Na Mwandishi maalum, New York.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza kuwa ataliamrisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuongoza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na faru na ukataji haramu wa miti kwa shughuli za biashara ambao umefikia kiwango kikubwa Tanzania.Aidha, alisema sekta ya utalii nchini Tanzania sasa imeanza kutishiwa na uuaji wa wanyama hao na biashara haramu ya meno ya tembo na faru, na kuwa tishio hilo ni kubwa kwa sababu sekta ya utalii inachangia kiasi cha asilimia 17 katika mapato ya taifa na inaajiri kiasi cha watu 300,000.
Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo jioni juzi wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa nchi na serikali kuhusu biashara haramu ya wanyama na bidhaa zake pamoja na biashara haramu ya bidhaa za miti na mbao.
Aliuambia mkutano huo ulioandaliwa na Rais Ali Omar Bongo Ondimba wa Gabon na serikali ya Ujerumani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwa mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na tembo kiasi cha 350,000 lakini kutokana na ujangili idadi hiyo ya ilishuka hadi 110,000 ilipofika mwaka 2009.
Kuhusu faru, alisema mwaka 1974 walikuwepo 700 na sasa wako chini ya 100 kwa sababu ya vitendo vya kijangili.
“Katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa kilele cha ujangili katika mikonga ya wanyama, tulilazimika kutumia jeshi kutuliza hali hiyo. Tuliona matokea mazuri na tulikuwa na utulivu wa aina fulani. Lakini katika miaka minne iliyopita, tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwa ari na kasi mpya. Kwa mfano kati ya mwaka 2010 na Julai, 2013, zaidi ya tembo 1,386 waliuawa,” alisema.
“Tumechukua hatua kali za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na sera, sheria na kanuni za kupambana na ujangili. Aidha, tumetia saini mikataba mbali mbali ya kimataifa ya kupambana na ujangili huu,” alisema.
“Vile vile, tumechukua hatua za kukamata majangili na hata kukamata silaha zinazotumika katika ujangili. Kati ya mwaka 2010 hadi katikati ya mwaka huu, 2013, jumla ya majangili 5,189 wametiwa mbaroni na silaha kiasi cha 1,952 zimekamatwa. Isitoshe, vipande vya 3,788 vya meno ya tembo vimekamatwa vikiwa na uzito wa kilo 10,756 zilikamatwa nchini. Nimeamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kukabiliana na hali hiyo na naamini kuwa tutapata mafanikio makubwa zaidi katika operesheni inayoandaliwa,” aliongeza.
Hata hivyo, alisema bado shughuli za kupambana na ujangili, zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na mahitaji ya watumishi 4,800 wapya kwa ajili ya kupambana na ujangili.
“Pamoja na kwamba tuna matatizo ya watumishi, bado pia tuna matatizo ya raslimali fedha. Bajeti ya sasa ya dola za Marekani 6.9 milioni kwa ajili ya Idara ya wanyamapori haitoshi kutimiza yote haya. Tunahitaji dola za Marekani milioni 19.4 kwa ajili ya shughuli hiyo na nyongeza ya dola milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi. Tukiachiwa pekee yetu hatuna uwezo. Tunaomba twende pamoja katika hili,” alisema.
No comments:
Post a Comment