinishiwa Shilingi 172,860,000.00. Hadi kufikia Machi 2013, Shilingi 65,244,700.00 zimetumika kwa malipo ya mishahara na stahiki nyengine za watumishi na Shilingi 41,709,200.00 kwa matumizi mengineyo. Shilingi 787,200,000.00 ziliidhinishwa kwa kazi za Maendeleo na hadi kufikia Machi 2013, fedha zilizopatikana ni Shilingi 237,251,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 48,612,000.00 (30%) ni kutoka Serikalini na Shilingi 188,639,000.00 (30%) kutoka kwa washirika wa maendeleo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

25. Mhe. Spika, katika mwaka 2013/14 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha Uratibu wa Sera, Mipango, Miradi ya Maendeleo na Ripoti za Utekelezaji;

ii. Kukamilisha Waraka wa Mkakati wa Mabadiliko Katika Sekta ya Sheria;

iii. Kufanya utafiti wa taarifa za msingi za sekta ya Sheria (baseline study); na

iv. Kutayarisha Sera ya Msaada wa Huduma za Kisheria Zanzibar (Legal Aid Policy).

26. Mhe. Spika, ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kutekeleza majukumu yake katika mwaka 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 184,152,000.00 kwa matumizi ya kawaida, zikiwemo Shilingi 94,596,000.00 za mishahara, na Shilingi 89,556,000.00 za matumizi mengineyo. Vile vile, naomba Baraza liidhinishe Shilingi 1,454,313,000.00 kwa kazi za maendeleo, zikiwemo Shilingi 150,000,000.00 kutoka Serikalini.



IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI

27. Mhe. Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi ina dhamana ya kusimamia na kuratibu shughuli zote za Uendeshaji na Utumishi zinazofanywa ndani ya Wizara na Taasisi zake. Katika mwaka wa fedha wa 2012/13, Idara imeendelea kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

28. Mhe. Spika, katika kuimarisha uwezo wa kuratibu masuala ya utumishi na kusimamia uendeshaji, Idara imeanzisha Kamati ya Utumishi ya Wizara. Kamati hiyo inajumuisha Maafisa Utumishi na inaendelea kukutana na kuratibu masuala ya kiutumishi, ikiwemo miundo ya utumishi na madaraja ya wafanyakazi, matayarisho ya nominal roll, mipango ya mafunzo, uajiri na utunzaji wa kumbukumbu za ofisi na za wafanyakazi.

29. Mhe. Spika, Idara kupitia kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, imekamilisha ukaguzi katika taasisi zote za Wizara, Unguja na Pemba. Ripoti za Ukaguzi wa Ndani za Julai – Septemba na Oktoba - Disemba 2012/13 zimeshawasilishwa kwenye Kamati ya Ukaguzi ya Wizara. Ripoti ya Januari – Machi 2013 iko kwenye hatua za kukamilishwa.

30. Mhe. Spika, Idara kupitia kitengo cha uhasibu imefanikisha kazi ya kurekebisha vifungu vya matumizi baada ya Marekebisho ya Bajeti ya Wizara; kutoa ufafanuzi wa Hoja za Ukaguzi wa Ndani na Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, na kutoa Ripoti ya Upatikanaji wa Matumizi ya Fedha kwa vifungu vya Wizara.

31. Mhe. Spika, Idara imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Manunuzi wa Wizara kwa kununua vifaa na huduma mbali mbali kwa mujibu wa sheria ya Manunuzi Nam. 9 ya 2005. Aidha, Idara imeendesha mafunzo ya siku mbili kwa Wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Wizara, kuhusu Sheria na Taratibu za Manunuzi, pamoja na utunzaji na uwekaji Kumbukumbu za Mali za Serikali. Katika kipindi cha Julai 2012 - Machi 2013, Idara imeandaa vikao tisa vya Bodi ya Zabuni.

32. Mhe. Spika, taratibu za kuanzisha data base ya Wafanyakazi wa Wizara zimeanza kwa kuhakiki na kupitia Mafaili ya Wafanyakazi. Kazi ya kuingiza taarifa kwenye data base inatarajiwa kuendelea katika mwaka wa fedha wa 2013/14. Aidha, Idara imeanza hatua za kutayarisha Mpango wa Rasilimali Watu wa Wizara (Human Resource Plan) kwa kukusanya na kuhakiki taarifa za awali. Matayarisho kamili ya mpango yanasubiri muongozo kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Pamoja na kazi hiyo, Idara inafanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa Wizara, na tayari imeandaa Mpango wa Mafunzo wa mwaka mmoja.

33. Mhe. Spika, hali ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Idara na Taasisi za Wizara. Hivi sasa Wizara ina jumla ya wafanyakazi 797 wakiwemo wanawake 293 na wanaume 504. Idadi ya wafanyakazi wenye elimu ya Stashahada au zaidi ya hapo ni 33% ya wafanyakazi wote. Angalia Viambatanisho 9a-c.

34. Mhe. Spika, katika kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara, Idara imesomesha Wafanyakazi 12; mmoja Shahada ya pili, mmoja shahada ya kwanza, watatu Stashahada ya Uzamili, watano stashahada, na wawili cheti. Kati ya watumishi hao wanawake ni saba na wanaume ni watano. Aidha, Idara imo katika hatua za kukiimarisha Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara na kwa kuanzia imeajiri Afisa Mawasiliano atakayefanya kazi za kitengo hicho. Idara pia inaendelea kuimarisha tovuti ya Wizara kwa kuingiza kumbukumbu.

35. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Idara ya Uendeshaji na Utumishi iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 566,653,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 314,343,000.00 zilitengwa kwa malipo ya mishahara na stahiki za Watumishi na Shilingi 252,310,000.00 kwa matumizi mengineyo. Hadi kufikia Machi 2013, zilipatikana Shilingi 228,011,820.00 (73%) kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi, na Shilingi 116,289,299.00 (46%) kwa matumizi mengineyo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

36. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/14, Idara ya Uendeshaji na Utumishi inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha uratibu wa majukumu ya Rasilimali Watu;

ii. Kuimarisha uratibu wa kazi za utawala za Wizara; na

iii. Kuimarisha miundo mbinu ya kutoa huduma.

37. Mhe. Spika, ili Idara ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza majukumu yake, naomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 591,141,000.00 kwa kazi za kawaida, zikiwemo 338,831,000.00 kwa mishahara na 252,310,000.00 kwa matumizi mengineyo.



MAHKAMA

38. Mhe. Spika, Mahkama ndicho chombo chenye jukumu la kikatiba la kusimamia utoaji wa haki. Katika kufanikisha jukumu hilo usikilizaji wa kesi za jinai, madai, pamoja na rufaa za jinai na madai ni jambo la msingi. Katika mwaka wa fedha 2012/13 Mahkama imepokea na kusajili kesi 6,039 kutoka Mahkama zote, Unguja na Pemba. Angalia Viambatanisho 5a&b.

39. Mhe. Spika, kutoka Julai 2012 hadi Machi 2013, Mahkama Kuu imepokea mashauri mapya 237, na kuifanya iwe na jumla ya mashauri 492, ukijumuisha na mashauri 255 yaliyopokelewa kabla. Katika kipindi hicho, Mahkama Kuu imetoa uamuzi kwa mashauri 16. Katika Divisheni ya Mahkama ya Kazi, yamepokelewa Mashauri mapya 6, na kuifanya Divisheni hiyo iwe na mashauri 31 kwa kujumuisha na mashauri 25 yaliyosajiliwa kabla. Mahkama hiyo imetoa uamuzi kwa mashauri 2.

40. Mhe. Spika, katika Mahkama za Mkoa, mashauri mapya 291 yamepokelewa na kufanya Mahkama hizo ziwe na jumla ya mashauri 720, kwa kujumuisha na mashauri mengine 429 yaliyosajiliwa kabla ya kipindi hicho. Katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013, Mahkama za Mikoa zimetolea maamuzi mashauri 21. Wakati huo huo, Mahkama za Wilaya zilipokea mashauri mapya 1,927 na kufikisha jumla ya mashauri 2,890, yanapojumuishwa na mashauri 963 yaliyosajiliwa kabla. Katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013, Mahkama hizo zimetolea uamuzi mashauri 875.

41. Mhe. Spika, katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013, Mahkama ya Kadhi wa Rufaa imepokea mashauri mapya 63, na kuifanya iwe na jumla ya mashauri 78, yanapojumuishwa na mashauri 15 yaliyosajiliwa kabla. Mashauri 37 kati ya hayo yametolewa uamuzi. Vile vile, Mahkama za Kadhi wa Wilaya zilipokea mashauri mapya 1222, na kuwa na jumla ya mashauri 1852, baada ya kujumuishwa na mashauri 630 ya siku za nyuma. Baina ya Julai 2012 na Machi 2013 Mashauri 311 yametolewa uamuzi.

42. Mhe. Spika, katika Mahkama za Mwanzo mashauri mapya 2263 yamepokelewa na kufanya Mahkama hizo kuwa na jumla ya mashauri 2711 yanapojumuishwa na mashauri 443 yaliyosajiliwa kabla. Kuanzia Julai 2012 hadi Machi 2013, mashauri 1502 yametolewa uamuzi.

43. Mhe. Spika, Mahkama ya Rufaa ya Tanzania ilianza mwaka wa fedha 2012/13 ikiwa na idadi ya mashauri 134 yaliyosalia kutoka miaka ya nyuma na kupokea mashauri mapya 5 na hivyo kufanya idadi ya mashauri kufikia 139. Aidha katika kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013 Mahkama ya Rufaa ya Tanzania imetolea uamuzi mashauri 133.

44. Mhe. Spika, tathmini hiyo inatuonyesha kwamba kwa wastani Mahkama zetu zimeweza kutoa uamuzi kwa kesi 2,897 kati ya kesi 8,913 ambayo ni jumla ya kesi 6,039 zilizofunguliwa katika mwaka wa fedha 2012/13 na kesi 2,874 zilizosajiliwa kabla ya kipindi hicho. Kiwango hiki ni kidogo na hakiridhishi. Kwa sababu hiyo, Wizara yangu kupitia Mahkama inachukua hatua za kufanya mabadiliko yatakayoongeza ufanisi wa kazi za Mahkama. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuharakisha uendeshaji wa kesi ili haki za walalamikaji na walalamikiwa zipatikane kwa wakati, kwani kuichelewesha haki ni kuikataa. Kamati maalum imeundwa kushughulikia uharakishwaji wa kesi, na Kamati hiyo imefanya vikao viwili katika mwaka 2012/13, kujadili mbinu zinazoweza kusaidia kupunguza muda wa kuendesha kesi. Hatua nyengine ni kuanzishwa Mahkama za kushughulikia mambo maalum kama ilivyo kwa Mahkama ya Watoto na Mahkama ya Biashara; na kuongeza idadi ya mahakimu. Katika mwaka huu wa fedha 2012/13 Mahkama imeajiri wafanyakazi zaidi ya 30, wakiwemo mahakimu.

