HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR , MHE. BALOZI SEIF A. IDDI KATIKA
UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA NNE WA BARAZA LA
WAWAKILISHI ZANZIBAR , TAREHE 20 DISEMBA, 2013
1.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uzima, afya njema na utulivu na pia kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu tuliyojipangia katika
Mkutano huu wa Kumi na Nne kwa salama na
amani. Pili, nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Wasaidizi wako wote
kwa umakini, busara na hekma zilizopelekea kuendesha Mkutano huu wa Baraza la
Wawakilishi kwa ufanisi mkubwa sana .
2.
Mheshimiwa Spika, vile vile napenda
niwashukuru Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Baraza kwa kuziongoza Kamati
zao na kutekeleza majukumu yao
vyema.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa
nimpongeze Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa
kuiongoza nchi yetu kwa umakini na kuweza kupata mafanikio makubwa. Ushauri na
miongozo yake kwetu inatusaidia sana
katika kutekeleza majukumu yetu, kwa manufaa ya nchi yetu na wananchi wote.
4.
Mheshimiwa Spika, aidha, nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe
wote wa Baraza lako Tukufu kwa majadiliano mazuri na ushauri wenye kujaa busara
na hekima wenye nia ya kuimarisha utendaji na utekelezaji wa majukumu yetu ya
kila siku. Pia, napenda kuwashukuru sana
Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi wa kina wa hoja mbali mbali
zilizoulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi kwenye mkutano huu.
5.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 5
Disemba, 2013 Bara letu la Afrika na ulimwengu kwa jumla ulipata msiba mkubwa
na usioweza kusahaulika wa kuondokewa na kiongozi shupavu, mvumilivu na mtetezi
wa haki za binaadamu wote na mkombozi wa wananchi wa Afrika ya Kusini, Mheshimiwa Mzee Nelson Mandela. Ni wazi
kwamba kiongozi huyu aliepigania uhuru katika nchi yake ya Afrika Kusini
hatosahaulika kwa kuionesha dunia utu wa hali ya juu kwa kuweza kusamehe na
kusahau yaliyopita na kuwataka wananchi wote wa Afrika Kusini kushirikiana bila
ya ubaguzi wa dini, rangi au ukabila.
Mzee Mandela hakuwa mtu wa kulipa kisasi kama
wengi wangeweza kufikiria. Mzee Mandela
ameutumia umri wake wote wa ujanani jela ambako amefungwa kwa muda wa miaka 27.
6.
Mheshimiwa Spika, bila shaka tuna mengi
ya kujifunza kutokana na maisha ya Mzee Nelson Mandela katika kujali utu,
kusamehe, uvumilivu na moyo wa kuipenda nchi na Bara letu na kuwa na mahusiano
mema na binaadamu wote katika dunia.
Mzee Mandela aliwasamehe waliomfanyia uovu huo, pamoja na kuamini kuwa
Mungu hakumuumba mtu muovu ila uovu ni wa mtu mwenyewe.
7.
Mheshimiwa
Spika, kama sote tunavyoelewa kwamba, kila
ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka, nchi yetu inaadhimisha sherehe za
Mapinduzi yetu Matukufu yaliyotokea mwaka 1964. Ifikapo tarehe 12 Januari, 2014
Mapinduzi hayo yatatimiza miaka 50.
8.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla
Maadhimisho haya yaliyozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
tarehe 15 Agosti, 2013 yanaendelea vizuri. Tangu yalipozinduliwa tumeshuhudia
wananchi wakisherehekea kwa kufanya usafi wa mazingira, kushiriki katika
matamasha mbali mbali ya michezo na burudani pamoja na uzinduzi, uwekaji wa mawe ya msingi na
ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo. Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa
Baraza lako Tukufu wazidi kuhamasisha wananchi kuendelea kushiriki kwa wingi
katika matukio mbali ya sherehe hizi pamoja na siku ya kilele hapo Uwanja wa
Amaan, tarehe 12 Januari, 2014.
Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote
waliopangiwa kuzindua au kuweka mawe ya msingi kwa miradi mbali mbali ya maendeleo
kwa kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi.
9.
Mheshimiwa Spika, katika kusherehekea
miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali imeandaa maonesho yatakayofanyika katika
viwanja vya Beit al Ras kwa siku nne kuanzia tarehe 2 Januari, 2014 hadi tarehe 5 Januari, 2014
ambapo Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi na Jumuia za Kiraia watapata fursa
ya kuonesha shughuli zao wanazozifanya, huduma wanazozitoa au bidhaa
wanazozalisha. Hii ni fursa ya pekee kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na wageni kutembelea kwenye maonesho
haya ili kuona mafanikio yetu ya miaka 50 tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya
Januari 12, 1964.
10. Mheshimiwa Spika, sote tunaelewa
kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Awamu ya Tatu (TASAF III) tayari umeshaanza
shughuli zake hapa Zanzibar
na imeshafanya shughuli nyingi zikiwemo kutoa mafunzo ili kujenga uelewa wa
lengo la TASAF Awamu ya Tatu kwa wadau mbali mbali tukiwemo Waheshimiwa
Wawakilishi wa Baraza lako tukufu. Aidha, kaya maskini tayari zimeanza
kutambuliwa kwa mashirikiano na wanajamii wenyewe. Kwa Unguja jumla ya kaya
maskini 2,500 zimetambuliwa na kwa Pemba hadi
sasa jumla ya kaya 4,000 zimeshatambuliwa. Kazi ya kuzitambua kaya maskini
inaendelea kwa Shehia zote za Unguja na Pemba .
Aidha, hatua ya kuzihakiki kaya zilizokwisha tambuliwa zimeanza na tunatarajia
kuanza kutoa malipo kwa kaya hizo ifikapo mwezi Januari, 2014. Nachukua nafasi
hii, kuwaomba Waheshimiwa Wawakilishi kuendelea kutoa ushirikiano katika zoezi
zima la kuzitambua na kuzihakiki kaya maskini ili malipo yaweze kufanyika kwa wale
wanaostahiki na si vyenginevyo.
11.
Mheshimiwa Spika, bado tumo katika kipindi
cha mvua za vuli na katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia kupatikana
kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na
athari zake kuikumba dunia, ni vyema kwa taasisi zote zinazohusika kufuatilia
mwenendo wa hali ya hewa na kutoa taarifa za mapema kwa wananchi hususan
wakulima na wavuvi na wanaosafiri kwa kutumia usafiri wa angani na baharini ili
kuchukua tahadhari na kupanga vyema shughuli zao.
12.
Mheshimiwa
Spika, Sekta za Kilimo na Maliasili bado zinaendelea kuwa ni
muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja
katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi
walio wengi vijijini na mijini. Kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hizi zilichangia asilimia 30.2 ya pato la Taifa
na inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70
ya wananchi wanategemea sekta hii kwa kuwapatia ajira na mapato.
13.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza
azma yake ya kuleta Mapinduzi ya kilimo nchini Wizara imeweza kufanikisha mambo yafuatayo:-
Serikali ya Awamu ya Saba
kwa kupitia na Wizara ya Kilimo na Maliasili itaendelea kulipa kipaumbele suala
la kuwapatia wakulima ruzuku kwenye nyenzo na pembejeo za kisasa (mbegu bora,
mbolea, dawa na huduma za matrekta) ili kuinua uzalishaji hasa kwa mazao ya
chakula ikiwemo mpunga na mboga mboga. Aidha, katika kipindi cha misimu ya
kilimo 2010 hadi 2013 kumekuwa na ongezeko maradufu la ununuzi na matumizi ya
pembejeo hizo kama ifuatavyo:-
Kwa mbegu bora, Serikali imeongeza pembejeo kutoka
tani 55 mwaka 2010 na idadi hiyo kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia tani
620 mwaka 2013, mbolea – TSP na Urea kutoka tani 130 mwaka 2010 hadi kufikia
tani 1,500 mwaka 2013 na dawa ya magugu kutoka lita 12,000 mwaka 2010 hadi
kufikia lita 30,000 mwaka huu.
