Na Khamis Mohammed, Jiangxi-China
NCHI za Afrika bado zina nafasi ya kupiga hatua kubwa ya maendeleo ikiwa viongozi wake watazitumia vyema rasilimali zilizomo ndani ya mataifa hayo.Hayo yalielezwa na Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji ya Kamati ya Chama cha Kikoministi cha China jimbo la Jiangxi, Yao Yaping, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya Zanzibar wanaonedelea na mafunzo jijini hapa.
Alisema, nchi nyingi za Afrika zimejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo kama zitatumiwa vizuri, zitaweza kuzipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambayo yatawaondosha wananchi wake katika umasikini na huduma mbovu za kijamii ikiwemo miundombinu ya kimawasiliano na usafirishaji.
Yaping alisema, rasimali kama hizo ndizo zilizoisaidia China kupiga hatua iliyopo sasa huku rasilimali watu wakitumika moja kwa moja kuibadilisha nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu duniani.
Alisema, pamoja na misingi mizuri iliyojengwa na muasisi wa taifa la China marehemu Mao Dzedong, lakini pia viongozi waliomfuata shujaa huyo, waliamini kuwa rasilmali za taifa hilo ndizo pekee ambazo zingeweza kuikomboa nchi hiyo kiuchumi na kijamii bila kuweka mbele maslahi binafsi.
“China ni nchi kubwa sana iliyojengwa kimajimbo, lakini hakuna tofauti ya kimtazamo kuanzia mwananchi hadi kiongozi wa juu, ubinafsi wa kiongozi hauna nafasi nchini hapa,” alisema Yao.
“Kiongozi wa kweli ni yule anayejali maslahi ya wengi badala ya kujilimbikizia mali na kupenda madaraka,” alisema.
Aidha alisema, mara baada ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii, China ilifungua ukurasa wa kuijenga nchi hiyo katika misingi ya kujitegemea huku wananchi wakipewa nafasi ya kwanza kuhakikisha wanalijenga taifa lao kwa kujitolea kuwapatia huduma bora na zenye kujali maslahi ya umma.
Alisema, China bado inaendelea kuwa muumini wa chama kimoja, lakini inatoa fursa kubwa kwa wananchi kuendelea kuheshimu mila na silka zao na kutoa uhuru wa kimawazo katika kulijenga taifa hilo.
Jimbo la Jiangxi lina ukubwa wa kilomita za mraba 166,900 na idadi ya watu milioni 45 ambapo limezungukwa na milima mikubwa na mito ambayo hutumika kama sehemu ya utalii wa ndani na wageni wanaotoka mataifa mbalimbali duniani.
Mbali na milima hiyo mikubwa iliyojengewa miundombinu bora ya barabara inayowawezesha mtalii kuifikia kwa urahisi pia jimbo la Jiangxi lina idadi kubwa ya maporomoko ya maji yanatoka milimani ambayo huwavutia watalii huku likishika nafasi ya tatu kwenye vivutio 10 bora vinavyohifadhiwa.
Pia jimbo la Jiangxi limebeba sehemu kubwa ya kumbumbuku za muasisi wa taifa la China ambazo pia hutumika kiutalii sambamba na kuenzi historia ya chini na majemedari wake waliopigana kuikomboa chini hiyo yenye watu bilioni 1.3
Katika hatua nyengine, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari China (CJA), Su Haihe, alisema uhuru wa vyombo vya habari nchini China upo na kwamba unaendelea kuheshimiwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Zanzibar waliotembelea ofisi za chama hicho jijini Beijing, Haihe, alisema vyombo vya habari vya China vimekuwa vikifanyakazi katika hali uweledi wa taaluma ya habari bila ya kuingiliwa na serikali, huku maslahi ya taifa yakipewa kipaumbile.
“China ina idadi kubwa ya vyombo vya habari, kama kungelikuwa hakuna uhuru wa habari, nafikiri kusingelikuwa na idadi kama hiyo,” alieleza.
Hata hivyo, alisema uandishi wa habari ni taaluma kama zilivyo taaluma nyengine ambapo maadili na mipaka ya kazi inazingatia uhalisia wa kitaaluma.
“Sisi kama taasisi ya kihabari, tumekuwa tukisisitiza maadali ya taaluma, vyombo vya habari vinawajibika kwa asilimia kubwa juu ya hili,” alisema.
Alisema kuwepo kwa idadi hiyo ya vyombo vya habari kumeonesha jinsi China ilivyo mstari wa mbele katika kuwafikishia habari wananchi wake huku suala la kulinda silka, utamaduni na mila za nchi likipewa uzito unaostahili.
Wakati huo huo, ujumbe huo wa waandishi wa habari wa Zanzibar ulitembelea ofisi ya radio China Kimataifa (CRI), ambayo hurusha matangazo yake kupitia lugha 61 duniani, kikiwemo kiswahili.
No comments:
Post a Comment