Habari za Punde

Maalim Seif Amtembelea Dkt. Sengondo Mvungi.

Dk. Mugisha Clement Mazoko (kulia) akizungumza na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif, alipomtembelea Dk. Sengondo Mvungi,katika hospitali ya Taifa Muimbili kumjulia haliyake baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana hivi karibuni.kulia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia. (Picha na Salmin Said OMKR).  
Na Khamis Haji OMKR  
Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi ambaye amejeruhiwa vibaya na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi imeamuliwa akapatiwe matibabu zaidi nchini Afrika Kusini.
Kiongozi wa madaktari wanaomtibu Dk. Mvungi, Mugisha Clement Mazoko ameeleza hayo leo alipokuwa akimpa taarifa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alifika hospitali na Muhimbili kujua maendeleo ya matibabu ya Mjumbe huyo.
Dk. Mugisha amesema afya ya Dk. Mvungi aliyekuwa akipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi hadi jana Alasiri inaendelea vizuri.
Hata hivyo, alisema Serikali imeamua kumsafirisha kwenda nchini Afrika Kusini ili kupata matibabu zaidi.
“Serikali imeamua kumsafirisha kwenda kupatiwa matibabu zaidi Afrika Kusini na anatarajiwa kuondolewa wakati wowote kuanzia sasa”, alisema Dk. Mugisha majira ya saa 11: 15 jioni.
Habari zaidi zilizopatikana zimeeleza kuwa, Dk. Mvungi alitarajiwa kusafirishwa majira ya saa 12 jioni kwenda kupatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
Dk. Mvungi alijeruhiwa vibaya na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huko nyumbani kwake jijini Dar es Salaam juzi.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.