Habari za Punde

Maoni ya Kamati ya Katiba Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi.

MUHTASARI WA HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA YA BARAZA LA WAWAKILISHI, KUHUSU MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA MWAKA 2013/14


Mheshimiwa Spika, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutujaalia afya na tukaweza kukutana hapa kwa ajili ya kutekeleza wajibu wa kulijenga taifa letu. Aidha napenda kuchukua nafasi hii pia kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kutoa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakari pamoja na watendaji wa Wizara hii wote kwa mashirkiano yao ya dhati waliyoipatia Kamati yetu katika kutekeleza kazi zake za msingi kama ilivyoelekezwa katika kanuni za Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Spika, Kazi yetu ya kupitia Bajeti ya Wizara hii isingekamilika bila ya mashirikiano ya hali ya juu ya wajumbe wote wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambao walifanya kazi hii kwa kujitolea na kujifungia siku nzima bila ya malipo kabla ya siku iliyopangwa kukutana na Wizara na kukipitia kifungu kwa kifungu kwa lengo la kuchambua kwa umakini bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, Naomba nitumie nafasi hii ndogo kuwatambuwa wajumbe wote wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala huku nikithamini mchango wao mkubwa uliofanikisha Kamati hii kuwasilisha muhutasari huu wa hotuba, naomba tena niwataje kama ifuatavyo:-

1. Mhe. Ussi Jecha Simai Mwenyekiti

2. Mhe. Abdalla Juma Abdalla Makamo Mwenyekiti

3. Mhe. Wanu Hafidh Ameir Mjumbe

4. Mhe. Nassor Salim Ali Mjumbe

5. Mhe. Bikame Yussuf Hamad Mjumbe

6. Mhe. Mansoor Yussuf Himid Mjumbe

7. Mhe. Suleiman Hemed Khamis Mjumbe

8. Ndg. Aziza Wazir Kheir Katibu

9. Ndg. Khamis Hamad Haji Katibu

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo sehemu ya kielelezo cha utawala wa nchi, bila ya uwepo wake nchi ingekuwa na utaratibu mbovu wa taratibu na sheria. Wizara hii ndiyo inayoratibu uendeshaji wa moja ya mihimili mitatu ya dola ambao ni Mahakama, kutokana na jambo hilo ndiyo maana nikatangulia kusema kuwa Wizara hii ni sehemu ya kielelezo cha utawala wa nchi kutokana na umuhimu wake huu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria ni miongoni mwa Wizara za Serikali ambazo zinatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi na kukusanya mapato mbali mbali yanayotokana na huduma hizo kwa wananchi. Mwaka uliopita wa Bajeti, Wizara ya Katiba na Sheria ilikadiriwa kukusanya jumla ya Tsh. Milioni 447 katika vyanzo vyake vya mapato.

Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi, 2013, jumla ya Tsh. 288,708,060, zilikusanywa na kuingizwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali, ambazo ni sawa na asilimia 65% ya makadirio. Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja alieleze Baraza lako ni kwanini Wizara yake haikufikia malengo ya ukusanyaji ingawa imevuka malengo hayo.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inapendekeza njia mbadala za kukusanya mapato ya huduma zinazotolewa na Wizara kupitia Taasisi zake mbali mbali, yalipwe kwa utaratibu mwengine kama vile kupitia benki badala ya malipo kufanywa mikononi mwa watu.

Mheshimiwa Spika, Naeleza hivyo kutokana na ukweli kwamba Baraza lako tukufu ambalo lilielezwa kuwa mapato yaliyokadiriwa kupatikana katika bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika kutoka kodi za Mawizarani ni Tsh. Bilioni 20, lakini kwa bahati mbaya kabla ya robo ya mwisho ya bajeti hiyo kumalizika ni Tsh. 8.8 bilioni tu ndizo zilizokusanywa. Kamati yangu haitaki kuamini kuwa Makadirio hayo hayawezi kufikiwa lengo. Kamati inaamini kuwa Makadirio hayo ili yaweze kufikiwa ni vyema utaratibu wa makusanyo ukabadilika na kuwa wa kibenki.

Mheshimiwa Spika, Kwenye miradi ya Maendeleo Wizara ya Katiba na Sheria bado inasuasua na inakwenda taratibu mno, jambo ambalo limesababishwa na kusita kwa baadhi ya miradi yake kama vile mradi wa Kuimarisha Mfumo wa Usajili wa Makampuni na Kuimarisha Afisi chini ya mpango wa kuimarisha mazingira ya Biashara, mradi huu ulitarajiwa kufadhiliwa na Benki ya dunia,kwa bahati mbaya hadi hivi sasa fedha hazikupatikana.

