Habari za Punde

Mufti wa Oman Aipongeza Ofisi ya Mufti Zanzibar kwa Kuwaunganisha Waislam.

Na Mwandishi wetu
MUFTI Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmad Al-Khaliyly, ameipongeza afisi ya Mufti wa Zanzibar kwa juhudi inazochukua kuwaunganisha Waislamu nchini.

Pongezi hizo alizotoa wakati alipozungumza na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi ofisini kwake Kiembesamaki mjini Zanzibar.

Aidha alisifu uhusiano mzuri uliopo kati ya afisi yake na afisi ya Mufti wa Zanzibar na kupongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa uhusiano huo.

Sheikh Al-Khaliyly amemualika Mufti wa Zanzibar kutembela Oman na kuahidi kuendeleza udugu wa kihistoria na kusema afisi yake ipo tayari kusaidia ndugu zao wa Zanzibar katika hali zote.

Akijibu hotuba hiyo, Mufti wa Zanzibar aliishukuru serikali ya Oman kwa misaada mingi inayotoa kwa Zanzibar ikiwemo jengo jipya la afisi ya Mufti wa Zanzibar lililofunguliwa mwaka 2009.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi Mdogo wa Oman aliepo Zanzibar, Sheikh Saleh Suleiman, Naibu Mufti, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, watendaji wa afisi ya Mufti na baadhi ya maofisa kutoka ubalozi wa Oman.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.