45. Mhe. Spika, Mahkama ya Watoto ilizinduliwa mwezi Februari 2013 kwa ajili ya kushughulikia mashauri yanayohusu watoto. Tangu kuanza kazi Mahkama hiyo imemaliza kesi saba na kuzitolea uamuzi kati ya kesi 56 zilizoanza kusikilizwa.

46. Mhe. Spika, pamoja na juhudi hizo, Mahkama imeipitia Sheria ya Mahkama ya Kadhi Nam. 3 ya 1985. Rasimu ya sheria hiyo imekamilika na inatarajiwa kuwasilishwa kwenye Kamati ya Makatibu Wakuu hivi karibuni. Kupitishwa kwa sheria hiyo kutaleta mabadiliko makubwa ya utendaji wa Mahkama ya Kadhi.

47. Mhe. Spika, kwa upande mwengine Mahkama imewajengea uwezo baadhi ya Majaji na Mahakimu kwa kuwawezesha kushiriki katika mikutano, makongamano na semina Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Afrika ya Kusini. Aidha, Mahkama imewapatia nafasi ya kuongeza elimu wafanyakazi wa Unguja na Pemba, katika ngazi ya stashahada na cheti kwenye fani za Sheria, Uongozi na Kompyuta.

48. Mhe. Spika, katika kuelimisha jamii, Mahkama imeendelea kurusha vipindi vya elimu kupitia ZBC ambapo vipindi vinne vya televisheni na vitatu vya radio vimetolewa. Vile vile, toleo la kwanza la Jarida la Mahkama limechapishwa na kusambazwa kwa wasomaji. Uzinduzi wa Jarida hilo umefanywa kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, tarehe 7/2/2013. Aidha, Mahkama imefanya mikutano minne ya hadhara kuzungumza na wananchi katika baadhi ya maeneo.

49. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Mahkama iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 3,145,000,000.00 kwa kazi za kawaida na Shilingi 600,000,000.00 kwa kazi za maendeleo kutoka Serikalini. Vile vile, jumla ya Shilingi 72,000,000.00 zilikadiriwa kukusanywa ili kuchangia mapato ya Serikali. Hadi kufikia Machi 2013, Shilingi 1,657,639,000.00 (70%) zilitumika kulipia mishahara na stahiki nyingine za watumishi, na Shilingi 344,843,836.00 (43%) kwa matumizi mengineyo. Kwa kazi za maendeleo, Shilingi 100,000,000.00 (17%) zilipatikana. Angalia Kiambatanisho Nam. 1&3.

50. Mhe. Spika, katika mwaka 2013/14 Mahkama imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kupunguza mrundikano wa kesi na kuongeza ufanisi katika utowaji wa haki.

ii. Kuyafanyia matengenezo majengo ya Mahkama Unguja na Pemba.

51. Mhe. Spika, ili Mahkama iweze kutekeleza malengo yake mwaka 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 3,583,000,000.00 kwa matumizi ya kazi za kawaida, zikiwemo Shilingi 2,350,100,000.00 za mishahara na Shilingi 1,232,900,000.00 za matumizi mengine. Vile vile, naomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 150,000,000.00 kwa kazi za maendeleo. Aidha, Mahkama inatarajia kuchangia Serikalini mapato ya Shilingi 90,000,000.00. Angalia Viambatanisho Nam. 2&3.



AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR

52. Mhe. Spika, jukumu la msingi la Afisi ya Mwanasheria Mkuu (AMM) ni kuishauri Serikali kwa mambo yote ya kisheria. Katika kutekeleza wajibu huo AMM inafanya kazi ya kutayarisha miswada ya Sheria, kusimamia kesi na mashauri ya madai kwa niaba ya Serikali, kuandaa hati na nyaraka za kisheria, kutoa ushauri wa kisheria kuhusiana na Mikataba ya Serikali, na kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi za Serikali.

53. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, AMM imetayarisha Miswada 10 ya Sheria ambayo imewasilishwa Baraza la Wawakilishi. Angalia Kiambatanisho Nam. 6. Aidha, AMM imeandaa na kuchapisha matangazo 81 ya kisheria na kanuni 20 za sheria mbalimbali, na imesimamia mikataba 23 kwa ajili ya Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Wakati huo huo, Afisi inaendelea kusimamia kesi 45 za madai zilizofunguliwa dhidi ya Serikali.

54. Mhe. Spika, AMM imeandaa mikakati ya uimarishaji wa usimamizi wa kesi za madai za Serikali kwa kukutana na Watendaji Wakuu wa baadhi ya taasisi za umma kujadili suala hilo. Hatua inayofuata ni kujiimarisha zaidi katika usimamizi wa kesi.

55. Mhe. Spika, pamoja na kazi hiyo, AMM imepanga kuziweka pamoja na kuzichapisha sheria za Zanzibar. Kazi hiyo imeshaanza siku za nyuma. Kwa mwaka 2013/14, AMM imekusudia kuzishughulikia Sheria za mwaka 1980 – 2010. Afisi imekamilisha mazungumzo na kampuni za uchapishaji sheria za Law Africa ya Kenya na Law Publisher ya India ili kuangalia uwezekano wa kuzichapisha sheria zote katika mfumo wa elekroniki na karatasi. Kazi hiyo ikikamilika Zanzibar itakuwa na toleo jipya la Sheria za Zanzibar. Toleo la mwisho kama hilo lilitoka mwaka 1958.

56. Mhe. Spika, katika hatua nyengine, AMM imekamilisha kazi ya upembuzi wa sheria ili kubaini sheria zinazotumika na zisizotumika, na sasa imo katika maandalizi ya Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria Zisizotumika. Vile vile, AMM inaendelea kuandaa Sheria mpya kuchukua nafasi ya baadhi ya Sheria za zamani za kiingereza zilizoanza kutumika wakati wa ukoloni na ambazo sasa zimepitwa na wakati. Wataalamu wanaofanya kazi hiyo wamekamilisha hatua za awali. Hatua iliyobaki itakamilika mwaka wa fedha 2013/14. Sheria zinazofanyiwa kazi ni Sheria ya Hati ya Uwakala (Power of Attorney Act), Sheria ya Wasimamizi wa Amana na Wasii (Trustees Act), na Sheria ya Tafsiri na Masharti ya Jumla Namba 7/84, (Interpretation and General Clauses Act) na Sheria ya Kusimamia Hundi (Bill of Exchange Act). Aidha, Afisi inakusanya na kuyaweka pamoja Magazeti Rasmi ya Serikali kutoka 1910 hadi 1963, ili kuzihifadhi kumbukumbu muhimu zilizomo, kama vile Kumbukumbu za Vikao vya Baraza la Kutunga Sheria la wakati huo (LEGCO).

57. Mhe. Spika, ili kuimarisha utaratibu wa kazi ya kuandaa Miswada ya Sheria, AMM imeandaa Muongozo wa Uandaaji wa Miswada. Muongozo huo ambao uko katika hatua za mwisho kukamilishwa, utaweka bayana taratibu za kuandaa Miswada. Aidha, Muongozo utaweka mfumo mmoja wa uandishi wa miswada, kulingana na aina za miswada.

58. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, AMM imetimiza moja kati ya malengo muhimu kwa kukamilisha Sheria ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu, ambayo ilipitishwa na Baraza hili kwa kauli moja. Utekelezaji wa sheria hiyo utaanza baada ya taratibu zinazohusika kukamilika. Afisi tayari inayo Dira na Mpango kazi wa utekelezaji wa sheria hiyo.

59. Mhe. Spika, katika kujenga uwezo kiutendaji, AMM imeajiri wafanyakazi 12 wakiwemo wanasheria wapya sita na wengine wanne wamepatikana kutoka taasisi nyengine za Serikali ili kuongeza ufanisi. Vile vile Afisi imewapatia nafasi za masomo wafanyakazi wawili katika ngazi ya Shahada, na mmoja ngazi ya Stashahada. Aidha, wafanyakazi watatu wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi kuhusu Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi na watano wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi Afirika ya Kusini, juu ya udhibiti wa fedha haramu.

60. Mhe. Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/13 AMM iliidhinishiwa jumla ya shillingi 802,000,000.00 zikiwemo Shilingi 197,000,000.00 za mishahara na stahiki za watumishi, na Shilingi 605,000,000.00 kwa matumizi mengineyo. Kufikia Machi 2013, jumla ya Shilingi 170,885,550.00 (87%) zilipatikana kwa ajili ya mishahara na Shilingi 264,545,421.00 (44%) kwa matumizi mengineyo. Aidha, kwa kazi za Maendeleo, ziliidhinishwa jumla ya Shilingi 1,800,000,000.00 na kupatikana Shilingi 844,289,230.00 (47%). Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

61. Mhe. Spika, katika mwaka 2013/14, Afisi ya Mwanasheria Mkuu inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kukamilisha utekelezaji wa mpango mpya wa Afisi chini ya Sheria ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu;

ii. Kutekeleza Mikakati ya Utekelezaji wa Sheria ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu;

iii. Kukamilisha Matayarisho ya Toleo jipya la Sheria za Zanzibar na kulichapisha;

iv. Kuimarisha Uwezo wa Watendaji; na

v. Kukamilisha ujenzi na kuhamia kwenye Jengo Jipya la Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

62. Mhe. Spika, ili AMM iweze kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 919,000,000.00 kwa kazi za kawaida zikiwemo Shilingi 245,400,000.00 za mishahara na 673,600,000.00 za matumizi mengine.



TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

63. Mhe. Spika, Tume ya Kurekebisha Sheria (TKS) Zanzibar ina jukumu la kuzifanyia mapitio Sheria za Zanzibar na kupendekeza marekebisho yake. Katika kutekeleza jukumu hilo, Tume inatekeleza shughuli mbali mbali ikiwemo kufanya utafiti unaowashirikisha wananchi katika mchakato wa kupitia Sheria. Aidha, Tume inatoa elimu kwa umma juu ya Sheria za Zanzibar ili kuwaongezea uelewa. Lengo la kupitia hatua hizo ni kutunga sheria ambazo zinahusisha wananchi.

64. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Tume imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kawaida kwa kuzipitia sheria nne zifuatazo:- Sheria ya Vileo Sura 163, Sheria ya Mifugo Na. 11/1999, Sheria ya Mikataba Sura 149/1917 na Sheria ya Usafirishaji Bidhaa kwa njia ya Bahari Sura 155/1926. Kufikia sasa, kazi ya kuipitia Sheria ya Vileo imekamilika na kazi ya kupitia Sheria ya Usafirishaji Bidhaa kwa Njia ya Bahari na Sheria ya Mikataba, inaendelea.