Mheshimiwa Spika, Miradi mengine ambayo ilianza vizuri lakini sasa hivi inakwenda Kwa kusuasua ni pamoja na ujenzi wa jengo la Afisi ya Mwanasheria Mkuu, inasikitisha kuona hatua iliyofikiwa ya ujenzi ule imekwama njiani, kamati yangu inaiomba Serikali kurekebisha mipango na kuhakikisha kuwa inatafuta fedha za kumalizia ujenzi wa jengo lile.

MAHAKAMA

Mheshimwa Spika, Kamati imebahatika kufanya ziara katika baadhi ya majengo ya mahakama za Wilaya na kujionea hali mbaya ya baadhi ya majengo ya Mahakama hizo ambayo ndiyo taswira ya eneo la kutolea uamuzi wa mashauri mbali mbali yanayofikishwa hapo. Mfano wa majengo ya mahakama ambayo hali yake haiwezi kusubiri bajeti yetu itoshe ndiyo yafanyiwe kazi ni jengo la mahakama ya Mwanakwerekwe, Mfenesini na Makunduchi.

Mheshimwia Spika, Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe hali yake ni mbaya sana, chumba wanachotumia waendesha mashitika na polisi kwa ajili ya kutayarisha ushahidi na mashahidi hakipo katika mazingira mazuri hata kidogo ya kuendesha shughuli hizo. Ni chumba kidogo cha futi kumi kwa tisa, watu zaidi ya ishirini wanakitumia, vielelezo vya ushahidi kama chupa za mikojo, kemikali, madumu ya ulevi wa kienyeji, mabati, nondo nakadhalika, vyote vimejumuishwa na binaadamu wanaofanya kazi hapo. Aidha chumba hicho ni mazalia mazuri ya wadudu waharibifu kama vile panya ambapo wadudu hao huzaliana kutokana vitu nilivyovitaja hapo juu vikiwekwa kama ushahidi lakini kutokana na ufinyu wa sehemu hiyo na vitu hivyo hukaa muda mrefu husababisha ushahidi huo kugeuka na kuwa taka taka ambazo zina athari kwa afya ya binadamu. Vile vile katika Mahakama hiyo Kamati ilipata bahati ya kuoneshwa chumba cha kuwekea mahabusu ambacho ni kidogo sana na kimekuwa na msongamano mkubwa baadhi ya wakati.

Mheshimiwa Spika, Hali siyo hiyo tu, kamati yangu ilitembelea Mahakama ya Wilaya ya Makunduchi, kwakweli hali ni mbaya sana na inasikitisha kuona kuwa sehemu ambayo mwananchi anategemea kupata haki zake za msingi kisheria liko kama jinsi tulivyolikuta ambapo hivi sasa jinsi lilivyo nathubutu kusema ni kama gofu la zamani ambalo linavuja, halina dari, sakafu yake imechimbika hali ya hewa ya vumbi na ukungu ndani ya jengo , kutokana na hali hiyo Napata nguvu ya kusema kuwa jengo hilo halifai kutumika kutokana na mazingira halisi ya jengo hilo kuenda kinyume na mazingira ambayo binadamu yeyote yule angependa kukaa na kufanya kazi zake kwa utulivu.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na ufinyu wa muda, kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, haikuweza kutembelea majengo mengine ya mahakama za Wilaya, lakini imepata taarifa za uhakika kuwa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mfenesini halina hata chumba cha waendesha mashita na badala yake waendesha mashitaka wanatayarisha mashahidi wakiwa kwenye gari.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Katiba na Sheria imeamua kuyaweka wazi mambo iliyoyaona katika kipindi kifupi tu tokea kuundwa kwa kutaka Baraza lako lielewe kuwa tunapotoa pongezi kwa Waheshimiwa Mawaziri kwa kufanya kazi vizuri, tusisahau kuwapa pole watendaji wanaoumia kwa kufanya kazi kwenye mazingira magumu huku tukiwategemea wafanye hivyo kwa ufanisi. Licha ya yote hayo, kamati yangu imesikitishwa sana na kasma ndogo ya fedha za maendeleo iliyopewa Mahakama katika bajeti ya mwaka huu 2013/2014 kwa ajili ya matengenezo ya majengo yake.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu imesikitishwa sana wakati ilipokuwa ikipitia bajeti kwa kugundua utofauti wa fedha katika fungu la 36 la fedha za maendeleo ambapo kulijitokeza kasma mbili tofauti, moja ikiwa ni shilingi milioni 300 na ya pili ni milioni 150 na baada ya kutaka maelezo Kamati ilielezwa kuwa kasma ya shilingi milioni 150 ndio sahihi.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kuna haja kwa Wizara ya fedha kuwa makini katika uwekaji wa fedha katika bajeti ili kuepuka utata kwa Wajumbe hali ambayo inaweza kusababisha mzozo ndani ya Baraza hasa ukizingatia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ni ndogo katika maeneo ya Mahakama ambapo Kamati yangu haikuridhishwa na fedha zilizotengwa hasa tukizingatia kuwa kuna changamoto nyingi tulizozieleza.

