Habari za Punde

Kesi 23 za Ubakaji Zaripotiwa Mahakama ya ChakeChake.

Na Shemsia Khamis, Pemba
KESI 23 za ubakaji zimeripotiwa katika mahakama ya mkoa ya Chake Chake, kuanzia Januari 2012 hadi Julai mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Karani wa kesi, Abass Mwinyi Mkuu alisema kati ya kesi hizo ,wilaya ya Chake Chake inaongoza kwa kuwa na kesi 13, wakati wilaya ya Mkoani imeripoti kesi 10.

Alisema kati ya kesi hizo,kesi tisa tayari zimeshaondolewa mahakamani kutokana na kukosekana ushahidi.

Alisema kesi nyengine mbili zimeondolewa kutokana na walalamikaji wenyewe kuiomba mahakama kuziondoa, kutokana na sababu zao binafsi.

Alisema kesi 14 bado zipo mahakamani hapo zinaendelea katika hatua mbali mbali.

Hata hivyo alisema bado jamii ina muamko mdogo wa kuziripoti kesi za aina hiyo, kutokana na kuoneana muhali kwa jamii.

Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama ya Mkoa Chake chake, Khamis Ramadhan Abdalla, alisema kuna chanagamoto kadhaa zinazowakabili katika kusikiliza kesi za ubakaji, ikiwa ni pamoja na mashahidi kukataa kutoa ushahidi.

Hata hivyo aliitaka jamii kuwa na ushirikiano ili kuhakikisha vitendo vya ubakaji vinatokomezwa kwa kushirikiana na mahakama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.