65. Mhe. Spika, pamoja na kazi hiyo, Tume inaendelea kufanya uchambuzi kwa ajili ya kubaini Sheria zinazohitaji kufanyiwa mapitio ili kuisaidia Tume katika kuandaa Mpangokazi na kuiwezesha Serikali kujua mahitaji yaliyopo ya kazi ya kupitia sheria, na kusaidia upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kwa kazi hiyo.

66. Mhe. Spika, ili kuzitekeleza vyema kazi zake, TKS imeendelea kuimarisha mashirikiano na taasisi zenye majukumu sawa ndani na nje ya nchi. Katika kufanikisha suala hilo, Tume imefanya mawasiliano na Tume za Kurekebisha Sheria katika baadhi ya nchi za Afrika na taasisi za kimataifa zinazojumuisha Tume za Kutunga Sheria. Katika harakati hizo, Tume imejiunga na Umoja wa Tume za Kurekebisha Sheria za Afrika Mashariki na Kati (Association of Law Reform Agencies of Eastern and Southern Africa - ALRAESA), na Umoja wa Tume za Kurekebisha Sheria za Jumuiya ya Madola (Commonweath Association of Law Reform Agencies - CALRAs). Kupitia taasisi hizo, Tume inapata uzoefu na kujifunza mbinu mpya za kufanyia kazi, na kuongeza ufanisi na uwiano katika utendaji.

67. Mhe. Spika, katika kujiimarisha kiutendaji, Tume imefanya mapitio ya Sheria ya Kuanzishwa kwa Tume ya Kurekebisha Sheria. Hatua hiyo imechukuliwa ili kuleta mabadiliko ya msingi katika Muundo na shughuli za Tume. Rasimu ya Sheria hiyo imekamilika na inatarajiwa kuwasilishwa Wizarani kwa hatua zaidi. Vile vile, ili kuwajengea uwezo Watendaji, Tume imewapatia Wafanyakazi watatu (3) mafunzo ya muda mfupi kuhusu " Computer Crime", na Uandishi wa Sheria nchini Afrika ya kusini, India na Korea. Aidha, Wafanyakazi wawili (2) wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi.

68. Mhe. Spika, kwa upande mwengine, Afisi imetoa mafunzo kwa umma kuhusu matumizi ya Sheria za Zanzibar. Jumla ya vipindi vinane vya televisheni na 12 vya redio vimerushwa hewani kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC); na Semina kuhusu mapitio ya Sheria zimefanywa kwa wadau wakiwemo Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Walimu, Wanafunzi, Madaktari, Polisi, Masheha, Wanasheria wa kujitegemea, Wanasheria wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) pamoja na wanajamii.

69. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, TKS iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 271,000,000.00 kwa matumizi yake. Kati ya fedha hizo, Shilingi 94,000,000.00 zilitengwa kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi, na Shilingi 177,000,000.00 kwa matumizi mengineyo. Fedha zilizopatikana hadi kufikia Machi 2013 ni Shilingi 101,233,200 kwa ajili ya kulipa mishahara na stahiki nyengine za watumishi na Shilingi 98,538,620.00 kwa matumizi mengineyo. Vile vile, jumla ya Shilingi 145,000,000.00 ziliidhinishwa kwa kazi za maendeleo kutoka Serikalini. Kufikia Machi 2013 Shilingi 73,280,000.00 (50.5%) zilipatikana. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

70. Mhe. Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Tume imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo;

i. Kuzifanyia mapitio Sheria za Zanzibar zifuatazo; Limitation Decree Cap 12/1917, The Penal Decree Cap 13/1934, The Legal Practitioners Decree Cap 28 1941, The Notaries Public Decree Cap 29/1948;

ii. Kutoa elimu kwa Umma;

iii. Kuimarisha Utendaji wa kazi za Tume; na

iv. Kuimarisha Ushirikiano na taasisi zenye majukumu sawa na Tume za ndani na za kimataifa.

71. Mhe. Spika, ili kuiwezesha Tume ya Kurekebisha Sheria kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 483,000,000.00 kwa kazi za kawaida. Kati ya fedha hizo Shilingi 147,000,000.00 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 336,000,000.00 kwa matumizi mengine.



AFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA

72. Mhe. Spika, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ndio msimamizi mkuu wa mashtaka yote ya jinai Zanzibar kwa ajili ya upatikanaji wa haki kwa raia. Afisi imeendelea kusimamia kesi zinazondelea kusikilizwa mahakamani, kufungua kesi mpya, na kutoa ushauri juu ya masuala yanayohusu mashtaka na haki za jinai.

73. Mhe. Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/13 Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imetekeleza kazi za kawaida kwa ufanisi. Afisi imeendelea kusimamia kesi za jinai na kutoa ushauri wa kiufundi kwa Jeshi la Polisi na taasisi mbali mbali za Serikali pamoja na Raia. Jumla ya kesi za jinai 2,051 zimefunguliwa katika Mahkama za Zanzibar katika ngazi tafauti na majalada ya uchunguzi wa jinai 409 kutoka kwa Jeshi la Polisi yamepokelewa na kufanyiwa kazi. Vile vile, jumla ya wananchi 576 waliokuwa wakihitaji huduma ya ushauri wa haki ya jinai wamehudumiwa.

74. Mhe. Spika, Afisi imeendelea kujenga mashirikiano baina ya vyombo vinavyosimamia masuala ya jinai, ili kuongeza ufanisi. Mikutano 13 kati ya waendesha mashtaka na wapelelezi imefanyika. Mikutano hiyo imesaidia kujenga ukaribu baina ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na taasisi zinazohusika na uendeshaji wa mashtaka, zikiwemo Jeshi la Polisi, Mahkama, Mawakili wa Utetezi, na jamii kwa jumla. Vile vile, Afisi imeandaa mikutano minane ya wadau wa jinai, zikiwemo baadhi ya taasisi za umma kama vile Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), na Baraza la Manispaa ya Zanzibar. Aidha, Afisi imetoa mafunzo kwa wadau mahsusi, yaani Halmashauri za Wilaya, Mahkama za Mwanzo, na Masheha.

75. Mhe. Spika, katika mwaka 2012/13 Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ilikusudia kukamilisha kazi ya kuweka mfumo wa uendeshaji mashtaka kiraia katika Wilaya ambazo bado Polisi wanaendesha mashtaka. Katika kutekeleza jukumu hilo, Afisi imeajiri wanasheria wapya watano ili kuwapeleka kwenye Wilaya hizo. Mpaka sasa uendeshaji wa mashtaka kiraia unafanyika katika Mahkama nne za Wilaya ambazo ni Mjini, Magharibi, Chake Chake na Mkoani. Tunatarajia kuwa uendeshaji mashtaka kiraia utafanyika kwenye Wilaya zilizobakia, Unguja na Pemba. Afisi imeanza kutayarisha makaazi kwa ajili ya kuwaweka Waendesha mashtaka watakaopangiwa kufanya kazi kwenye vituo vya Makunduchi na Mkokotoni.

76. Mhe. Spika, katika hatua nyengine, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeanza kazi ya kufanya utafiti wa sheria zinazohusu makosa ya jinai. Pamoja na kazi hiyo, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeanza kuupitia Muongozo wa Mashtaka ili kuufanyia marekebisho uendane na mahitaji yaliyopo. Wakati huo huo, Afisi imo katika hatua ya kusambaza Kanuni za Maadili ya Waendesha Mashtaka.

77. Mhe. Spika, Afisi kupitia Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Sheria inaendelea kutoa mafunzo ya usimamizi wa sheria kwa watendaji mbali mbali wakiwemo wanasheria na watendaji wengine wa Serikali na taasisi binafsi. Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa na kituo hicho ni Uandishi wa Sheria (Legislative Drafting), Usimamizi wa Sheria za Kazi (Labour laws Implementation Training), Uandishi wa Miradi (Project Write-up) na ufundi maalum wa Uandishi wa Mikataba (Contract Drafting and Negotiation Skills). Chuo kiko katika hatua za awali za kuanzisha mashirikiano na taasisi za kimataifa ili kujenga na kuimarisha uwezo wake. Baraza la Uongozi wa Chuo tayari limezinduliwa na limeanza kazi kwa mujibu wa sheria.

78. Mhe. Spika, katika kujiimarisha kiutendaji, wafanyakazi 35 wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wamepatiwa mafunzo katika nyanja mbali mbali zikiwemo Sheria, Utawala na uwekaji kumbukumbu; kati yao wanaume ni 28 na wanawake ni saba. Aidha, baadhi ya wanasheria wameshiriki katika semina mbali mbali na mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

79. Mhe. Spika, katika kuelimisha jamii kuhusu haki za jinai, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeandaa na kurusha hewani vipindi tisa kwa njia ya redio, na Jarida la Shahidi limeendelea kutolewa na kusambazwa kwa wadau.

80. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,229,000,000.00 kwa matumizi mbali mbali. Kati ya hizo Shilingi 411,000,000.00 zilitengwa kwa ajili ya mishahara na maslahi mengine ya watumishi, Shilingi 468,000,000.00 kwa Matumizi mengineyo, Shilingi 250,000,000.00 kwa kazi za maendeleo, na Shilingi 100,000,000.00 za ruzuku. Hadi kufikia Machi 2013, fedha zilizopatikana ni Shilingi 434,418,950.00 (106%) kwa mishahara na stahiki za watumishi; Shilingi 277,164,290.00 (59%) kwa matumizi mengineyo; Shilingi 100,000,000.00 (40%) kwa matumizi ya kazi za maendeleo; na Shilingi 43,900,000.00 (44%) ni ruzuku kwa ajili ya kuendeshea shughuli za chuo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

81. Mhe. Spika, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imejiwekea malengo yafuatayo kwa mwaka wa fedha 2013/14:-

i. Kukuza uwezo wa Afisi;

ii. Kukuza na kuimarisha kazi za uendeshaji mashtaka;

iii. Kukuza uwezo wa rasilimali watu; na

iv. Kuendeleza uendeshaji mashtaka kiraia.

82. Mhe. Spika, ili kuiwezesha Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka itekeleze majukumu yake ipasavyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 1,103,000,000.00 kwa kazi za kawaida, zikiwemo 612,000,000.00 za mishahara na 491,000,000.00 za matumizi mengineyo, Shilingi 150,000,000.00 kwa kazi za Maendeleo, na ruzuku ya Shilingi 80,000,000.00 kwa ajili ya kuendeshea Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Sheria.



