Na Mwandishi wetu, Mbeya
VURUGU kubwa zimeibuka jana mkoani Mbeya baada ya wafanyabiashara kupambana na polisi kufuatia kugoma kununua mashine za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinazouzwa kwa shilingi 800,000.Mapema asubuhi makundi ya wafanyabiashara yalipita duga moja baada ya jengine kuhamasisha wenzao kufunga maduka na kushiriki katika maandamano kupinga mashine hizo, huku wakitishia kuwashambulia wale wanaokaidi.
Baada ya polisi kupata taarifa walifika katika eneo la tukio na kuanza kuwatawanya vijana hao, lakini waliamua kukimbilia barabarani.
Wafanyabiashara hao walifunga barabara kwa mawe na mgogo ya miti na kuchoma matairi moto huku wakiwarushia mawe polisi.
Hali hiyo ilisababisha polisi kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa na hasira.
Mapambano hayo yalidumu hadi mchana jana huku baadhi ya wafanyabiashara wakitiwa mbaroni.
Kabla, polisi walitumia vipaza sauti kuwataka wafanyabiashara kutawanyika lakini walikaidi amri hiyo.
Maandamano hayo yaliathiri huduma za usafiri na chakula mjini humo.
Wafanyabiashara hao wanapinga mashine hizo zinazouzwa kwa bei ya juu.
Baadae serikali ilikutana na wafanyabiashara hao kujaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani amesema watu 70 wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na vurugu hizo.

No comments:
Post a Comment