MWANASHERIA MKUU

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Mwanasheria Mkuu imeongezewa majukumu kwa kupewa jukumu la kuwasimamia wanasheria wote wa Serikali, kuwajengea uwezo na kuratibu utendaji kazi wao uwe wa ufanisi. Kamati yangu inamashaka na utekelezaji wa azma hiyo kwa kuwa bajeti ya mwaka huu ya Tsh. 919 milioni ni ndogo mno ambayo haikidhi utekelezaji wa majukumu hayo ya ziada.

Mheshimiwa Spika, Kamati inakumbusha tena wasiwasi wake wa kusita kwa ujenzi wa jengo la Afisi za Mwanasheria Mkuu ujenzi ambao ulianza vizuri lakini hivi sasa umesimama. Kamati inaiomba Serikali kukata pua na kuunga wajihi, kwa kutafuta fedha na kupunguza matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima ili waweze kusaidia jengo lile limalizike ili liweze kutumika kama ilivyokusudiwa.



TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

Mheshimiwa Spika, Tume ya Kurekebisha Sheria ni miongoni mwa Taasisi nyeti zilizopo hapa nchini kutokana na ukweli kwamba chombo hiki kina jukumu la kuhakikisha kuwa kinatafsiri sheria hizo katika lugha nyepesi na kuzifanya zieleweke kwa wananchi. Kazi hii siyo nyepesi hata kidogo, inahitaji utulivu na wataalamu wa kada tofauti zinazohusu Sheria husika. Sambamba na hilo elimu kubwa kwa wananchi inatakiwa itolewe ili kuwawezesha wananchi hao kushirikina na Tume katika kuzifanyia marekebisho sheria zetu wakati wowote wananchi watakapohisi utekelezaji wa sheria hizo ni mgumu.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuona umuhimu huo, kamati inaishauri Serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa Ofisi ya Tume kwa kuwa na Afisi za kudumu badala ya kuhama hama na kukodi majengo kwa ghrama kubwa. Aidha Kamati imeona jinsi Tume hii inavyotumia fedha nyingi za kulipia kodi ya Ofisi ambapo fedha hizo hizo kama zingetumika kidogo kidogo kujenga jengo la Ofisi za Tume lingekuwa katika hatua nzuri kwa sasa.

AFISI YA WAKALA WA USAJILI WA MAKAMPUNI

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Wakala wa Usajili wa Makampuni inahitaji kuimarishwa kwa kuhakikisha inakuwa na watendaji wenye uwezo na utaalamu mkubwa. Kamati imepata wasiwasi wa kukimbia kwa wataalamu wa Afisi ya wakala wa Usajili wa Makampuni hasa katika fani za Mawasiliano na kompyuta, Mheshimiwa Spika, uondokaji huu unaelezwa kusababishwa na maslahi madogo wanayolipwa wataalamu wa fani hizo adimu.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kuwa katika kuifanya Afisi ya Wakala wa Usajili wa Makampuni kutatua baadhi ya changamoto zake basi iwezeshwe kubakisha asilimia maalum ya makusanyo ya fedha za huduma wanazozitowa. Hatua hii inaweza kupunguza utegemezi wa Afisi na kujiendesha yenyewe bila ya mwega wa Serikali.

