Na Kadama Malunde, Shinyanga
KATIKA harakati za kuokoa maisha ya mama na mtoto Tanzania, Shirika la utafiti la Afya Barani (AMREF) linatarajia kutoa mafunzo ya awali ya afya kwa wakunga elfu moja hadi kufikia mwaka 2015.Lengo la mpango huo ni kuleta mabadiliko na kupambana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo wakunga.
Ofisa mradi wa Tubadilike kutoka AMREF mkoa wa Shinyanga, Zahara Swalehe aliyasema katika tamasha kuhusu afya ya uzazi kwa vijana lililofanyika katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga.
Tamasha hili liliwakutanisha wanafunzi wa skuli tisa za sekondari kutoka wilaya nne za mkoa Shinyanga.
Ofisa mradi alisema mpaka sasa shirika la AMREF limeshatoa elimu ya afya kwa wakunga kumi mkoani Shinyanga na mwaka huu linatarajia kutoa elimu hiyo kwa wakunga 70 kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Simiyu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto hasa kwa wananchi wanaoishi mbali na huduma hizo za afya.
Alisema kwa mujibu wa utafiti walioufanya wamegundua kuwa akina mama hususani waishio vijijini wamekuwa wakipoteza maisha pamoja na watoto wao kutokana na huduma za afya kuwa mbali na maeneo wanayoishi
Aidha alifafanua kuwa ukosefu wa elimu ya uzazi na ukosefu wa wataalamu ni miongoni kwa sababud zinazochangia kutokea vifo hivyo.
''AMREF linafanya utafiti wa kiafya katika maeneo mengi barani, tunatoa elimu ya afya ya uzazi kwa wakunga mkoani Shinyanga ili kuondokana na vifo vya mama na mtoto sababu ya ukosefu wa huduma za afya", alisema.
Katika hatua nyingine aliwataka wanafunzi kuacha kujihusisha na masuala ya ngono wakiwa katika umri mdogo hali ambayo inaweza kuwasababishia kuharibu mfumo wa uzazi kwani viungo vyao bado havijakomaa. Pia aliwaasa wanaotumia dawa za kulevya kuacha mara moja kwani madhara yake ni makubwa.
Naye Katibu tawala wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi, aliwataka wazazi na walezi mjini humo kuacha kuendekeza mila na tamaduni za kisukuma za kuozesha watoto wao wakiwa katika umri mdogo ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia huduma za afya za kienyeji kwani hali hiyo inahatarisha maisha ya mama na mtoto.
Wanafunzi walioshiriki katika tamasha hilo walilishukuru shirika la AMREF kwa kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vifo vya mama na mtoto hasa vijijini.
Aidha alitoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa AMREF kwa kutembelea maeneo ya vijijini kuona hali halisi ya maisha ya wanawake kwani Tanzania bila vifo vya akinamama na watoto inawezekana
No comments:
Post a Comment