Habari za Punde

Mazungumzo kati ya Redio Ujerumani DW na Mansoor Yussuf Himid

 
Mansoor Yussuf Himid
Idhaa ya Kiswahili ya radio ya Ujerumani, leo hii katika kipindi chake cha mchana (saa za Afrika Mashariki) imetangaza mahojiano mafupi ambayo yalifanywa na mtangazaji wa redio hiyo na aliyekuwa Mbunge wa Kiembesamaki, Mjini Magharib, Unguja aliyevuliwa uanachama na hivyo kupoteza nyadhifa zake kichama na Kiserikali, ndugu Mansoor Yussuf Himid na kumwuliza maswali kadhaa kuhusiana na kilichotokea kwenye uamuzi wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinzuzi kilichofanyika huko Dodoma na kutangazwa kwenye vyombo vya habari hapo jana.

Hapa ninanukuu nilichokisikia.

Mwandishi wa DW: Umeuchukulia vipi uamuzi huo?

Mansoor Yussuf Himid: Nimepata taarifa hizo za Chama Cha Mapinduzi, chama changu kunivua uanachama. Niseme kwamba namshukuru Mwenyezi Mungu na nimepokea kwa hatua hii kwa namna ilivyotoka.

Mwandishi: Kwa maana chama ambacho umekulia humo na mzee wako Yussuf Himid alikuwa mwasisi leo hii haumo?

Himid: Ndiyo wenzangu wameashaamua hivyo. Basi hatua hii yatosha hayo.

Mwandishi: Na zipi fikira zako zilizokujia haraka haraka kichwani baada ya uamuzi huu?

Himid: Nimemshukuru Mwenyezi Mungu

Mwandishi: Umefika ukingoni katika uwanja wa siasa?

Himid: Bado ni mapema mno na sikuwa na dhamira ya kuzungumza lakini wewe mwenzangu umeniuliza na
unanipigia simu hii siku ya tatu ya nne mfululizo, nikasema nikupe heshima angalao basi niseme mawili matatu, na kwa sasa yatosha. Lalini wakati utafika nitakapokuwa nimejihahikishia mimi mwenyewe, kwamba saa niko tayari kuzungumza, nitasema hayo machache ambayo ninayo na ninadhani yanafaa kuzungumzwa.

Mwandishi: Kuna tuhuma kadhaa zimetajwa ambazo zimesababisha pengine uondolewe chamani, hizi unazizungumziaje?

Himid: Ndugu yangu, nimezisikia hizo tuhuma. Na kama nilivyokwambia  mwanzo, unajua wanasema “anayekutukana hakuchagulii tusi,” sasa madamu zimeletwa hizo tuhuma na wenzangu wameziona za msingi kujadiliwa na ndiyo za msingi wa mimi kuvuliwa uanachama, kama nilivyokwambia namshukuru mwenyezi mungu.

Mwandishi: Kwa safari hii, kwa yale yote yaliyosemwa bila shaka wasikilizaji wangependa kujua --kuna ukweli katika hili, kuna uoneaji katika hili-- wewe binafsi unasemaje?

Himid: Hatua hii bado ni ya  mapema mno.

Mwandishi: Unazungumziaje demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi?

Himid: Nikiwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikiwa Mzanzibari kwenye huu utaratibu unaoendelea wa kutafuta hiyo katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nitaendelea kuzungumza yale amba yo mimi ninayaamini.

Mwandishi: Kwa kutukumbusha tu, yapi ya msingi ambayo wewe unaamini?

Himid: Mimi ninaamini huwezi kuwa na katiba ya maana, ya msingi inayoridhiwa na wingi wa watu ikiwa hakuna uhuru wa watu kujieleza. Ni udaganyifu na upotoshaji mkubwa. Huwezi kuwa na Katiba ya maana, na inayoandikwa na watu wa maana, na nchi ya maana ikiwa hakuna fursa ya watu kueleza yale waliyokuwa nayo ili hatimaye maamuzi yawe yale ambayo yaliridhiwa na wengi. Kwa hivyo naendelea kusema hilo niliendelea kuliamini hilo huko, ninaendelea kuliamini hilo hivi sasa. Na ikiwa hilo halijapatikana basi nafikiri tunaendelea kucheza mchezo ambao hauna mwelekeo.

Mwandishi: Una wasiwasi kwamba pengine rasimu ya Katiba Mpya haitazaa matunda mema ya kuleta Katiba iliyo bora kwa maslahi ya wote?

Himid: Matumaini ya Wazanzibari kwa hapa tulipofika hayazuilka. Wakati wake utafika. Limezama katika nafsi na nyoyo za Wazanzibari na wanachokitaka  ni very simple, wanataka haki hayo ya kusikilizwa, wanataka haki yao na wao kuwa na nafasi yenye heshima iliyo kuwa ya haki na ya  usawa ndani ya Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwandishi: Hili ni moja kati ya ya sababu ambazo pengine zimesababisha uondolewe katika Chama, kwa nini umeshindwa kutumia majukwaa ama mikutano ya chama kufanikisha azma yako?

Himid: Looh, ndugu yangu kama nilivyokwambia wazi, sikuwa tayari kuzungumza hivi ghafla.

Yalikomea hapo mazungumzo hayo.

2 comments:

  1. ukiwa katika madaraka ya kidunia kumbuka kamla hujaamua kwani ni furaha au mauzi na hao ccm wakumbuke wanamwisho wao.wakiwa kiongozi basi kwanza uweke mazingira mazuri jela(prison)

    ReplyDelete
  2. Kama ingekuwa tupo katika nchi zilizoendelea basi muheshimiwa ungewashitaki hao CCM ukala mapesa yako lakini.........., mana hao wakuu wa hicho chama waongo wote walisikika wakisema mtu atoe maoni yake binafsi sasa naona kama walikua na mpango huu ili wawafukuze kazi watu, hata watu wanofanya kazi serekalini waliogopa kutoa maoni kwa sababu kama hizi

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.