Kwa upande wa matrekta Wizara ya Kilimo na Maliasili
inatarajia kuingiza nchini matreka 20 kutoka Suma JKT ya Tanzania Bara hivi
karibuni.
Mambo Yaliyojitokeza Barazani:
14.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla
ya maswali 57 ya msingi na maswali kadha ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa
Wajumbe na kupatiwa majibu na ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri.
Nawapongeza kwa dhati Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu
kwa kuuliza maswali hayo ambayo yalikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi.
Aidha, Waheshimiwa Wajumbe walijadili na kupitisha jumla ya
Miswada mitatu ambayo ni:-
a)
Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Baraza la Vijana la Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na
Hayo;
b)
Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Amri ya Barabara, Sura 134 na
Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo;
c)
Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Kukinga na Kusimamia
Maswala ya UKIMWI Zanzibar, Kulinda na Kuendeleza Haki za Watu Wanaoishi au
Walioathirika na Virusi vya UKIMWI na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
15.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Kwanza
uliowasilishwa kwenye Baraza lako Tukufu na kujadiliwa ni Mswada wa Sheria ya
Kuanzisha Baraza la Vijana la Zanzibar
na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Kuwasilishwa kwa mswada huu kunatokana
na kilio cha siku nyingi cha vijana wetu wa Zanzibar kutaka kuwa na chombo chao
kilichoanzishwa kisheria cha kuwaunganisha na kufuatilia masuala mbali mbali
yanayowahusu na ya maendeleo kwa nchi yetu.
16.
Mheshimiwa Spika, madhumuni makubwa ya
Mswada huu ni kuwakuza vijana wetu ili wawe wazalendo kwa Taifa lao kwa
kuwajenga ili wajitambue, wajiheshimu wao na waheshimu wengine na pia kuitambua
kwa kina jamii yao kisiasa na kiuchumi na pia kuuthamini utamaduni wa nchi yao.
Aidha, Mswada huu una lengo la kuwaweka pamoja vijana wetu na kuweza
kubadilishana mawazo ambayo yatawasaidia wao pamoja na kulisaidia Taifa letu
ili liendelee kusonga mbele. Taifa lenye nguvu kazi imara ambayo ni vijana
linapata maendeleo kwa kasi sana .
Hivyo, nasi hatuna budi kuwakuza vijana wetu kwenye mtazamo wa kizalendo na
kimaendeleo ili kuisaidia nchi yetu.
17.
Mheshimiwa Spika, Mswada mwengine
uliowasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Wajumbe ni Mswada wa Sheria ya
Kurekebisha Amri ya Barabara, Sura 134 na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mswada huu una lengo la kurekebisha Sheria ya Barabara Sura 134 ambapo vifungu
vingi vilivyomo kwenye sheria hii haviwezi kufanya kazi kwa wakati tulionao
kutokana na kuwa Sheria hii ni ya muda mrefu na baadhi ya vifungu haviendi
sambamba na mabadiliko yaliopo ya ufanyaji kazi.