AFSI YA MSAJILI WA HAKIMILIKI

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Msajili wa Haki Miliki tumeibebesha dhima ya kusimamia haki za wasanii, kutokana na jukumu hilo kubwa tuliyoibebesha Afisi hii ni lazima tukumbuke kuwa ni lazima watendaji wa Afisi hii wapatiwe vitendea kazi vitakavyowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Miongoni mwa vitendea kazi muhimu ni pamoja na usafiri ambao utaisaidia ofisi na kurahisisha kazi za kila kila siku. Kutokana na kilio cha muda mrefu kilichokuwepo katika taasisi hii, tunapenda kutoa pongeza kwa Serikali katika bajeti ya mwaka huu kulizingatia suala hilo kwa kuweka kasma kwa ajili ya ununuzi wa gari. Aidha Kamati ilipotembelea katika taasisi hii ilipewa taarifa kuwa baadhi ya wataalamu wake wanahamia katika taasisi nyengine kutokana na mishahara midogo wanayolipwa, kutona na hali hiyo, Kamati inaiomba Serikali ilifikirie suala hilo ili wataalamu hao wanaosomeshwa na Serikali waweze kuzitumikia taasisi zinazowagharamia katika masomo yao.

Mheshimiwa Spika, Mwaka huu wa fedha 2013/14, Afsi ya Msajili wa Hakimiliki imekadiriwa jumla ya Tsh.140 milioni zikiwa ni ruzuku ya mishahara na shughuli nyengine za uendeshaji. Hata hivyo Kamati inamashaka makubwa na kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kutokana na ukweli kuwa fedha hizo ni kidogo na tunahisi kuwa fedha hizo huenda zisikidhi mahitaji katika uendeshaji wa shughuli za Afisi hiyo kutokana na majukumu mazito yaliyokuwepo. Aidha, wasiwasi mkubwa wa Kamati yetu unakuja kutokana na Afisi hii kukosa jengo la ofisi na wataalamu.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Serikali kudhibiti upotevu na wizi wa kazi za wasanii kwa kuiwezesha Afisi hii kufanya marekebisho ya Sheria yake ambayo ingeweka sharti la kutorejesha leseni kwa vituo vya utangazaji ambavyo havilipi mirahaba.

AFISI YA MRAJIS WA VIZAZI NA VIFO

Mheshimiwa Spika, Kamati wakati inachunguza fungu 36 la Wizara ya katiba na Sheria kwenye kifungu 0901 cha Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo haikuridhika na maelezo iliyopewa kuhusiana na kifungu hicho. Kutokana na kutoridhika huko Kamati imeagiza marekebisho yafanyike kwa baadhi ya vifungu ambavyo kasma zake zimewekwa kwenye vifungu visivyoombewa matumizi. Marekebisho hayo yamefanyika kama kamati ilivyo agiza kama ifuatavyo kijifungu 220408 gharama za umeme zilikuwa sifuri, hivi sasa kijifungu hicho kimewekewa fedha zilizokuwa katika kijifungu 220302 cha safari za nje ambazo ni Tsh. 4,535,000. Kijifungu 311203 cha fedha za Ununuzi wa vyombo vya Usafiri, kimepunguzwa Tsh. 1.5 milioni ambazo zimeongezwa kwenye kifungu 220301 cha safari za ndani na hivi sasa kimewekewa Tsh. 7,500,000 kutoka 600,000 za awali.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Serikali kuisadia Afisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo kwa kuitafutia wafadhili kusaidia utoaji wa taaluma kwa wanachi hasa katika kukabiliana na changamoto ya kughushi vyeti vya kuzaliwa. Aidha, kamati inaiagiza Idara hii kukutana na Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari kueleweshana kuhusu nani hasa mwenye dhamana ya kuthibitisha uhalali wa cheti cha Kuzaliwa.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Afisi ya Mrajisi wa Vizazi na Vifo kutokana na ukarabati wa vituo vya Wilaya ya Kaskazini “A” kwa kituo cha Gamba, Wilaya ya Kaskazini “B” kwa kituo cha Mahonda, kituo cha Wilaya ya kati kilichopo Dunga na kituo cha Wialaya ya Kusini kilichopo Makunduchi, Kamati iliridhika na ukarabati uliofanyika na inaiomba Ofisi hii iendelee na juhudi za kuvikarabati vituo vyake vyote vilivyopo nchini. Aidha Kamati inaiomba Serikali ilizingatie suala la wafanyakazi wa Ofisi za vizazi na vifo hasa wale walioko katika vituo mbali mbali ambao inaonekana wanfanya kazi katika Wizara mbili, hasa linapokuja suala la posho la wafanyakazi hao ambapo tatizo linajitokeza la kuijua ni Wizara ipi inayohusika na malipo ya posho za wafanyakazi hao. Hivyo Kamati inaomba suala hilo lizingatiwe na Wizara zote kwa kukaa pamoja na kuamua nani atawajibika kwa wafanyakazi hao.