AFISI YA MUFTI WA ZANZIBAR

83. Mhe. Spika, Afisi ya Mufti wa Zanzibar ina dhima kisheria ya kutoa miongozo kuhusu masuala ya kidini kwa Zanzibar. Afisi ya Mufti katika mwaka wa fedha wa 2012/13, imetekeleza majukumu yake kwa mujibu wa malengo yake ya kibajeti, yakiwemo kuratibu na kusimamia shughuli za kiislamu kama vile Mikutano ya Baraza la Ulamaa, Mikutano ya Kamati ya Kuandama kwa Mwezi, Ziara za misikiti na madrasa; na kutatua migogoro na kushajiisha amani na utulivu.

84. Mhe. Spika, katika utekelezaji, Afisi ya Mufti imesimamia uzinduzi wa Baraza la Ulamaa uliofanyika Januari 2013. Baraza hilo limefanya mikutano miwili. Vile vile, Ofisi ya Mufti imeandaa na kusimamia vikao vya Kamati ya kuthibitisha kuandama kwa mwezi na kutoa taarifa kwa umma. Jumla ya vikao sita vimefanyika. Kazi nyengine ambayo Afisi ya Mufti imeifanya ni kuzitembelea Madrasa na Misikiti. Jumla ya madrasa 83 na misikiti 43 imetembelewa Unguja na Pemba. Kwenye ziara hizo ushauri na maelekezo mbali mbali yametolewa kwa viongozi wa misikiti na madrasa. Katika jitihada zake za kuwa na takwimu sahihi za madrasa na misikiti, Afisi ya Mufti imesajili jumla ya madrasa 210 kati ya madrasa 2431 na misikiti 254 kati ya misikiti 2017 iliyopo Zanzibar. Kazi hii itaendelea kwa mwaka 2013/14.

85. Mhe. Spika, katika jitihada za kudumisha amani, Afisi ya Mufti imefanya mikutano kadhaa na Jumuiya zinazohusishwa na matukio ya uvunjifu wa amani. Vile vile, Afisi imepokea migogoro 51 ya ndoa na mmoja wa msikiti. Migogoro 43 ya ndoa kati ya hiyo iliyopokelewa imepatiwa ufumbuzi, mitano imepelekwa mahakamani na minne inafanyiwa kazi.

86. Mhe. Spika, katika kujenga mahusiano baina ya taasisi za kidini nchini, Afisi ya Mufti imefanya mikutano na baadhi ya Jumuiya za Kiislamu Unguja na Pemba. Masuala kadhaa yalijadiliwa kwenye mikutano hiyo likiwemo suala la kupiga vita vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa kidini. Aidha, Afisi ya Mufti kwa mashirikiano na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam, imefanya matembezi ya hiyari kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jumuiya zenye vituo vya kuwatibu watumiaji wa madawa ya kulevya (Sober Houses), na kuvitembelea mara nne vituo hivyo ili kutoa mawaidha kwa vijana wanaopata huduma ya vituo hivyo.

87. Mhe Spika, Afisi ya Mufti imeendelea na utaratibu wake wa kudumisha uhusiano wa kimataifa. Afisi imepokea wageni kutoka nchi mbali mbali, wakiwemo Sheikh kutoka Misri na viongozi wa dini kutoka Iran, iraq, Marekani, Ujerumani, Newziland, Ufaransa, Uturuki na Kenya. Vile vile, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Saudi Arabia, Ofisi ya Mufti inaratibu msaada wa ujenzi wa misikiti minne kisiwani Pemba. Afisi pia imepata msaada wa mafunzo kuhusu njia bora za kulingania dini ambapo vijana 14 wa Zanzibar watapatiwa mafunzo hayo nchini Misri na India.

88. Mhe Spika, Afisi ya Mufti imeendelea na utamaduni wake wa kutoa elimu kwa umma kwa njia ya redio. Vipindi vya masuala na majibu vimeendelea kutolewa ambapo jumla ya masuala 210 yamejibiwa kupitia vyombo vya habari (ZBC). Aidha, Afisi imepokea watu 378 waliofika kutaka ufafanuzi wa mambo mbali mbali ya kisheria. Mbali na hatua hiyo, vipindi 14 vya nasaha na mawaidha ya dini vimetolewa kuhusu mambo yanayoiathiri jamii wakati huu, yakiwemo ubaya wa rushwa na riba. Aidha, muongozo wa kusheherekea sikukuu za kiislam umetolewa kupitia vipindi hivyo.

89. Mhe. Spika, katika kuimarisha nyenzo za taaluma, Afisi imeanzisha Maktaba ya Kiislam na sasa imo katika jitihada za kutafuta vitabu zaidi kuimarisha maktaba hiyo. Katika hatua nyengine, Afisi ya Mufti imeendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya kupambana na UKIMWI kwa mbinu za kiislam. Afisi imefanya semina ya kuwaelimisha zaidi wafanyakazi wake kuhusu njia za udhibiti wa maambukizi ya UKIMWI. Katika kuwajengea uwezo watendaji wake kitaaluma, Afisi imempatia fursa ya kujiendeleza Mfanyakazi mmoja katika ngazi ya Stashahada.

90. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, Afisi ya Mufti wa Zanzibar iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 338,324,000.00. Kati ya hizo, Shilingi 235,298,000.00 zilitengwa kwa malipo ya mishahara na stahiki nyengine za watumishi, na Shilingi 103,026,000.00 kwa matumizi mengineyo. Hadi kufikia Machi 2013, zilipatikana Shilingi 159,786,000.00 (68%) kwa kulipa mishahara na Shilingi 40,562,700.00 (39%) kwa matumizi mengineyo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

91. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14, Afisi ya Mufti imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha uratibu wa shughuli za dini; na

ii. Kuongeza uwezo wa Afisi kiutendaji

92. Mhe. Spika, ili kuiwezesha Afisi ya Mufti wa Zanzibar itekeleze majukumu yake ipasavyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 485,666,000.00 kwa kazi za kawaida, zikiwemo Shilingi 302,639,000.00 kwa ajili ya mishahara na Shilingi 183,027,000.00. kwa matumizi mengineyo.



WAKALA WA USAJILI WA BIASHARA NA MALI

93. Mhe. Spika, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali ‘The Business and Property Registration Agency’ (BPRA) ndio yenye jukumu la kusimamia masuala ya usajili unaohusu taasisi za biashara, tasnia ya mali za ubunifu, pamoja na usajili wa nyaraka mbali mbali zinazowahusu wananchi na wageni wanaofanya shughuli zao Zanzibar. Afisi hii mpya imeasisiwa baada ya kupitishwa kwa sheria ya Kuanzishwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar Na. 13 ya 2012, ambayo imefuta Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali.

94. Mhe. Spika, katika hatua nyengine, BPRA imeendelea na kazi za usajili. Katika kipindi cha miezi tisa katika mwaka wa fedha 2012/13, BPRA imesajili jumla ya Kampuni 105, Majina ya biashara 281, Alama za biashara 513, NGO's 82 na Nyaraka za aina mbali mbali 608.

95. Mhe. Spika, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali imefanya mikutano na wadau mbali mbali wakiwemo ZRB, ZIPA, TRA, Mtakwimu Mkuu wa Serikali na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kujadili hali ya mifumo ya usajili, na jinsi inavyoweza kusaidia taasisi hizo katika kufanikisha shughuli zake. Aidha, katika mwezi wa Novemba 2012 BPRA iliandaa mkutano wa Baraza la Utawala 'Administrative Council' la ARIPO. Zaidi ya nchi 25 na Mashirika kutoka ndani na nje ya Afrika zilishiriki mkutano huo. Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali pia ilishiriki mikutano mbali mbali ya kiutendaji iliyofanyika nchini Tanzania, Norway na Switzerland pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mikutano hiyo ilijadili mambo mbali mbali ikiwemo usajili na kubadilishana taarifa za makampuni baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

96. Mhe. Spika, katika kujenga uwezo wa kiutendaji, Wakala imefanya Semina elekezi kwa wafanyakazi wake na kuandaa mikutano ya wadau kwa ajili ya kuitambulisha Sheria mpya ya Wakala pamoja na Sheria nyengine zinazoongoza shughuli za usajili Unguja na Pemba. Vile vile, Wakala imewasomesha wafanyakazi watano, katika kiwango cha Shahada ya Kwanza ya Sheria, Stashahada ya Utunzaji Nyaraka, na watatu mafunzo ya muda mfupi ya udereva, kompyuta (Oracle database Administrator) na Usimamizi wa Tasnia za Mali Ubunifu.

97. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, BPRA wakati huo ikiitwa Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 265,673,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 115,674,000.00 zilitengwa kwa ajili ya kulipia mishahara na stahiki za watumishi na Shilingi 149,999,000.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Hadi kufikia Machi, 2013 zimepatikana Shilingi 94,646,950.00 (82%) kwa ajili ya mishahara na Shilingi 75,777,000.00 (51%) kwa matumizi mengineyo. Aidha, Shilingi 100,000,000.00 ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya Maendeleo kutoka Serikalini. Kati ya hizo zimepatikana Shilingi 40,000,000.00 (40%). Vile vile, Afisi ilikadiria kukusanya Shilingi 195,000,000.00. Kufikia Machi 2013, zimekusanywa Shilingi 102,554,010.00 (53%). Angalia Viambatanisho Nam. 1,3&7.

98. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali imedhamiria kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha mazingira ya kazi kwa ajili ya kutoa huduma bora;

ii. Kuandaa kanuni za sheria za Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali, Usajili wa Taasisi za Biashara pamoja na Usajili wa Dhamana za Mali zinazohamishika; na

iii. Kuendeleza uwekaji wa mifumo ya kisasa ya usajili na utoaji huduma.

99. Mhe. Spika, ili kuiwezesha Afisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali itekeleze majukumu yake ipasavyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 289,006,000.00 kwa kazi za kawaida zikiwemo 139,008,000.00 za mishahara na 149,998,000.00 za matumizi mengineyo; na Shilingi 100,000,000.00 kwa kazi za maendeleo. Aidha, Afisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali inakadiria kukusanya mapato ya Shilingi 125,700,000.00. Angalia Viambatanisho Nam. 2&3.



AFISI YA MRAJIS WA VIZAZI NA VIFO

100. Mhe. Spika, Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo (AMVV) kisheria ina majukumu ya kusajili Vizazi na Vifo na kutunza kumbukumbu zitokanazo na usajili huo. Mbali na hayo, Afisi ina jukumu la kuishauri Serikali kuhusu masuala ya Usajili wa Vizazi na Vifo, kuelimisha jamii, na kutoa mafunzo kuhusu usajili kwa watendaji na mawakala wa usajili, wakiwemo watendaji wa Afya, masheha, na viongozi wa dini.

