Habari za Punde

Kamati ya Baraza la Wawakilishi Kuaza Kazi Wiki Ijayo.

Na Himid Choko, BLW
KATIBU wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ndugu Yahya Khamis Hamadi amewahimiza Watendaji wa Mawizara na taasisi wanazoziongoza kutoa mashirikiano ya kutosha kwa Kamati za Kudumu za Baraza hilo zinazotarajiwa kuendelea tena na kazi zake za kawaida wiki ijayo.

Amesema Shughuli zote za umma zinafanywa kwa niaba na maslahi ya wananchi, na wananchi kupitia Wawakilishi wao kwenye Baraza la Wawakilishi wanahaki ya kujua namna halisi yab serikali yao inavyotenda haki hizo.

Amesema kwa mantiki hiyo watendaji hao wana jukumu la kutoa mashirikiano na taarifa sahihi juu ya mambo wanayoyashughulikia katika utumishi wote wa umma ili kuwawezesha wananchi kupitia wawakilishi wao kujua mambo yanayofanywa kwenye Mawizara ya serikali kwa maslahi yao.

“ Napenda kuwasisitiza tena watendaji wote wa Mawizara na Taasisi zao, kuzipa ushirikiano Kamati hizo kwa muda wote zitakapokua katika taasisi zao pamoja na kuzipatia taarifa sahihi kwa dhana ile ile ya kuendeleza uwazi na uwajibikaji’ Alisisitiza Katibu Yahya.

Amesema hiyo ndio dhana kubwa inayojenga wajibu wa Serikali na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusiana na haki za Kamati.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ndugu Yahya amesema Kamati hizo za Kudumu za Baraza la Wawakilishi zitaendelea na kazi zake za kawaida kuanzia Septemba 9 hadi Septemba 20, 2013.

Amesema pamoja na Kufuatilia Utendaji wa Kila Wizara na taasisi zake Kamati hizo pia zitapokea taarifa ya utekelezaji wa Maagizo yaliyotolewa na Baraza kupitia Ripoti za Kamati za Mwaka 2012/2013.

Amesema ingawa Kanuni ya 108 (15) inaweka masharti kwa kila Wizara kuwasilisha mbele ya Baraza , Ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza katika kila Mkutano wa mwezi wa Machi ya kila mwaka lakini pia Kamati zinawajibu wa kufuatilia zaidi utekelezaji wa maagizo hayo kwa kujiridhisha.

Amesema Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (PAC), Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo na Kamati ya Ujenzi na Mawasiliano zitafanyakazi zake Unguja.

Amezitaja Kamati nyengine zitakazofanyakazi Unguja kua ni Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii pamoja na Kamati ya Mifugo, Utalii , Uwezeshaji na Habari.

Ndugu Yahya amesema Kamati ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa itafanyakazi huko Dar es Salaam wakati Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itakwenda huko Pemba.

Himid choko- BLW 5 September 2013

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.