Habari za Punde

Vyombo vya Habari Nguzo ya Maendeleo China.

Na Khamis Mohammed, BEIJING
KUWEPO kwa vyombo huru vya habari vyenye kuzingatia maslahi ya umma, kumetajwa kusaidia kuharakisha kuinua maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa katika taifa la China.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Shirika la Habari la China, Xinhua, Prof. Yan Wen Bin, alisema hayo wakati akiwasilisha mada juu ya wajibu wa vyombo vya habari katika kusaidia maendeleo ya nchi.

Prof. Bin alisema pamoja na wajibu wa vyombo vya habari katika kuburudisha, kuelimisha, kukosoa au kutetea, lakini pia vina wajibu wa kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na nafasi iliyonayo kwa taifa kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Alisema, iwapo vyombo vya habari vitashindwa kutumia dhima ya uwajibikaji kwa umma, maendeleo ya taifa yanaweza kukosa hamasa za wanajamii na taifa kujikuta likishindwa kupata maendeleo ya kweli katika kutoa huduma bora kwa wananchi wake sambamba na kupoteza muoenekano wake kwa mataifa mengine.

Alisema, vyombo vya habari nchini China mara zote vimekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu, ambapo asilimia kubwa ya wananchi wake wamekuwa wakipata fursa nyingi za kihabari kupitia magazeti, redio na televisheni.

Alisema, China pamoja na ukubwa wake kieneo imekuwa kama kijiji wakati huu wa maendeleo ya kisayansi na teknolojia, hivyo ni lazima jamii ya Wachina ielekezwe huko kwa msaada wa vyombo vya habari.

Alisema, programu za aina mbali mbali za kuelimisha jamii ya Wachina na dunia kwa ujumla zimekuwa zikitayarishwa kupitia televisheni ya taifa ya nchi hiyo (CCTV), hali ambayo imeweza kuwafikia wananchi wengi hata wale walioko vijijini.

“China ina magazeti 1943 ambapo magazeti 816 ni ya kila siku, ni fursa kubwa kwa wananchi katika kupata habari”, alisema Prof. Bin.

Aidha, mbali na wingi wa magazeti, China ina idadi kubwa ya vituo vya televisheni vipatavyo 360 vikiwa na chaneli zaidi ya 2000 ambazo huangaliwa na watu zaidi ya milioni 900.

Akuzungumzia rushwa kwa vyombo vya habari, Prof. Bin alisema, China imekuwa ikipambana na aina zote za rushwa na kwamba serikali ipo makini mno katika vita hivyo.

“Wapo watu wameshahukumiwa mpaka adhabu ya kifo kwa kujishughulisha na rushwa na wengine kutumikia vifungo vya muda mrefu, hii yote ni kuonesha jinsi serikali inavyokerwa na rushwa”, alisema.

Alisema, vyombo vya habari vimekuwa vikifichua aina tafauti ya vitendo vya rushwa na kuitaja kashfa ya maziwa yaliokuwa na sumu mwaka 2008, kwamba ilifichuliwa na vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.