Habari za Punde

Mahakama, Bodi Rufaa za Kodi Kumaliza Kero za Wafanyabiashara

Na Salum Vuai, Maelezo
HATIMAYE malalamiko ya walipa kodi wa Zanzibar kuhusu mambo mbali mbali yanayohusiana na kodi, yamepata jukwaa la kuyasemea kufuatia kuzinduliwa kwa bodi ya rufaa za kodi pamoja na mahakama ya rufaa za kodi.

Vyombo hivyo vimezinduliwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee katika ukumbi wa mikutano wizarani kwake Vuga mjini Zanzibar.

Akizungumza na wajumbe wa bodi na mahakama hiyo, Mzee aliwaasa kutoa maamuzi kwa kuzingatia haki na maadili yanayoongoza taaluma yao, ili kuweka mazingira mazuri kwa walipa kodi na taasisi zinazokusanya kwa maana ya serikali.

Wakati wakisikiliza kesi za walipa kodi, aliwataka kutoziangalia taasisi za serikali kwa uhalisia wake kwamba labda wanapaswa kuzikingia kifua, bali watoe hukumu ya haki kwa pande zote.

“Mkifanya hivyo, mtashindwa kuendesha kesi kwani ni wazi utashi utatawala zaidi, wachukulieni wote walalamikaji na wanaolalamikiwa kwa misingi ya haki ili hukumu na maamuzi yenu yaridhishe wote,” alisema.

Aidha aliwasisitiza kufanya kazi bila kusikiliza maneno ya mitaani, bali wazingatie taaluma yao ambayo ndiyo itakayowajengea heshima na hadhi mbele ya jamii.

Alisema, hatua ya serikali kuanzisha bodi na mahakama za kushughulikia kesi za kodi, imelenga kuweka hali nzuri na utulivu kwa wafanyabiashara, ili wazidi kuhamasika kulipia kodi ambayo ni umuhimu kwa kujenga nchi na kuiletea maendeleo.

Kwa upande mwengine, alivishauri vyombo hivyo viwili kufanya kazi kwa ushirikiano kunapotekezea mkanganyiko wa kesi zinazofikishwa kwao ili hatimaye watoe maamuzi ya haki kwa pande zinazoshtakiana.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya rufani za kodi, Khamis Ramadhan Abdalla, aliahidi kufuata ushauri wa waziri huyo wakati wakifanya kazi kwa lengo la kuwatendea haki wahusika wote.

Aidha alisema, bodi hiyo ya rufaa za kodi haiwahusu wafanyabiashara na walipa kodi wengine pekee, bali hata taasisi zinazokusanya kodi nchini zinazoweza kupeleka malalamiko dhdi ya watu wanaokwepa au kukiuka taratibu za kodi.

Fatma Saleh Amour, mjumbe kutoka mahakama ya rufaa za kodi, alieleza kuwa chombo hicho hakitaegemea upande wowote, bali kitajitahidi kufuata maadili na miongozo inayoongoza taaluma yao.

Mwanzoni mwa wiki hii, kundi la wafanyabiashara wa makontena Michenzani, waliungana kwenda katika ofisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini, kudai punguzo la kodi wanayotozwa huku wakisema biashara zao hazina tija yoyote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.