Habari za Punde

WanaCCm watakiwa kujidhatiti kuweza kutekelezea majukumu ya chama

Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein  amewataka viongozi, wanachama, waasisi na  wapenzi wa chama hicho kujidhatiti zaidi kukiimairsha ili kiweze kutekeleza majukumu yake likiwemo la kushinda chaguzi zinazokuja.

Dk Shein ametoa kauli hiyo jana usiku wakati wa hafla ya kuchangia Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Unguja iliyofanyika huko katika hoteli ya Karafuu Wilaya ya Kati Mkoa Kusini.

Amewaambia viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho pamoja na wageni waalikwa kuwa hivi sasa chama hicho kinatekeleza mradi wa kuimarisha chama ambao umejikita katika kuimarisha majengo ya chama pamoja na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao hivyo suala la kukichangia ni jambo la msingi.

“Tunakabiliwa na mambo mawili muhimu kuimarisha majengo ya chama chetu na kujiandaa na uchaguzi unaokuja ”alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa wakati umewadia kufanya maandalizi ya uchaguzi huo.

Kwa hiyo ametoa wito kwa Ofisi za chama kubuni na kutekeleza mipango endelevu ya kukipatia chama mapato ya uhakika ili kitekeleze majukumu yake ipasavyo kwa ufanisi mkubwa na weledi.

“Lazima tujiandae mapema na katika hali ya sasa CCM inahitaji kuwa na miradi endelevu,makini na yenye mwelekeo mzuri ili chama kiwe imara zaidi” alisisitiza Dk. Shein.


Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na wana CCM na wageni mbali mbali kutoka Zanzibar na Tanzania Bara jumla ya shilingi milioni 163 zilichangwa; kati ya fedha hizo shilingi milioni 28 zikiwa fedha taslim na ahadi ni shilingi 135.   Dk. Shein alichangia shilingi milioni 10.

Amewataka wanachama na wapenzi wa CCM kukaza kamba kuhakikisha kuwa kasi ya vuguvugu la kukiimarisha chama hicho aliyoianzisha mwezi Aprili mwaka huu inazidi kupanda hadi uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2015  na kuwatanabahisha kuwa “kujidhatiti zaidi na kujiimarisha zaidi ni kupata mafanikio zaidi”

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM ameupongeza uongozi wa chama hicho Mkoa Kusini Unguja kwa maandalizi mazuri ya hafla hiyo ambayo yamewezesha chama hicho kuchangiwa kiasi hicho cha fedha.    

“michango hii imewezekana kwa kuwa sisi viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM azma yetu ni moja, lengo letu ni moja na shabaha yetu ni moja ambayo ni kukiwezesha chama chetu kiweze kutekeleza majukumu yake” Dk. Shein alieleza.

Alieleza kuwa mafanikio ya michango katika hafla hiyo imedhihirisha uwezo wa Chama cha Mapinduzi na dhamira yake ya kujiimarisha  ili kuendelea kuwa chama bora  na kushinda uchaguzi.

Aliwakumbusha wanachama na wapenzi wa chama hicho kuwa wao kuchangia chama chao  si kitu kigeni katika ulimwengu wa siasa za ushindani na imekuwa ikifanyika hivyo kote ulimwenguni.

“Ndivyo inavyofanyika ulimwenguni kote. Wanachama na wapenzi kwa ridhaa yao huchangia vyama vyao kwa mujibu wa uwezo wao. Wenye uwezo mkubwa wanatoa kikubwa na wenye uwezo mdogo wanatoa kidogo”alifafanua na kutoa mfano katika hafla hiyo ambapo wachangiaji walitoa kwa mujibu wa uwezo wao.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM kwa michango yao waliyoitoa wakati wa hafla hiyo na mengine wanayoitoa kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi.

Hafla hiyo ilipambwa na burudani maridhawa kutoka kikundi cha taarab cha Culture ambacho kilikonga nyoyo za washiriki kwa burudani safi ya nyimbo zao zamani na za sasa. Mgeni Rasmi alikitunuku kikundi hicho shilingi milioni mbili kama motisha kwa tumbuizo lao la muziki wa taarab asilia jioni hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa Ramadhani Abdalla mbali ya kumshukuru mgeni rasmi pamoja na wageni waliohudhuria aliahidi kuwa michango hiyo itatumika kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa na chama hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.