Na Salim Said Salim
TUME ya Uchaguzi  Zanzibar (ZEC) imeelezea kwa masikitiko makubwa juu ya kile ilichokiona kuwa ni  mwamko mdogo wa watu kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
  Kauli hii ya ZEC  inatokana na watu wachache kujitokeza kufanya hivyo katika mchakato  uliomalizika hivi karibuni wa kuwaandikisha wapiga kura wapya katika daftari  hilo.
Kwa mujibu wa  mwenyekiti mpya wa ZEC, Jecha Salum Jecha, waliojitokeza ni watu 30,999, sawa  na asilimia 22.7 tu kati ya 136,697, waliokisiwa.
Kauli ya ZEC  inashangaza na kukwepa ukweli. Hali hii ni kielelezo cha watu kukosa imani na  namna ambavyo chaguzi zimekuwa zikiendeshwa Zanzibar.
Kwanza ni wazi  kwamba kupiga kura Zanzibar bado sio haki ya raia, bali ni kama kupewa zawadi  na ZEC inayoamua nani apewe haki hiyo na nani anyimwe.
Kwa maana nyingine  kuwa Mzanzibari na kuwa na sifa za kuandikishwa kupiga kura haitoshelezi kupewa  haki ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Hadi sasa uamuzi wa  nani apige kura ni wa sheha ambaye huangalia zaidi kama huyo anayetaka  kujiandikisha ni ‘mwenzetu au sio mwenzetu’.
Uhuni ambao baadhi  ya hawa masheha wameufanya katika chaguzi zilizopita unaweza kuandikiwa kitabu  cha kuchekesha na kusikitisha. Hii inatokana na baadhi yao kuwanyima haki ya  kupiga kura watoto, ndugu na majirani zao.
Bila aibu hawa  masheha wamedai kutowajua watu hawa, wakiwemo wale ambao ni baba zao. Lakini  kwa vile huo ni mpango maalumu hapana hata sheha mmoja aiyefunguliwa mashitaka  ya kusema uongo na kutenda kosa la jinai la kumnyima raia haki ya kupiga kura.
Mara nyingi  tumesikia kwamba kipengele cha kutaka mtu kuwa mkazi wa eneo kwa muda wa miaka  mitatu (zamani miaka mitano) katika eneo moja kimesababisha maelfu ya watu  kunyimwa haki ya kupiga kura.
Hapa nataka kwa  mara nyingine kuweka wazi kwamba kama sheria za Zanzibar ni za kidemokrasia na  zenye utawala bora, basi huyo mtu angalau apewe haki ya kupiga kura kwa  uchaguzi wa rais.
Hii ni kwa sababu  visiwa vya Unguja na Pemba ni jimbo moja kwa uchaguzi wa rais wa Zanzibar na  eneo lolote lile la Tanzania ni jimbo moja la uchaguzi wa rais wa Muungano. Kwa  hivyo mtu awe anaishi popote pale (hata baharini au juu ya mti), madhali ni  Mzanzibari basi awe na haki ya kuchagua rais wa Zanzibar na wa Muungano.
Lakini watu hawa  wamekuwa watazamaji tu wa chaguzi na wapo waliotishiwa kufunguliwa mashitaka  kwa sababu tu wametaka kujiandikisha kupiga kura.
Usiri juu ya namna  kura zilivyopigwa bado una shaka, maana wapo waliofukuzwa kazi serikalini kwa  sababu hawakupigia kura chama cha CCM. Hata Rais mstaafu, Komandoo Salmin  Amour, bila ya aibu alisema wazi kuwa hakuona sababu ya kuwapa kazi serikalini  watu ambao hawakumpigia kura.
Waziri wa zamani wa  Elimu wa Zanzibar, Omar Ramadhani Mapuri, hawezi kusahaulika kwa kuwafukuza  shule zaidi ya wanafunzi 100 wenye asili ya Pemba waliotaka haki yao ya  kujiandikisha kupiga kura kwa vile walitimiza umri wa miaka 18. Hadi hii leo  Mapuri hajawaomba radhi vijana wale na Wazanzibari kwa uamuzi wake ule  uliokwenda kinyume na sheria na kuathiri maisha yao na familia zao.
Mapuri  anapokumbushwa uchafu huu huruka na kuwataka watu wasitoneshe vidonda wakati  yeye ndiye aliyevisababisha.
Kama Tume ya  Uchaguzi ilikuwa inafanya shughuli zake kwa uwazi basi ingekuwa na ubavu wa  kusema watu wangapi walinyimwa kujiandikisha katika zoezi hilo. Hii itatoa sura  ya jinsi hali ya uandikishaji ilivyo hivi sasa.
Unapowauliza  Wazanzibari wengi  juu ya mtizamo wao kwa  ZEC jawabu unalopata kutoka kwao ni kwamba hiyo ni tume ya kuwachuja wapiga  kura na sio kuwapa watu haki ya kupiga kura. Hii ni kusema watu wengi bado  hawana imani na namna ZEC inavyoendesha shughuli zake.
