Habari za Punde

DK.SHEIN:AAGIZA TATIZO LA MAJI MAKUNDUCHI LIMALIZWE HARAKA

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                    18 Disemba, 2013
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtaka Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha kuhakikisha kuwa tangi la maji la Makunduchi linajengwa ndani ya kipindi cha miezi sita ili kumaliza tatizo la maji linaloukabili mji huo na maeneo mengine yanayouzunguka.

Dk. Shein alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha afya cha Kajengwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja ambapo pamoja na mambo mengine wananchi wa Kajengwa walieleza tatizo la ukosefu wa maji katika eneo hilo linavyoathiri shughuli zao.
Alisisitiza kuwa kama tatizo ni fedha basi Wizara hizo zikae na kuangalia mafungu ya kutoa fedha hizo ili tangi hilo la chuma liweze kujengwa bila ya kuchelewa na kuwaondoshea wananchi kadhia ya kukosa huduma ya maji.
Dk. Shein alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mwalimu Haroun Ali Suleiman kwa kukiwezesha kituo cha afya Kajengwa kupata maji kwa kuchimba kisima kwa thamani ya shilingi milioni tano.
Aliwataka wananchi wa Kajengwa kuwa na subira wakati Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha huduma ya maji hatua ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na washirika mbalimbali wa maendeleo na kutolea mfano msaada wa visima 50 kutoka Serikali ya Ras Al Khaimah.

Hata hivyo aliwaeleza kuwa kwa kuwa baadhi ya maombi likiwemo la maji walishamueleza katika ziara zake za nyuma na kwamba aliyatolea maelekezo ya utekelezaji aliwataka wasikilize maelezo kutoka kwa viongozi wa taasisi husika.
Kwa hiyo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati pamoja na watendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar-ZAWA na Shirika la Umeme Zanzibar –ZECO kutoa maelezo kuhusu tatizo hilo.
Akitoa maelezo katika mkutano huo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mheshimiwa Ramadhani Abdalla Shaaban alieleza kuwa Serikali imo katika kutekeleza mpango wake wa kuongeza huduma za maji Unguja na Pemba na matarajio ni kuwa ifikapo mwezi Septemba, 2014 tatizo hilo litakuwa limekwisha.
Alifafanua kuwa katika eneo la Kajengwa Makunduchi huko nyuma tatizo lilikuwa pampu ya kusukuma maji lakini baada ya kupatikana pampu hivi sasa kisima nacho hakina uwezo wa kutoa maji ya kutosheleza mahitaji ya wakazi wa kijiji hicho.
Alieleza kuwa sambamba na kisima kutotoa maji ya kutosha lakini pia ongezeko la haraka la matumizi ya umeme kwa wananchi wa eneo hilo limesababisha umeme kutotosheleza mahitaji hivyo kuathiri upatikanaji maji kwa kuwa mashine haiwezi kufanyakazi wakati wote.
Akifafanua zaidi kuhusu tatizo hilo Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA Dk. Mustafa Ali Garu alisema tatizo la maji Kajengwa limeongezeka kufuatia kuharibika kwa tangi la maji lililoko Makunduchi Uwandani ambalo lilikuwa likisaidia kuleta maji kijijini hapo.
Alibainisha kuwa kijiji hicho kilikuwa kikipata maji kutoka kisima kilichopo kijijini hapo pamoja na kutoka tangi hilo la Makunduchi Uwandani hivyo kuharibika kwa tangi hilo kumeathiri huduma ya maji kijijini hapo.
Dk. Garu alisema hatua zinachukuliwa hivi sasa kwa kushirikiana na Wizara kujenga tangi jipya huko Makunduchi Uwandaji na litakapokamilika tatizo la maji katika sehemu nyingi ikiwemo Kajengwa litakuwa limemalizika.
Aliongeza kuwa kwa sasa katika eneo la Mkunduchi vimechimbwa visima vitatu ambavyo viko Mzuri, Makunduchi Uwandaji na Mtende.
Hata hivyo alipotakiwa kutoa maelezo kuhusu huduma ya umeme Meneja Uendeshaji wa ZECO ndugu Abdalla Haji Seti aliahidi kuwa Shirika lake, ndani ya mwezi mmoja, litakuwa limekamilisha uwekaji wa njia mpya ya umeme kwa ajili ya kuendesha mashine ya maji ya eneo hilo.
Uzinduzi wa kituo cha afya Kajengwa ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kusirikiana na wadau wengine wakiwemo Serikali ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari, 1964.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdulla Shaban, Waziri wa Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mwalimu Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Afya Bibi Sira Ubwa Mamboya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Jidawi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.