101. Mhe. Spika, kwa mwaka 2012/13, AMVV imesajili jumla ya vizazi 31,540 wakiwemo wanaume 15,930 na wanawake 15,610, Unguja na Pemba. Vile vile, Afisi imesajili vifo 1,885 vikiwemo vya wanaume 1,072 na wanawake 813, Unguja na Pemba. Takwimu hizo zinabainisha vifo kuandikishwa kwa idadi ndogo. Tatizo hilo linasababishwa na mwamko mdogo wa jamii na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuandikisha vifo. Wizara yangu kwa mwaka 2013/14 imepanga kutoa elimu kwa jamii ili kuhamasisha uandikishaji wa vizazi na vifo. Kwa kuanzia napenda kutoa wito kwa Wajumbe wa Baraza lako walichukulie suala la uandikishaji wa vizazi na vifo kwa usawa na umuhimu mkubwa, na wasaidie kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao juu ya umuhimu huo.

102. Mhe. Spika, usajili wa vizazi na vifo umekuwa na matatizo mengi kwa muda mrefu na unaleta usumbufu wa mara kwa mara kwa watu wanaohitaji huduma ya vyeti vya kuzaliwa. Ukosefu wa magamba ya kuchapishia vyeti, uwezo mdogo wa uchapaji na ukosefu wa fedha ndiyo matatizo ya msingi yanayosababisha hali hiyo. Hata hivyo, Wizara yangu imefanya jitihada za kulipunguza tatizo hilo kwa kushirikiana na taasisi nyengine za Serikali, kama vile Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Idara ya Mpiga Chapa wa Serikali.

103. Mhe. Spika, pamoja na hatua hizo, Wizara yangu imeanza kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kuondokana na tatizo hilo kwa kufanya marekebisho ya mfumo wa usajili kwa kutumia kompyuta. Majaribio ya mfumo huo yamepangwa kufanyika katika mwaka 2013/14 kwa Mkoa wa Mjini Magharibi. Ili kuuwezesha mfumo huo kufanya kazi, hatua kadhaa zimefikiwa. Rasimu ya Sheria ya Usajili wa Matukio ya Kijamii imekamilika na imefikia hatua ya kujadiliwa Baraza la Mapinduzi. Hatua nyegine ni kutoa mafunzo kwa Mawakala wa Usajili Wilaya za Mjini na Magharibi, na kuingiza taarifa za miaka ya nyuma kwenye kompyuta, ili kusaidia uwekaji kumbukumbu na upatikanaji wa vyeti kwa haraka. Hatua itakayofuata ni kutoa mafunzo kwa mawakala wa usajili kwenye Wilaya zilizobakia, kutoa elimu kwa umma, kuweka miundombinu ya mfumo wa mawasiliano, na kuajiri Maafisa Usajili wa Wilaya.

104. Mhe. Spika, katika maandalizi ya mfumo mpya wa usajili Wilayani, AMVV imeanza kazi ya matengenezo na marekebisho ya Afisi za Usajili za Wilaya. Matengenezo hayo yamekamilika katika Afisi za Wilaya ya Kusini, Kati, Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’ Unguja. Matengenezo kama hayo yataendelea kwa Wilaya zilizobaki. Aidha, chumba kimoja kwenye Afisi Kuu, Forodhani, kimefanyiwa matengenezo makubwa ili kuweka ‘server computer’ ambayo itakuwa ndiyo kituo kikuu cha taarifa zote za vizazi, vifo, ndoa na talaka.

105. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, Afisi ya Mrajis Vizazi na Vifo iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 305,159,000.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 134,222,000.00 zilitengwa kwa ajili ya kulipia mishahara na stahiki za watumishi na Shilingi 170,937,000.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Hadi kufikia mwezi wa Machi 2013, fedha zilizopatikana ni Shilingi 79,559,600.00 (59%) kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi, na Shilingi 72,124,492.00 (42%) kwa matumizi mengineyo. Aidha, jumla ya Shilingi 400,000,000.00 ziliidhinishwa kwa ajili ya shughuli za Maendeleo kutoka Serikalini na zilipatikana jumla ya Shilingi 262,732,297.00 (66%). Afisi pia ilikadiriwa kukusanya mapato ya Shilingi 180,000,000.00, na kufikia Machi 2013, Shilingi 105,333,550.00 (59%) zilikusanywa. Angalia Kiambatanisho Nam. 1&3.

106. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14, Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma;

ii. Kuimarisha uwezo wa Afisi kiutendaji; na

iii. Kufanya mageuzi ya mfumo wa usajili na utoaji wa vyeti.

107. Mhe. Spika, ili Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 353,460,000.00 kwa matumizi ya kawaida; kati ya hizo Shilingi 145,221,000.00 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 208,239,000.00, kwa matumizi mengineyo. Vile vile, naliomba Baraza lako liidhinishe matumizi ya Shilingi 300,000,000.00 kwa kazi za maendeleo, na makusanyo ya Shilingi 219,300,000.00 kuchangia Mfuko Mkuu wa Hazina. Angalia Viambatanisho Nam. 2&3.



AFISI YA MSAJILI WA HAKIMILIKI

108. Mhe. Spika, Afisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar ina dhima kisheria ya kuhakikisha hali, hadhi na maslahi ya wabunifu wa Zanzibar yanaimarika kwa kuthaminiwa na kupatiwa malipo yanayotokana na matumizi ya kazi zao kibiashara. Vile vile, Afisi ya Hakimiliki inahusika na usimamizi na utendaji kisheria wa mfumo wa hakimiliki kitaifa na kimataifa. Jukumu hilo linatekelezwa kwa kusajili kazi za hakimiliki, kutoa leseni kwa matumizi halali ya kazi hizo kibiashara, pamoja na kukusanya na kugawa mirabaha kwa wabunifu waliosajili kazi zao.

109. Mhe. Spika, Afisi ya Hakimiliki ni Wakala wa Wenye Hakimiliki zilizosajiliwa. Mojawapo ya kazi zake muhimu ni kukukusanya na kugawa mirabaha. Hadi kufikia mwezi Machi 2013, jumla ya Shilingi 37,648,000.00 zilikusanywa. Utaratibu wa kugawa mirabaha kwa wabunifu 726 wa muziki, kasida, mawaidha na filamu waliosajiliwa na Afisi zimekamilika na ugawaji utafanyika hivi karibuni.

110. Mhe. Spika, katika kutekeleza lengo lake la kupunguza uharamia wa kazi za hakimiliki, Afisi imeimarisha uwezo wa kiutendaji kwa Dawati la Hakimiliki la Jeshi la Polisi na Waendesha Mashtaka. Mafunzo juu ya masuala ya Hakimiliki yametolewa kwa Kikundikazi cha Askari Polisi wa Mikoa, Waendesha Mashtaka na Maafisa Kodi. Pia kwa kushirikiana na Shirika la Milki Ubunifu Ulimwenguni (WIPO) yalifanyika mafunzo ya utambuzi wa jinai za hakimiliki kwa Jeshi la Polisi, mahakimu na maofisa kodi.

111. Mhe. Spika, Afisi pia inatoa taaluma kwa wabunifu, watumiaji wa kazi za hakimiliki, pamoja na kutoa taarifa za kitaalamu kwa umma, taasisi za umma na taasisi binafsi kuhusiana na masuala ya hakimiliki. Kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2013, jumla ya vipindi 28 vya redio na 31 vya televisheni vilirushwa hewani. Pia, Ofisi imetoa elimu ya ana kwa ana kwa watu 22, wakiwemo wanafunzi wa sekondari 15 na wanafunzi saba wa vyuo ambao wanafanya utafiti.

112. Mhe. Spika, katika kujiimarisha kiutendaji, Afisi ya Msajili wa Hakimiliki imewapatia mafunzo watendaji watatu. Mfanyakazi mmoja anasoma Shahada ya pili katika fani ya “Development Policy”, Morogoro, mmoja amehudhuria mafunzo ya “Cyber Crime” nchini Korea, mmoja amehudhuria mafunzo Dar es Salaam kuhusu “Practical Approaches to Intellectual Property Utilisation and Protection in Africa”.

113. Mhe. Spika, ili kujiimarisha kiutendaji, Afisi ya Usajili wa Hakimiliki inaipitia Sheria ya Hakimiliki Namba 14 ya mwaka 2003, kwa ajili ya kuifanyia marekebisho. Rasimu ya mwanzo imekamilika na sasa imeanza kujadiliwa na Wataalamu wa Shirika la Milki Ubunifu (WIPO), na baadae itajadiliwa na wadau wa Hakimiliki wa ndani ya nchi.

114. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Afisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar iliidhinishiwa ruzuku ya Shilingi 120,000,000.00; Shilingi 39,548,800.00 kwa malipo ya mishahara na stahiki za watumishi na Shilingi 80,452,000.00 kwa matumizi mengineyo. Hadi kufikia Machi 2013, fedha zilizopatikana ni Shilingi 50,747,850.00 (128%) kwa ajili ya mishahara na Shilingi 32,187,000.00 (40%) kwa matumizi mengineyo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

115. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Afisi imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kukamilisha mapitio ya Sheria ya Hakimiliki;

ii. Kupunguza uharamia wa kazi za hakimiliki; na

iii. Kuimarisha uwezo wa Afisi kiutendaji.

116. Mhe. Spika, ili Afisi ya Hakimiliki iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi 140,000,000.00 kwa matumizi ya kawaida zikiwemo Shilingi 63,347,000.00 kwa mishahara na Shilingi kwa 76,653,000.00 matumizi mengineyo.



KAMISHENI YA WAKFU NA MALI YA AMANA

117. Mhe. Spika, Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ina jukumu la kusimamia masuala yote yanayohusu mali za Wakfu, Amana, Mirathi ya Waislamu, Sala na Mabaraza ya Idd Kitaifa, Hijja, Zakka na Misaada ya Kheri.

118. Mhe. Spika, katika kutekeleza majukumu hayo Kamisheni iliweka lengo la kuimarisha Mfumo wa ukusanyaji na ugawaji wa Zakka katika mwaka 2012/13. Katika kufanikisha suala hilo Elimu ya Zakka imetolewa kupitia semina nne kwa mikoa ya Unguja, ziara za vikundi 118 na wajasiriamali 20 Unguja na Pemba, na Vipindi vitatu vya TV. Aidha, vitabu 135 vya Muongozo wa Zakka na vipeperushi 200 vimegaiwa. Afisi imefanya na kukamilisha uchambuzi wa mahitaji ya utendaji na uimarishaji wa kumbukumbu za Zakka. Jumla ya Shilingi 321,807,200.00 za Zakka zimegaiwa na Shilingi 2,100,000.00 zilikusanywa. Aidha, Misaada ya kheri yenye thamani ya Shilingi 930,000.00 kutoka Baitulmali na wachangiaji mbali mbali imetolewa. Angalia Kiambatanisho Nam. 8a.