KAMISHENI YA WAKF NA MALI YA AMANA

Mheshimiwa Spika, Wakati wa kuwasilishwa Bajeti ya mwaka unaomalizika wa fedha, 2012/13, Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana ilikuwa katikati ya mijadala mizito ya Wajumbe wa Baraza hili, hasa katika suala la nyumba za amana za Michenzani zilizo chini ya amana ya Kamisheni ambazo zilizokuwa mikononi mwa Idara yaNyumba. Kwa mujibu wa maelezo tuliyopatiwa ni kuwa Kamisheni inashindwa kuzifuatilia suala hili kutokana na kukosa “Appointment” na wahusika wa Idara ya Nyumba, aidha kwa majibu wa maelezo hayo inaonekana kuwa Mkurugenzi wa Idara ya nyumba anawakwepa watu wa wakfu kwa ajili ya kukaa na kulizungumzia suala hili na hatimaye makabidhiano ya nyjmba hizo yaweze kufanyika. Kutokana na hali hiyo Kamati inaiomba Wizara kuwasiliana na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo na hatimayer nyumba hizo zikabidhiwe kwa wahusika ambao ni Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.

Mheshimiwa Spika, Suala hilo bado halijamalizika na kamati haitapenda lijitokeze tena katika mijadala ya Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2013/14. Kamati imeshatoa agizo kwa Kamisheni ya Wakf kukutana haraka na Idara ya Nyumba kulimaliza suala hili.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaguswa na suala la malipo ya kodi za nyumba za Wakf ambapo kodi hizo zinalipwa kwa kiwango kidogo na wapangaji. Wapangaji wengi wa nyumba hizo wanapangishwa kwa fedha kidogo chini ya Tsh. 50,000/= huku wao wakizipangisha kwa bei ya juu ambayo ni zaidi ya Tsh. 200,000/= Mheshimiwa Spika, hii ni dhuluma hasa ukizingatia mazingira ya nyumba zenyewe.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri kamisheni kuandaa mikataba mipya itakayokuwa na vipengele visivyoruhusu mikataba mingine kwa wanaopangishwa (sub letting).

AFISI YA MUFTI

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Katiba na Sheria inatambua mchango wa Afisi ya Mufti katika kuimarisha mshikamano na ustawi wa maadili mema ya jamii yetu. Kama tunavyojua kuwa jamii yetu hivi sasa imekumbwa na janga kubwa la mporomoko wa maadili na vitendo viovu hasa vya udhalilishaji wa watoto na wanawake kijinsia katika maeneo ya utoaji wa taaluma kama vile shule, madrasa, majumbani pamoja na meneo mengine.

Kutokana na hali hiyo, Kamati inaiomba Serikali kushirikana na Afisi ya Mufti kwa kuipatia fedha za kufanya kampeni na kutoa elimu ya mwamko wa jamii kupambana na vitendo hivyo. Aidha, kamati inapendekeza Afisi ya Mufti kuandaa utaratibu mpya wa kuhakiki madrassa na kutayarisha leseni maalumu kwa ajili ya Walimu wa Madrassa hizo, ili kubaini baadhi ya watu waovu wanaojipenyeza katika Madrassa kwa nia mbaya na kudhalilisha watoto kijinsia.

AFISI YA MKURUGENZI WA MASHITAKA

Mheshimiwa Spika, Kamati inachukua fursa hii kuipongeza Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka katika kuimarisha mpango wake wa kueneza uendeshaji wa mashitaka kiraia katika Wilaya zote. Mpango huo utawezesha Mahakama nyengine za Wilaya ambazo hazijafikiwa na waendesha mashitika wa Serikali kuanza kuutumia utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, Kamati inasikitika sana kuona juhudi hizo zinarudishwa nyuma kutokana na hizo fedha kidogo zinazotengwa katika bajeti kutopatikana kwa wakati. Hivyo Kamati inaiomba Serikali kuhakikisha kuwa fedha hizo kidogo zinazokuwa zimetengwa zinapatikana kwa wakati ili yale malengo ya ndani ya taasisi husika yaweze kutekelezeka. Aidha ukosefu huo wa fedha au ucheleweshaji huo huleta athari kubwa ya kiutendaji ktika Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa uendeshaji wa mashitaka kiraia unapokwama maana yake tunaendelea kuruhusu uendeshaji wa kesi katika Wilaya kwa kutumia Polisi ambao ni hao hao wanafanya upelelezi wa kesi na wakati mwengine kukosa ufanisi wa uendeshaji wa kesi zenyewe na hatimaye watuhumiwa wa uhalifu wanaachiwa pengine kwa kukosa ufanisi wa kuendesha kesi tu na wala sio ushahidi.

Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha unaomalizika 2013/14, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ilikadiriwa kupata kiasi cha Tsh. 250 milioni, fedha za maendeleo, ambazo hadi mwezi Machi, 2013 ni Tsh. 100 milioni tu ndizo walizopatiwa kati ya fedha hizo. Kamati imeridhika jinsi fedha hizo kidogo zilivyotumika katika ujenzi ya nyumba ya Mwendesha Mashitika Mkoa wa Kusini Unguja, Kuimarishwa kwa Afisi ya Pemba na Kununuliwa Kiwanja cha Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu hairidhishwi hata kidogo na mwenendo huu, fedha za maendeleo ilizopatiwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mshitiaka katika mwaka huu wa fedha 2013/14 ni Tsh. 100 milioni ambazo kamati imeshindwa kujuwa zitatumika vipi mwaka huu wakati Afisi imebakisha njiani malengo ya mwaka jana ambayo yanahitaji zaidi yaTsh. 150 kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, Hali hiyo inamaanisha kuwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mshtaka kwa mwaka huu wa fedha haitaweza kukamilisha mipango yake, hii ni kutokana na kutokamilika kwa mipango ya mwaka wa fedha uliopita ambayo pia inahitaji kukamilishwa kabla ya utekelezaji wa mipango ya mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Hali hii inasikitisha na inaipa changamoto kubwa Kamati ya kujiuliza endapo ni kweli tunapanga mipango yetu kwa uhalisia kwa kuweka vizuri vipaumbele vyetu?. Kutokana na hali hii Kamati inainasisitiza Serikali kuitazama jicho la pekee Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ambayo imebebeshwa majukumu mazito na yenye hatari, huku maslahi ya wafanyakazi wake yakiwa madogo. Kwa mwaka huu wa fedha kifungu cha posho la mazingira magumu cha Afisi hii kina kasma sifuri, licha ya mazingira ya hatari wanayofanyakazi wafanyakazi wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.

Mheshimiwa Spika, Mazingira ya kazi ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mshitaka yana changamoto nyingi ambazo zinahitaji uwezo wa kifedha ambao utasaidia kuzipunguza changamoto hizo. Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Afisi hii lakini bado kuna tatizo la uelewa wa wananchi katika kutoa mashirikiana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, hasa katika suala la kutoa ushahidi. Kesi nyingi zinashindwa kuendelea kutokana na wananchi kushindwa kutoa mashirikiano na Afis na hatimaye kesi kufutwa, tatizo hili linahitaji kampeni na elimu kubwa kwa umma ambayo kamati inashauri Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ipatiwe fedha za kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, Hakuna hatia bila ya Ushahidi, hiyo ni kaulimbiu ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ambayo kamati inakubaliana nayo. Ukosefu wa kukusanya ushahidi kwa njia za kisasa unasababisha kazi ya Waendesha Mashitaka kuwa ngumu. Kamati inakumbusha ahadi ya Serikali ya kupatikana kwa kifaa cha DNA ambacho kitasaidia sana ushahidi wa kitaalamu badala ya kutegemea ushahidi wa kiramli wa kuona peke yake hasa katika kesi zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru tena kwa kunipa fursa hii na kunivumilia muda wote kutoa Hotuba hii kwa niaba ya kamati. Aidha, nawashukuru wajumbe wa Baraza kwa utulivu na ukimya wao wakati nikiwasilisha maoni haya ya kamati. Ni imani yangu wataipokea, kuichangia na hatimaye kuipitisha bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria na hatimaye kumsaidia Waziri kurejeshewa mafungu yake yaliyopunguzwa katika baadhi ya Taasisi zake.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Ahsante

Ussi Jecha Simai

Mwenyekiti,

Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,

Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.