Habari za Punde

Wanafunzi Wanusurika na MotoFuoni.

Na Haroub Hussein
TAHARUKI iliwakumba wanafunzi , walimu na wakaazi wa karibu skuli ya Raudha Academy ya Fuoni Ijitimai baada ya dahalia namba moja ya skuli hiyo kuungua moto.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa tatu na robo jana asubuhi wakati wanafunzi wa skuli hiyo wakiwa wanaendelea na masomo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Bilal Badrudin Khamis alisema katika tukio hilo hakuna mtu aliejeruhiwa kwa vile wanafunzi walikua nje ya dahalia hiyo wakati moto ulipoanza kuwaka.

Aidha alisema moto huo uliathiri dahalia namba moja inayotumiwa na wanafunzi wapatao 20 wa darasa la kwanza mpaka la tano pamoja na nyumba mbili za walimu na kuongeza kuwa dahalia nyengine hazikuathirika na moto huo. Alisema hadi sasa wanakisia kuwa hasara iliyopatikana inafikia shilingi milioni 30.

Nao majirani walioshughudia tukio hilo walisema walianza kuona moshi katika paa la dahalia hiyo na ndipo walipoanza juhudu za kuuzima huku wakiwasiliana na kikosi cha Zimamoto na Uokozi ambapo walifika na kufanikiwa kuuzima moto huo.

Walisema inawezekana chanzo cha moto huo ikawa hitiliafu ya umeme iliyotokea katika dahalia hiyo wakati wanafunzi wakiwa wapo madarasani.

Walisema ni vyema Kikosi cha zimamoto na uokozi kikatoa mafunzo maalum kwa wananchi juu ya kuwa na ujasiri wa kutumia vifaa vya kuzimia moto katika sehemu zao.

“ Ipo haja kwa kikosi cha zimamoto kikatoa mafunzo ya ujasiri kwani katika dahalia kulikua na vifaa vya kuzimia moto lakini vilishindwa kutumiwa kutokana na woga wa watu waliokuwewepo, vingetumiwa athari ingekua sio kubwa kama vingeweza kutumika ipasavyo” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.