119. Mhe. Spika, katika kuendeleza mfumo bora wa usimamizi wa Mali za Wakfu na Amana, Kamisheni imeandaa Muongozo wa Wakfu; imefanya vikao 33 vya uelimishaji na uhamasishaji, na kutoa vipindi viwili vya TV, kipindi kimoja cha Radio na makala mbili katika gazeti. Vile vile, Kamisheni imo katika hatua za awali za kuanzisha database.

120. Mhe. Spika, Kamisheni imeendeleza utafiti, uhakiki na utekelezaji wa nyasia na wakfu, pamoja na ukusanyaji wa kodi za wakfu, amana na ada. Matokeo ya kazi hizo ni kupatikana kwa nyaraka 40; kutekelezwa kwa nyasia 20 kwa jumla ya Shilingi 46,215,344.90; na kusajiliwa kwa nyakfu tisa mpya. Aidha, jumla ya Shilingi 217,325,360.00 zimekusanywa kutokana na kodi ya nyumba za Wakfu, Shilingi 27,074,000.00 kutokana na Mali za Amana; Shilingi 3,688,000.00 mashamba; na Shilingi 790,000.00 kwa ada za mikataba 79.

121. Mhe. Spika, katika kufanya ukaguzi, hifadhi na uendelezaji wa nyumba na mashamba ya Wakfu na Amana, jumla ya nyumba 157 na mashamba tisa yamekaguliwa, nyumba 10 na msikiti mmoja zimefanyiwa matengenezo kwa gharama ya Shilingi 65,502,000.00, na miche 100 ya minazi imepandwa katika mashamba ya Wakfu.

122. Mhe. Spika, katika kutekeleza huduma za mirathi, jumla ya Majalada 389 yalifunguliwa, majalada 342 yenye mali ya thamani ya Shilingi 2,219,262,573.00 yalifungwa Unguja na Pemba, na mapitio ya majalada ya 2005 yamefanyika. Aidha, nyaraka 29 zikiwemo 23 za urithi na sita za mauzo zimetolewa. Vile vile, mizozo 12 inayohusu mirathi imeshughulikiwa na mingine 13 inaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

123. Mhe. Spika, katika mwaka wa 2012/13, Kamisheni imesimamia vyema shughuli za Hijja na kuimarisha huduma za Mahujaji. Jumla ya Mahujaji 2,146 walitekeleza ibada hiyo. Mahujaji 1,255 kati ya hao walisafiri kupitia vikundi vya Zanzibar na vikao tisa vimefanyika ndani na nje ya nchi kuratibu shughuli za Hijja. Vile vile, Kamisheni imeendelea kusimamia kwa ufanisi shughuli za Sala na Mabaraza ya Idd kitaifa. Angalia Kiambatanisho Nam. 8b.

124. Mhe. Spika, Kamisheni ya Wakfu imeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi. Katika mwaka wa fedha 2012/13 Kamisheni imeanzisha uhusiano na Wizara ya Wakfu ya Oman, Qatar, Taasisi ya Al-Rahma ya Falme za Kiarabu (UAE) na Shirika la Danmission la Denmark.

125. Mhe. Spika, katika kutayarisha nyenzo za kufanyia kazi, Kamisheni imo katika hatua za mwisho za kukamilisha Kanuni za Hiba na Wakfu, Wasia na Mirathi, Huduma, Ada na Malipo. Aidha, kazi ya kukamilisha Mpango Mkakati wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana zinaendelea sambamba na ukamilishaji wa Muundo wa Kamisheni. Katika kuwajengea uwezo watendaji, Kamisheni imesomesha wafanyakazi wawili ngazi ya Shahada, wanne Stashahada na wawili mafunzo ya muda mfupi. Aidha, Kamisheni imetoa mafunzo ya ndani kuwajenga wafanyakazi ili kutoa huduma bora zaidi.

126. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13 Kamisheni iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 460,000,000.00 za ruzuku zikiwemo 291,280,000.00 za mishahara, 168,720,000.00 za matumizi mengine, na Shilingi 179,000,000.00 za makusanyo ya ndani. Hadi kufikia Machi 2013, fedha zilizoingizwa ni Shilingi 184,789,875.00 (63%) zilizotumika kulipia mishahara na Shilingi 172,850,381.00 (102%) kwa matumizi mengineyo. Aidha, Shilingi 136,561,865.00 (76%) zilikusanywa kutokana na mapato ya ndani na zilichangia uendeshaji wa ofisi. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

127. Mhe. Spika, katika mwaka ujao wa fedha Kamisheni imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuimarisha utoaji wa huduma za Zakka na Wakfu;

ii. Kuimarisha Uwezo wa Afisi kiutendaji; na

iii. Kuimarisha shughuli za Uratibu na Uendeshaji.

128. Mhe. Spika, ili Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana iweze kutekeleza majukumu na malengo yake katika kipindi cha 2013/14 naliomba baraza lako tukufu liidhinishe Ruzuku ya Shilingi 510,000,000.00 zikiwemo Shilingi 303,745,000.00 za mishahara, na Shilingi 206,255,000.00 za matumizi mengine.



AFISI KUU PEMBA

129. Mhe. Spika, Afisi Kuu Pemba ina jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za utendaji wa Wizara Pemba. Katika kipindi cha mwaka 2012/13, Afisi Kuu Pemba imeendelea kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

130. Mhe. Spika, Afisi Kuu Pemba imefanya ziara tano za kutembelea Idara na Taasisi za Wizara na kufanya mikutano mitatu ya robo mwaka. Aidha, Afisi imefanya mkutano mmoja wa wafanyakazi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Vile vile, Afisi Kuu Pemba imeratibu maandalizi ya ripoti na taarifa za utekelezaji na maandalizi ya bajeti ya Wizara ya 2013/14 na kuziwasilisha Wizarani kwa hatua zaidi.

131. Mhe. Spika, mbali na majukumu hayo Afisi Kuu Pemba imeshiriki vikao mbalimbali vilivyojadili ripoti na bajeti ili kupata miongozo ya pamoja. Aidha, Afisi imeratibu kazi zinazohusiana na marekebisho ya utumishi wa umma yanayohusisha kuhakiki na kupitia mafaili ya wafanyakazi, kutayarisha nominal roll na madaraja ya wafanyakazi (Scheme of Service) wa Wizara kwa upande wa Pemba.

132. Mhe. Spika, miongoni mwa kazi za Afisi Kuu Pemba ni kuratibu shughuli za Jumuiya Zisizo za Kiserikali (NGOs). Katika mwaka wa fedha unaomalizika, Afisi Kuu Pemba imezitembelea Jumuiya zilizoko Pemba kwa lengo la kutathmini utendaji na kuwepo kwake. Jumla ya Jumuiya 26 zimetembelewa kati ya 36 zilizopangwa.

133. Mhe. Spika, katika kuwajengea uwezo watendaji wake, Afisi imeandaa mafunzo ya wafanyakazi yanayohusu Sheria ya Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Wizara. Afisi pia imeendelea kulipa gharama za mafunzo kwa watumishi watatu wa Afisi Kuu, mmoja katika ngazi ya Stashahada, na wawili mafunzo ya muda mfupi katika fani ya Uchunguzi wa Hesabu za Ndani na Utunzaji wa Kumbukumbu.

134. Mhe. Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Afisi Kuu Pemba, ilikadiria kutumia Shilingi 165,331,000.00 kwa kazi za kawaida zikiwemo Shilingi 80,159,000.00 kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi na Shilingi 85,172,000.00 kwa matumizi mengineyo. Kufikia Machi 2013 jumla ya Shilingi 60,119,250.00 (75%) zimetumika kwa kulipia mishahara na Shilingi 41,483,951.00 (49%) kwa matumizi mengineyo. Angalia Kiambatanisho Nam. 1.

135. Mhe. Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/14, Afisi Kuu Pemba inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

i. Kuendelea kuratibu shughuli za Wizara Pemba;

ii. kuwaendeleza wafanyakazi kielimu; na

iii. Kulifanyia matengenezo jengo la wizara Pemba.

136. Mhe. Spika, ili Afisi Kuu Pemba iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mwaka wa fedha 2013/14, naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 196,575,000.00 kwa matumizi ya kawaida zikiwemo Shilingi 105,704,000.00 za mishahara na Shilingi 90,871,000.00 za matumizi mengineyo.

RASIMU YA KATIBA

137. Mhe. Spika, sote tunaelewa kuwa rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Napenda kutanabahisha kuwa kazi iliyopo mbele ya Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu ni kubwa. Kwanza ni sisi wenyewe kujua tunataka Muungano upi na Katiba ipi. Baada ya kujua hayo, itatulazimu tuwaelimishe wananchi wetu ili waijadili rasimu hii iliyopo na kutoa maoni yao kupitia Wawakilishi wao, Mabaraza ya Katiba na, hatimaye, Bunge la Katiba.

138. Mhe. Spika, ninachowaomba wananchi na kwa kweli kwa kupitia Wawakilishi wao, ni kutazama na kujadili rasimu hiyo na kuona kama kweli inakidhi haja ya kuleta maendeleo kwa Zanzibar; maisha mazuri kwa Vizazi vya Wazanzibari; na Haki za Wazanzibari; na kwamba katiba itakayopatikana itaweza kuhimili misukosuko ya kisiasa na kibinaadamu na kuweza kuishi kwa miaka mingi ijayo bila ya mtikisiko wa vishindo vyovyote. Tuhakikishe kuwa Katiba hiyo inafufua matarajio ya Wazanzibari kwa Zanzibar yetu ya leo na ya siku za usoni.

139. Mhe. Spika, ni lazima tuelewe kuwa Katiba tuitakayo Wazanzibari itabadilisha sana taifa letu, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Baadhi ya mabadiliko hayo yatakuwa ya karibuni na tuwe tayari kuyaunga mkono. Lakini baadhi ya mabadiliko yatachukua muda, ni lazima pia tuwe imara na wenye uzingativu kwa kujibidiisha kulingana na mabadiliko hayo.

140. Mhe. Spika, kwa upande wa Serikali, napenda nichukue nafasi hii tena kwa kuwahakikishia Wazanzibari kuwa tutasimama na matakwa ya Wazanzibari na tutawatetea na kuwasimamia kwa yale yote mtakayokubaliana katika Mabaraza ya Katiba katika kuleta Maslahi ya Zanzibar.

SHUKRANI

141. Mhe. Spika, kwa dhati kabisa, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuiwasilisha hotuba hii mbele ya Baraza lako tukufu. Aidha, napenda kuwashukuru wale wote waliotoa michango yao katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Wizara yangu. Vile vile, natoa shukurani kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza lako tukufu, bila kuwasahau Watendaji Wakuu na Wafanyakazi wote wa Wizara ya Katiba na Sheria, kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza kazi za Wizara na kwa maandalizi mazuri ya hotuba hii. Mwisho, natoa shukurani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Baraza hili, kwa michango yao yenye manufaa kwa Wizara na Taifa kwa ujumla.