Kwa miaka nenda rudi masheha wamekuwa kikwazo  kikubwa katika kuifanya demokrasia ichanue na kustawi Zanzibar na licha ya  mapendekezo kadhaa ya kuwadhibiti watu hawa serikali inajifanya haisikii na  ndio kwanza inawaongezea madaraka.
Ukichunguza sifa za  watu hawa kuchaguliwa kuwa masheha, utagundua manyago mengi. Miongoni mwao ni  misimamo yao ya kisiasa sio taaluma na uwezo kazi.
Wapo walioamua  kuwatendea haki raia na kukataa kujiingiza katika kapu la kuonea na kudhulumu  watu. Matokeo yake ni kufukuzwa kazi, kuadhiriwa na kuakashifiwa kwa vile  wameonekana “sio wenzetu”.
Kwa tafsiri ya  wakubwa waliopo madarakani “wenzetu” ni watu ambao wanawanyima wenzao haki  ikiwa pamoja na ile ya kupiga kura.
Jingine ambalo lina  dosari katika utoaji haki Zanzibar ni utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari.  Idara ya Vitambulisho imefanya marekebisho makubwa kutaka kuhakikisha kila  mwenye haki ya kupata kitambulisho anapewa haki hiyo na imekuwa haina vikwazo  kusikiliza malalamiko ya wananchi.
Lakini hao masheha  hawasikii la muadhini wala mteka maji msikitini. Wapo ambao badala ya kujenga  mashirikiano na wananchi katika sehemu zao wamejijengea uhasama usiokuwa na  faida.
Njia pekee  itayovutia watu kuwa na imani na ZEC na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha  kupiga kura ni kuhakikisha kwamba kura sio zawadi, bali ni haki ya kila  Mzanzibari.
Siku hizi watu  waliopo nje ya nchi zao wanayo haki ya kupiga kura, lakini kwa Zanzibar hata  mtu ambaye hajawahi kuvuka bahari na kwenda nje ya visiwa vya Unguja na Pemba  hana haki hiyo.
Huu ndio ukweli na  wapo wanaonuna ukiwekwa hadharani. Kama hawataki maovu wanayoyafanya yaelezwe  hadhari basi wasiyatende.
Vile vile wale  wote, hasa masheha na akina fulani (wenyewe wanawajua) wanaowanyima watu haki  yao ya kupiga kura katika chaguzi za nchi yao wachukuliwe hatua za kisheria.
Kumnyima mtu haki  ya kupiga kura ni kosa kubwa la uvunjaji wa haki za binadamu, na kama kweli  tunaheshimu basi sheria za kuwadhibiti na kuwatia adabu wanaozivunja zionekane  zinachukuliwa.
Tuache porojo za  kujigamba kwamba tuna utawala bora na wa kidemokrasi wakati tunacheza ngoma ya  kudanganyana.
Tuwe wakweli au  tutajikuta historia inatuumbua na kutuhukumu siku za mbele kwa maovu  tunayoyatenda hii leo. Tujifunze haraka na tena kwa uadilifu kwa tunayoyaona na  kuyasikia  yanayowakuta wengine katika  nchi za nje ambao walitumia vibaya madaraka yao kuonea wananchi wengine.
Waswahili wanasema ‘mambo kangaja…huenda  yakaja’ na wakitaka wasitake hayo mabadiliko yanakuja na njia pekee ya salama  ni kuyapokea, tena kwa heshima na adabu na sio kwa shingo upande na nongwa.
Zama za kuonea watu  kwa wapi wanatoka, udhaifu wao au misimamo yao ya kisiasa zimepitwa na wakati  na hazirudi. Kwa ufupi zama hizo zimeshakwenda arijojo.
Ni vizuri sote  tukabadilika kabla ya wakati haujatulazimisha kubadilika na hatimaye kuona aibu  kwa tunayoyatenda hivi sasa.
Chanzo - Tanzania Daima
 

 
.jpeg) 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Namshanga, muandishi, ana ilaumu tume, bure, ana wasahau, cuf, ni chanzo, kikuu cha, watu kukosa haki zao, iliamuliwa, siku za uwandiki shaji kusiwe na mawakala, wa vyama, hawa, ndio, wanao sababisha vurugu, wabaki, watendaji wa serekali, tume na masheha, tume wao, hawajui, huyu au yule mkazi halali, isipokuwa shehe, sasa kuweka mawakala, kuna changia, fitna,sasa tunalumu tume bure,kwa uzembe wa,cuf, muamsho
ReplyDeletenampongeza mwandishi kwa kuwa mkweli , sema ukweli hata kama utakudhuru , Mtukufu Mola hawapendi wenye kudhulumu , lakini hapa kwetu ni kawaida , na ijumaa mstari wa mbele sijida kama muhuri usoni, kuhiji mbio mbio , kufuturisha sikwambii kebekebe lakini dhuluma wameweka mbele, hongera tena mwandishi kwa ukweli
ReplyDeleteHawa ZEC hawana maana kabisa! wameshindwa kusimamia chaguzi laikni siku moja watakuja kulipa gharama !
ReplyDelete