Habari za Punde

Mufti Mkuu Autaka Uongozi wa Al yamin kutowa Elimu kwa Vijana.

Na Aboud Mahmoud

UONGOZI wa Jumuiya ya Alyamin umeshauriwa kuzidhisha bidii katika kuwafundisha vijana na watu mbali mbali misingi bora inayotokana na dini ya Kiislamu.

Ushauri huyo umetolewa na Mufti Mkuu wa Zanzibar,Sheikh Saleh Omar Kaabi,wakati alipokuwa akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye sherehe za Baraza la Eid el Fitry zilizoandaliwa na jumuiya hiyo huko katika ukumbi wa Baytul-Yamin Malindi.

Mufti huyo alisema kwamba ingawa jumuiya hiyo ipo katika mstari wa mbele katika kuhamasisha na kuendeleza uislamu,lakini ipo haja kuongeza bidii ili visiwa vya Zanzibar viweze kurudi katika hadhi yake kama hapo mwanzo.

Alisema kwamba miaka ya nyuma Zanzibar ilikuw ani kitovu cha mambo mbali mbali yanayohusu uislamu ikiwemo usomaji wa Quraan na vitabu vyengine,lakini sasa hivi imepungua hadhi hiyo.

"Hapo awali miaka ya nyuma tulikuwa tunajivunia nchini kwetu kuwa tuna masheikh waliobobea na watu kutoka nchi mbali mbali walikuwa wanakuja kwa ajili ya kusoma dini,hivyo napenda kutoa ushauri kwa uongozi wa jumuiya hii kuhakikisha kwamba Zanzibar inarudi katika hadi yake,"alisema.

Aidha Mufti Saleh alisema kwamba hakuna haja ya kuangalia kabila la mtu katika maswala ya kidini ambapo alisema ni jukumu la kila muislamu kuhakikisha kwamba uislamu unazidi kusonga mbele.

Alifahamisha kwamba vijana wengi wamekuwa wakizitumia skukuu za kidini kwa kufanya mambo maovu,hivyo alisema jamii inahitajika kushirikiana na Serikali katika kupiga vita vitendo ambavyo vinachangia kuchafua uislamu.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,Dk Omar al-Sheikh,alisema kwamba Jumuiya yake imejipanga kikamilifu katika kuhamasisha hususan vijana katika maswala mazima ya dini.

Alisema kwamba kutokana na mashirikiano ya watu mbali mbali Jumuiya ya Alyamin imeweza kuwakusanya vijana katika kuwafunza mambo ya kheri ambayo yatasaidia kuutangaza uislamu kuwa ni dini ya amani na isiyopenda fujo.

Sherehe za Baraza la Eid hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Jumuiya hiyo ambapo katika mwezi mtukufu wa Ramadhan jumuiya hiyo iliweza kufanya mambo mbali mbali ikiwemo kufuturisha mwezi mzima katika eneo liliopo msikiti pamoja na eneo la makaburi huko Kiyanga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.