142. Mhe. Spika, kwa heshima na taadhima naomba uniruhusu niwashukuru wadau mbali mbali wa maendeleo ambao wamefanya kazi kwa mashirikiano makubwa na Wizara yangu. Wadau hao ni UNDP, UNICEF, UNFPA, Shirika la Kimataifa la Mali za Ubunifu (WIPO), Shirika la Mali Bunifu la Afrika (ARIPO), Benki ya Dunia, Jumuiya ya Ulaya, African Muslim Agency, Benki ya Maendeleo ya Kiislam (IDB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Save the Children, Wizara za Wakfu za Oman na Qatar, Taasisi ya Al-Rahma ya Falme za Kiarabu (UAE) na Shirikia la Danmission la Denmark; Saud Arabia, Oman, na Egypt; Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), na Chama cha Wanasheria Wanawake (ZAFELA); Vyombo vya Sheria vya Jamhuri ya Muungano zikiwemo Mahkama, Tume ya Kurekebisha Sheria na Afisi ya Mwanasheria Mkuu, na Jeshi la Polisi; Vikundi vilivyosafirisha Mahujaji, Jumuiya na Taasisi mbali mbali za kidini; na Masheha na Wanajamii wote wa Zanzibar kwa jumla. Hao wote tunathamini ushirikiano na misaada yao ya hali na mali, na kwa niaba ya Wizara yangu na Serikali kwa jumla hatuna zaidi cha kuwalipa isipokuwa kuwambia ahsante sana na Mungu awabariki.

HITIMISHO

143. Mhe. Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza malengo yake vyema, naomba Wajumbe wa Baraza lako tukufu wachangie hotuba hii, watushauri ipasavyo na hatimaye waidhinishe Shilingi 8,188,000,000.00 kwa matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 kwa kazi za kawaida. Kati ya fedha hizo Shilingi 4,480,499,000.00 zitumike kulipia mishahara na Shilingi 3,707,501,000.00 kwa matumizi mengine. Aidha, naliomba Baraza lako liidhinishe Shilingi 2,154,313,000.00 kwa kazi za maendeleo. Kati ya fedha hizo, 850,000,000.00 ni kutoka serikalini, na Shilingi 1,304,313,000.00 kutoka kwa washirika wa maendeleo. Vile vile, naliomba Baraza lako liidhinishe Ruzuku ya Shilingi 730,000,000.00. Naomba pia Baraza lako liikubalie Wizara yangu ichangie Shilingi 435,000,000.00 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Angalia Viambatanisho Nam. 2&3.



144. Mhe. Spika, naomba kutoa hoja.



Kiambatanisho 1: Muhtasari wa Upatikanaji wa Fedha na Matumizi, 2012/13

TAASISI/IDARA ENEO LA BAJETI BAJETI ILIOTENGWA KWA MWAKA 2012/13 FEDHA ILIYOPATIKANA JULAI-MACHI 2012/13 ASILIMIA (%)

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI Mishahara na Stahiki 83,306,000 65,244,700 78%

Matumizi Mengine 89,554,000 41,709,200 47%

Maendeleo SMZ 160,000,000 48,612,000 30%

Maendeleo Wahisani 627,200,000 188,639,000 30%

Jumla Kuu 960,060,000 344,204,900 36%



IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI Mshahara na Stahiki 314,343,000 228,011,820 73%

Matumizi Mengine 252,310,000 116,289,299 46%

Jumla Kuu 566,653,000 344,301,119 61%



MAHKAMA Mishahara na Stahiki 2,352,000,000 1,657,639,000 70%

Matumizi Mengineyo 793,000,000 344,843,836 43%

Maendeleo SMZ 600,000,000 100,000,000 17%

Jumla Kuu 3,745,000,000 2,102,482,836 56%

Makusanyo 72,000,000 80,820,500 112%



AFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI Mishahara na Stahiki 197,000,000 170,885,550 87%

Matumizi Mengineyo 605,000,000 264,545,421 44%

Maendeleo SMZ 1,800,000,000 844,289,230 47%

Jumla Kuu 2,602,000,000 1,279,720,201 49%



TUME YA KUREKEBISHA SHERIA Mishahara na Stahiki 94,000,000 101,233,200 108%

Matumizi Mengineyo 177,000,000 98,538,620 56%

Maendeleo SMZ 145,000,000 73,280,000 51%

Jumla Kuu 416,000,000 273,051,820 66%



AFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA Mishahara na Stahiki 411,000,000 434,418,950 106%

Matumizi mengineyo 468,000,000 277,164,290 59%

Maendeleo SMZ 250,000,000 100,000,000 40%

Ruzuku 100,000,000 43,900,000 44%

Jumla Kuu 1,229,000,000 855,483,240 70%

Mapato ya Ndani 118,000,000 35,000,000 30%



AFISI YA MRAJIS MKUU WA SERIKALI Mishahara na Stahiki 115,674,000 94,646,950 82%

Matumizi mengineyo 149,999,000 75,777,000 51%

Maendeleo SMZ 100,000,000 40,000,000 40%

Jumla Kuu 365,673,000 210,423,950 58%

Makusanyo 195,000,000 102,554,010 53%



AFISI YA MRAJIS WA VIZAZI NA VIFO Mishahara na Stahiki 134,222,000 79,559,600 59%

Matumizi mengineyo 170,937,000 72,124,492 42%

Maendeleo SMZ 400,000,000 262,732,297 66%

Maendeleo Wahisani 2,600,000,000 0 0%

Jumla Kuu 3,305,159,000 414,416,389 13%

Makusanyo 180,000,000 105,333,550 59%



AFISI YA MUFTI WA ZANZIBAR Mishahara na Stahiki 235,298,000 159,786,000 68%

Matumizi mengineyo 103,026,000 40,562,700 39%

Jumla Kuu 338,324,000 200,348,700 59%



KAMISHENI YA WAKFU NA MALI YA AMANA



Mishahara na Stahiki 291,280,000 184,789,875 63%

Matumizi Mengine 168,720,000 172,850,381 102%

Jumla Ruzuku 460,000,000 357,640,256 78%

Mapato ya Ndani 179,000,000 136,561,865 76%

Jumla Kuu 639,000,000 494,202,121 77%



AFISI YA MSAJILI WA HAKIMILIKI Mishahara na Stahiki 39,548,000 50,747,850 128%

Matumizi Mengineyo 80,452,000 32,187,000 40%

Jumla Kuu 120,000,000 82,934,850 69%



AFISI KUU PEMBA Mishahara na Stahiki 80,159,000 60,119,250 75%

Matumizi Mengineyo 85,172,000 41,483,951 49%

Jumla Kuu 165,331,000 101,603,201 61%



Jumla ya Wizara (Mishahara, Stahiki na OC) 7,591,000,000 4,909,058,935 65%

Jumla Mishahara 4,017,002,000 3,051,545,020 76%

Jumla Matumizi Mengine 2,893,998,000 1,373,038,809 47%

Jumla Ruzuku 680,000,000 484,475,106 71%



Jumla Maendeleo SMZ 3,455,000,000 1,468,913,527 43%

Jumla Maendeleo Wahisani (DPs) 3,227,200,000 188,639,000 6%

Jumla ya Wizara Maendeleo 6,682,200,000 1,657,552,527 25%

Jumla Kuu ya Wizara 14,273,200,000 6,566,611,462 46%

Jumla Makusanyo 447,000,000 288,708,060 65%







Kiambatanisho 2: Makadirio ya Matumizi kwa Mwaka 2013/14

FUNGU/ IDARA KAZI ZA KAWAIDA (000) KAZI ZA MAENDELEO (000)

JUMLA MSHAHARA NA STAHIKI MATUMIZI MENGINEYO UNGUJA PEMBA SMZ WAHISANI JUMLA MAENDELEO JUMLA KUU

14 - MahkamaKuu 3,583,000 2,350,100 1,232,900 2,732,556 850,444 150,000 0 150,000 3,733,000

15 – Afisi ya M/ Mkuu 919,000 245,400 673,600 919,000 - 0 0 0 919,000

46 - Tume ya K/ Sheria 483,000 147,000 336,000 483,000 - 0 0 0 483,000

35 - Afisi ya M/Mashtaka 1,103,000 612,000 491,000 888,519 214,481 150,000 0 150,000 1,253,000

36/03 - Afisi Kuu Pemba 196,575 105,704 90,871 - 196,575 0 0 0 196,575

36/04 - Idara ya MSU 184,152 94,596 89,556 184,152 0 150,000 1,304,313 1,454,313 1,638,465

36/05 - Afisi ya Mufti 485,666 302,639 183,027 375,124 110,542 0 0 0 485,666

36/06 - Idara ya Uendeshaji na Utumishi 591,141 338,831 252,310 591,141 0 0 0 0 591,141

36/11Wakala wa UBM 289,006 139,008 149,998 273,007 15,999 100,000 100,000 389,006

36/901 - Afisi ya Mrajis Vizazi na Vifo 353,460 145,221, 208,239 278,759 74,701 300,000 300,000 653,460

Ruzuku - DPP 80,000 30,000 50,000 80,000 - 0 0 0 80,000

Ruzuku - KWNMA 510,000 303,745 206,255 410,000 100,000 0 0 0 510,000

Ruzuku-Afisi ya Hakimiliki 140,000 63,347 76,653 140,000 - 0 0 0 140,000

Ruzuku V. 36 650,000 367,092 282,908 550,000 100,000 0 0 0 650,000

VOTE 36 2,100,000 1,125,999 974,001 1,702,183 397,817 550,000 1,304,313 1,854,313 3,954,313

Jumla Mish&OC 8,188,000 4,480,499 3,707,501 6,725,258 1,462,742 850,000 1,304,313 2,154,313 10,342,313

JUMLA KUU 8,918,000 4,877,591 4,040,409 7,355,258 1,562,742 850,000 1,304,313 2,154,313 11,072,313



Kiambatanisho 3: Makusanyo ya Mapato na Makadirio ya 2013/14

IDARA/TAASISI MAKADIRIO 2012/13 MAKUSANYO HALISI 2012/13 % MATARAJIO JUNI 2013 JUMLA HADI JUNI 2013 % MAKADIRIO 2013/14

36/11 WAKALA WA USAJILI BIASHARA NA MALI 195,000,000 102,554,010 53% 23,000,000 125,554,010 64% 125,700,000

14MAHKAMA 72,000,000 80,820,500 112% 15,000,000 95,820,500 133% 90,000,000

36/902 MRAJIS WA VIZAZI NA VIFO 180,000,000 105,333,550 59% 33,000,000 138,333,550 77% 219,300,000

JUMLA KUU 447,000,000 288,708,060 65% 71,000,000 359,708,060 80% 435,000,000



Kiambatanisho 4: Miradi ya Maendeleo 2013/14

Nam. ya Mradi Jina la Mradi Mchango wa Serikali Mchango wa Wahisani Mhisani Jumla Kuu

