Na Salum Vuai, Maelezo
IMEELEZWA kuwa, utunzi wa mashairi ya aina mbalimbali katika lugha ya Kiswahili, ni fani inayohitaji kuendelezwa kitaalamu ili iendelee kuwa njia ya kuielimisha jamii katika mambo mema.Akifungua mafunzo kwa vijana wanaojishughulisha na utunzi wa mashairi nchini, Msaidizi Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Mmanga Mjengo Mjawiri, alisema kimsingi, watunzi ni wajuzi lakini wanahitaji mafunzo juu ya nadharia ya utunzi ili waweze kutunga kitaalamu.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na BAKIZA na kufanyika jana kwenye ukumbi wa Kamisheni ya Michezo na Utamaduni Mwanakwerekwe, Mmanga alisema utunzi ni kipaji, ambacho kikiambatana na taaluma kinazidi kuimarika.
"Naelewa nyinyi si watunzi wachanga lakini tumewaandalia mafunzo haya ili muweze kuinua zaidi vipaji vyenu kwa lengo la kukuwezesheni kutunga kwa uhakika", aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo.
Mmanga alieleza kuwa, BAKIZA imedhamiria kuendeleza lugha ya Kiswahili katika fani na nyanya mbalimbali, lakini ili hilo lifanyike kwa ufanisi, ni lazima kuwepo ushirikiano na wadau wa lugha hiyo.
Alifahamisha kuwa, ushairi ni utanzu wa kwanza na wa kale, ambao hauna mipaka kwani hata mtu aliyekosa bahati ya kusoma skuli, anaweza kutunga mashairi.
Hata hivyo, alisema watu kama hao, ni lazima waendelewe ili utunzi wao ufuate kanuni za ushairi, kwani fani hiyo ni ya jadi na BAKIZA haitaki kuiona inapotea.
Aidha, alisema utunzi wa mashairi ni kazi ya wito ambayo mtu hatarajii malipo duniani, bali kama utunzi wake utalenga kusaidia jamii na kuiongoza katika maadili na ustaarabu, mshairi anaweza kupata tija mbele ya Mwenyezi Mungu.
Pamoja na kwamba kazi ya mashairi ni kuburudisha, lakini aliwataka washairi kuhakikisha pia tungo zao zinalenga kuielimisha jamii na kuiasa kufanya mambo mema kwao na kwa taifa lao.
"Tumieni fani hii kuishauri jamii iachane na maovu, ufisadi na hujuma za aina mbalimbali, na mkifanya hivyo, historia itakukumbukeni", alisisitiza Mmanga ambaye pia ni Mhadhiri wa lugha ya Kiswahili katika Chuo Kuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
Kwa upande mwengine alitaka jamii kujenga utamaduni wa kusoma vitabu, ili kujiongezea maarifa na kunufaika na maudhui yanayopatikana katika utunzi wa mashairi na riwaya.
Aidha, aliwashauri watunzi hao kuwa na tabia ya kusoma tungo za washairi wenzao wakongwe na chipukizi, ili aweze kujifunza zaidi na kutanua ufahamu na weledi wao.
Akitoa mada juu ya uandishi wa ushairi kwa jumla, Katibu wa Chama cha Kuendeleza Washairi Zanzibar (CHAKUWAZA), Said Suleiman Ali, alisema watunzi hawana budi kufuata kanuni na miadili ya utunzi ili tungo zao ziwe na kiwango na hadhi inayostahili.
Alisema ili tungo zifikie lengo, ni lazima zizingatie mambo matatu muhimu ambayo ni urari, muwala na utoshelezi, ambapo vina na mizani ni mambo ya msingi.
Naye Maalim Ali Mwalimu Rashid, mhadhiri wa SUZA, katika mada yake ya uandishi kwa jumla, alisistiza kuwa, mtunzi anapaswa kuwa na mambo manne, ambayo ni nia/dhamira, akili ya kutunga, muda na vifaa.
Nao washiriki wa mafunzo hayo, pamoja na kuishukuru BAKIZA, pia wameitaka kuangalia uwezekano wa kufanya kazi kwa karibu na wadau wa lugha ya Kiswahili ikiwemo CHAKUWAZA na wengine, ili kuiendeleza lugha hiyo.
No comments:
Post a Comment