Na Mwantanga Ame
HATMA ya uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki, baada ya Mwakilishi wake Mansour Yussuf Himid, kufukuzwa uanachama bado ni kitendawili baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kusema suala hilo litafahamika hadi Tume hiyo itakapoona haja ya kufanya hivyo.Ofisa Uhusiano wa Tume hiyo, Idrissa Haji Jecha, aliyasema hayo jana wakati akizunguimza na Zanzibar leo mjini Zanzibar.
Jecha alisema, ili uchaguzi mdogo ufanyike kunahitajika baadhi ya mambo kwa kupitia ngazi maalum za kisheria zinazosimamia uchaguzi.
Alisema jambo la awali linalohitajika kufanyika ni kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, kuiarifu rasmi Tume hiyo kama kuna nafasi ya mjumbe iliyowazi na inahitaji kujazwa.
Alisema baada ya hatua hiyo Tume ya Uchaguzi, ndipo itapokaa na kuangalia kama itangaze kuwapo kwa uchaguzi huku ikiangalia namna ya kuweza kupata gharama za kufanyia kazi hiyo.
Alisema ni vigumu kusema kama kuna uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo mdogo kwani bado yapo mambo yanahitaji kufanyika kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo.
“Tume ikishaarifiwa ina haki ya kukaa na kupima kama uchaguzi huo ufanyike ama usifanyike kwa kuangalia na muda inalazimika kupima hilo”, alisema Jecha.
Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar inaelekeza uchaguzi mdogo utafanyika baada ya mienzi mitatu pindipo nafasi hiyo itapotangazwa kuwa wazi.
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika 2015 jambo ambalo bado halijawekwa wazi kama uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki kama utaweza kufanyika kutokana na kubakiza kipindi cha mwaka mmoja na zaidi ya mienzi mitano.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, amekishangaa Chama cha CUF, kuingilia maamuzi ya Chama cha CCM, iliyoyachukua dhidi ya kumfukuza uanachama Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mansour Yussuf Himid.
Pinda alihoji hilo katika kipindi cha masuala ya papo kwa papo, baada ya Mbunge mmoja kutoka CUF, Haji kuhoji ni kwanini Chama cha CCM kiliamua kumfukuza Mansour, wakati alikuwa akitoa maoni yake ya kutaka mfumo wa muungano wa mkataba.
Akijibu suala hilo, Pinda alisema anashangazwa kuona wanachama wa CUF, kupingana na hatua hiyo wakati kuna kumbukumbu za chama hicho kuamua kumfukuza Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid ambaye hadi sasa ameendelea kuwa mbunge.
Alisema haoni haja ya vyama vyengine kushangalia maamuzi hayo, wakati kilichofanyika ni mambo ya ndani ya chama chao na haoni sababu ya kwa nini waanze kutoa hoja zinazoendana kinyume na maamuzi hayo.
Nae, Mbunge wa Kikwajuni, Hamad Yussuf Masauni, aliliomba Bunge kuelekeza kanuni kwa mbunge huyo kutokana na kudai sababu ya kufukuzwa kwa Mansour kudai suala hilo lilifanyika kutokana kuelezea msimamo wa kutaka mfumo wa serikali ya mkataba.
Masauni alisema anashangaa kuona Mbunge huyo kuelezea sababu za kufukuzwa kwake zilitokana na imani ya Mwakilishi huyo kuhubiri mfumo wa muungano wa mkataba wakati CCM ilielezea sababu nyengine jambo ambalo ni kulidanganya Bunge hilo.
Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge hilo Job Ndugai, aliwataka Wabunge hao, kuliacha suala hilo kwa vile lingeweza kuteka mjadala wa mswada wa sheria wa umwagiliaji maji.
No comments:
Post a Comment