74017 Ujenzi wa Jengo la Wizara ya KS 0.00 0.00 0.00

74018 Programu ya Mageuzi ya Sekta ya Sheria 150,000,000 1,304,313,600 UNDP 1,454,313,600

72201 Kurekebisha mfumo wa Usajili wa Kampuni ya Biashara na Kuimarisha Afisi ya Msajili Biashara na Mali 100,000,000 0.00 100,000,000

74019 Mradi wa Mageuzi katika Usajili wa Takwimu za Vizazi na Vifo 300,000,000 0.00 300,000,000

72212 Mradi wa kuimarisha Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka 150,000,000 0.00 150,000,000

72234 Matengenezo ya majengo ya Mahkama 150,000,000 0.00 150,000,000

JUMLA KUU 850,000,000 1,304,313,600 2,154,313,600





Kiambatanisho 5a:- Ufunguaji wa Kesi Mahkamani Julai hadi Machi 2012/2013

KESI ZILIZOFUNGULIWA RUFAA

Madai Jinai Madai Jinai

Mahkama Jumla Zilizofunguliwa Zilizofu

nguliwa Zilizotolewa Uamuzi Zilizofungu

liwa Zilizotolewa Uamuzi Zilizofu

nguliwa Zilizotolewa Uamuzi Zilizofungu

liwa Zilizotolewa Uamuzi

M/Rufaa Tanzania 5 0 0 0 0 3 0 2 0

M/Kuu Vuga 100 50 6 10 0 37 10 3 1

M/Kuu Pemba 59 15 0 2 0 41 0 1 0

Kazi 6 6 2 0 0 0 0 0 0

Kadhi wa Rufaa Unguja 50 0 0 0 0 50 25 0 0

Kadhi Rufaa Pemba 13 0 0 0 0 13 12 0 0

Mkoa Vuga 103 18 1 77 7 5 0 3 0

Mkoa Mfenesini 47 2 0 37 2 2 0 6 1

Mkoa Mwera 73 6 1 65 2 0 0 2 1

Mkoa Wete 53 2 0 45 4 0 0 6 0

Mkoa Chake 57 1 0 52 2 0 0 4 0

Wilaya Mw/kwe 588 33 4 553 242 2 0 0 0

Wilaya Mwera 365 13 11 352 171 0 0 0 0

Wilaya Mkokotoni 300 1 0 297 162 1 0 1 0

Wilaya Mfenesini 200 0 0 199 105 0 0 1 0

Wilaya Makunduchi 83 0 0 83 27 0 0 0 0

Wilaya Mkoani 60 1 0 59 8 0 0 0 0

Wilaya Chake 101 8 0 89 35 0 0 4 0

Wilaya Wete 106 2 0 104 35 0 0 0 0

Wilaya Konde 124 0 1 119 74 0 0 0 0

Watoto Vuga 22 0 0 22 2 0 0 0 0

Watoto Mwera 12 0 0 12 1 0 0 0 0

Watoto Mfenesini 11 0 0 12 2 0 0 0 0

Watoto Chake 9 0 0 9 2 0 0 0 0

Watoto Wete 2 0 0 2 0 0 0 0 0

Jumla 2549 158 26 2200 883 154 47 33 3





Kiambatanisho 5b: Ufunguaji wa Kesi Mahkama za Mwanzo na Kadhi 2012/13

Ufunguaji wa Kesi Mahkama za Mwanzo Ufunguaji wa Kesi Mahkama za Kadhi

Mahkama ya Mwanzo Kesi za Madai Kesi za Jinai Mahkama za Kadhi Wilaya Kesi za Madai

Jumla

(Madai+jinai) Zilizo funguliwa Zilizo tolewa uamuzi Zilizo funguliwa Zilizotolewa uamuzi

Zilizofunguliwa Zilizotolewa uamuzi

Manispaa Malindi Za jinai tu(358) 0 0 358 354

Mwanakwerekwe 373 52 7 321 200 Mjini 737 157

Mwera 121 10 3 111 45 Mwera 56 18

Makunduchi 163 12 3 151 69 Mfenesini 31 15

Chwaka 72 2 2 70 51 Mkokotoni 64 35

Mfenesini 226 5 5 221 125 Makunduchi 25 14

Mkokotoni 621 41 29 580 485 Chwaka 2 2

Mkoani 50 7 2 43 17 Mkoani 57 20

Kengeja 13 6 2 7 3 Kengeja 9 1

Chake chake 140 8 0 132 34 Chake chake 120 18

Wete 60 3 0 57 22 Wete 70 29

Konde 71 4 0 67 44 Konde 51 2

Jumla 2268 150 53 2118 1449 Jumla 1222 311

Kiambatanisho 6: Miswada – Afisi ya Mwanasheria Mkuu 2012/13


Miswada ya Sheria iliyoandaliwa

1. Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Tume ya Mipango;

2. Mswada wa Kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo

3. Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali

4. Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Utalii

5. Mswada wa Kuanzisha Bodi ya Vipimo na Tathmini ya Elimu Zanzibar

6. Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu

7. Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria Mbalimbali

8. Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Shirika la Bandari

9. Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati; na

10. Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa Mahkama ya Biashara Zanzibar



Kiambatanisho 7: Mapato – BPRA (Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali) 2012/13

KASMA ENEO LA MAPATO ZILIZOIDHINISHWA ZILIZOKUSANYWA PUNGUFU

114602 Estate Duty 4,000,000 1,323,600 2,676,400

142208 Usajili Ndoa na Talaka 36,000,000 12,960,500 23,039,500

142233 Usajili Alama za Biashara 48,000,000 39,961,000 8,039,000

142234 Usajili Kampuni 56,000,000 27,572,160 28,427,840

142235 Usajili Majina ya Biashara 25,000,000 8,332,500 16,667,500

142236 Ada mbalimbali 8,000,000 96,250 7, 903,750

142237 Ada za Usajili wa Nyaraka 18,000,000 12,640,000 5,360,000

JUMLA 195,000,000 102,886,010 92,113,990





Kiambatanisho 8a: Ugawaji wa Zakka katika Wilaya - KWNMA



WILAYA WANUFAIKA KIMA WILAYA WANUFAIKA KIMA

VIKUNDI WATU VIKUNDI WATU

MJINI 27 8 40,370,000 KASKAZINI “B” 14 2 26,300,000

MAGHARIBI 28 8 44,100,000 MKOANI 16 3 30,010,000

KATI 18 2 38,632,200 CHAKE CHAKE 8 5 30,370,000

KUSINI 25 1 36,200,000 WETE 13 3 29,810,000

KASKAZINI “A” 22 3 32,325,000 MICHEWENI 10 - 22,500,000

KASKAZINI “B” 14 2 26,300,000 WENGINEO 7 108 145,854,000







Kiambatanisho 8b: Vikundi vilivyosafirisha Mahujaji 2012 – KWNMA

SHIRIKA ME KE JUMLA WA Z'BAR

1. Ahlu Daawa Hajj and Travelling Agency 48 39 87 44

2. Alharamayn Development Fund 51 40 91 66

3-4. Alfirdaus & Hajj Caravan 108 72 180 55

5-6. Jumuiya ya Maimamu & Alkhayria 46 25 71 68

7. Jumuiya ya Istiqama 109 104 213 102

8. Khidmat Islamiyya Charitable Society 65 51 116 32

9-10. Zanzibar Hajj and Travelling Agency (ZAHATA) & Labayka 41 29 70 70

11. Zanzibar Istiqama Hajj Travelling Agency (ZIHATA) 81 87 168 131

JUMLA 549 447 996 568



Kiambatanisho 9a: Idadi ya Wafanyakazi na Elimu Zao 2012/13

Idara/Taasisi Jumla Unguja Pemba Wafanyakazi Kielimu

W/me W/ke W/me W/ke Cheti au chini Stashahada au zaidi % Stashahada au zaidi

Mahkama 351 152 84 80 35 266 85 16%

Afisi ya Mwanasheria Mkuu 50 30 20 0 0 23 27 39%

Tume ya Kurekebisha Sheria 17 9 8 0 0 7 10 47%

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka 87 46 23 14 4 34 53 56%

Idara ya Mipango, Sera na Utafiti 14 7 7 0 0 2 12 75%

Idara ya Uendeshaji na Utumishi 50 29 21 0 0 26 24 35%

Afisi Kuu Pemba 28 0 0 17 11 21 7 32%

Idara ya Mufti wa Zanzibar 42 16 12 10 4 28 14 32%

Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali 34 22 12 0 0 15 19 44%

Afisi ya Mrajis wa Vizazi Vifo 33 5 14 8 6 25 8 21%

Afisi ya Msajili wa Hakimiliki 6 0 5 1 0 0 6 100%

Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana 85 35 18 23 9 62 23 25%

Jumla 797 351 224 153 69 509 288 33%



Kiambatanisho 9b: Idadi ya Wafanyakazi Waliopo Mafunzoni 2012/13

SHAHADA YA UZAMILI STASHAHADA YA UZAMILI SHAHADA YA KWANZA STASHAHADA YA JUU STASHAHADA CHETI JUMLA

IDARA KE ME KE ME KE ME KE ME KE ME KE ME

Mahkama 2 3 4 4 8 17 28 12 78

Afisi ya Mwanasheria Mkuu 2 1 1 4

Afisi ya M/ Mashtaka 1 1 2 2 2 2 10

Tume ya Kurekebisha Sheria 1 1 2

Idara ya Mipango na Sera 3 1 1 1 6

Idara ya Uendeshaji na Utumishi 1 1 1 1 2 1 2 9

Afisi Kuu Pemba 1 1 2 4

Afisi ya Mufti wa Zanzibar 1 3 4

Wakala wa Usajili Biashara na Mali 1 1 2

Afisi ya Mrajis Vizazi na Vifo 2 2

Afisi ya Msajili wa Hakimiliki 1 1 1 3

Kamisheni ya Wakfu na MA 2 2 2 6

JUMLA 5 4 3 5 10 10 23 21 33 12 126

Kiambatanisho 9c: Idadi ya Waliohudhuria Mafunzo ya Muda Mfupi 2012/13

NA IDARA/TAASISI W/WAKE W/UME JUMLA

1 Mahkama 4 4 8

2 Afisi ya Mwanasheria Mkuu 1 3 4

3 Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka 6 4 10

4 Tume ya Kurekebisha Sheria 1 5 6

5 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti 1 1 2

6 Idara ya Uendeshaji na Utumishi 1 2 3

7 Afisi Kuu Pemba 2 1 3

8 Afisi ya Msajili wa Hakimiliki 1 1

9 Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo 2 2

10 Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana 2 2

JUMLA 19 22 41







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.