18.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa mwisho
uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Kukinga na Kusimamia
Masuala ya UKIMWI Zanzibar, Kulinda na Kuendeleza Haki za Watu Wanaoishi au
Walioathirika na Virusi vya UKIMWI na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mswada huu una madhumuni ya kuweka mfumo wa kisheria wa kuzuia na kusimamia
masuala yote ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI hapa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha haki za
binaadamu kwa wale wote wanaoishi au walioathirika na virusi vya UKIMWI. Aidha,
kuwepo kwa Mswada huu kutasaidia sana
kuweka uratibu mzuri wa masuala yanayohusiana na UKIMWI na Virusi vya UKIMWI
kwa Taasisi na Jumuiya zote zinazojishughulisha na masuala haya. Pia,
Mheshimiwa Spika, Mswada huu umetoa wajibu wa kila mmoja wetu kuweza kujua hali
yake ya Virusi vya UKIMWI kwa kupima afya yake na vile vile kuweza kujilinda
yeye mwenyewe na kuwalinda wengine kutokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Mswada unasisitiza jamii kujiepusha na mila
na itikadi potofu pamoja na mazoea ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha
kuenea kwa Virusi vya UKIMWI. Ni busara sisi Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na
wananchi wote tukazingatia sana
elimu tunayopata inayohusiana na masuala yote ya UKIMWI ikiwemo masuala ya
kinga, maambukizi, huduma na mengineyo. Sote tunaelewa kwamba UKIMWI ni ugonjwa
hatari na matibabu yake hadi sasa hayajapatikana. Hivyo, ni bora zaidi
kujikinga. Tusidanganywe na watu
wanaojidai madaktari wa dawa asilia na wanaweza kulitibu gonjwa hili. Si kweli bado dawa ya aina yoyote
haijapatikana pamoja na utafiti wote unaofanyika kuipata dawa ya kuponyesha
ugonjwa huu.
19.
Mheshimiwa Spika, Baraza lako Tukufu pia
lilipata nafasi ya kujadili kwa kina Ripoti ya Kamati Teule ya Kushughulikia
Migogoro ya Ardhi ambayo Mwenyekiti wake alikuwa ni Mheshimiwa Ali Mzee Ali.
Nachukua nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati hii pamoja na Wajumbe wake
wote kwa kuifanya kazi hii na kuikamilisha na kuwasilisha ripoti yake.
Nilihakikishie Baraza lako Tukufu kuwa Serikali imeipokea ripoti hii na
itaifanyia kazi ipasavyo. Hata hivyo,
ripoti hii imekuja kinyume na matarajio ya wengi, pamoja na baadhi ya Wajumbe
wenyewe. Maeneo mengi yenye migogoro na
malalamiko yameachwa bila ya kuchunguzwa.
Muda ambao Kamati hii iliyochukua ilitegemewa ingekuja na ripoti nzuri
zaidi. Serikali itaendelea kushughulikia
ile migogoro ambayo haikuzingatiwa na Kamati hii na hatua muafaka kuchukuliwa.
20.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeyapokea
mapendekezo yote yaliomo ndani ya Ripoti ya Kamati na hasa lile linalohusu
wananchi kuelimishwa juu ya dhana nzima ya ardhi kuwa mali ya
Serikali. Tunakubaliana na pendekezo
hili kuwa ipo haja ya kufanya hivyo na Serikali itaendelea kuwaelimisha
wananchi ili waielewe vema dhana hiyo.
Nawaomba Waheshimiwa Wawakilishi washirikiane na Serikali katika kutoa
elimu hiyo kwa wananchi wao Majimboni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kulipokea
pendekezo hili, Serikali pia imeyapokea mapendekezo mengine yote na itayafanyia
kazi kadri itakavyoona inafaa.
21.
Mheshimiwa Spika, Pia Baraza lako
lilipokea hoja mbili za Wajumbe wa Baraza hili zilizowasilishwa na Mhe. Hamza
Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura na Mhe. Mgeni Hassan Juma,
Mwakilishi Viti Maalum. Hoja hizo ni:-
a)
Hoja ya Mjumbe ya Kuomba ridhaa ya Baraza kwa ajili ya Kuwasilisha
Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza; na
b)
Hoja ya Mjumbe ya kuliomba Baraza Kutoa Azimio dhidi ya vitendo
vya udhalilishaji wa watoto, Zanzibar .
22.
Mheshimiwa Spika, hoja zote hizo zilipokelewa
na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu.
23.
Mheshimiwa Spika, hoja inayohusu Azimio
dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto ilipata michango mingi kutoka kwa
Wajumbe wa Baraza lako, na kwa kweli ilistahili kupata michango hiyo kwani
suala la udhalilishaji wa watoto ni jambo baya na la kukera sana na linatia
aibu nchi. Na ndiyo maana Wajumbe
waliichangia hoja hii kwa uchungu sana .
Naviomba vyombo vya sheria vitende haki kwa kuwachukulia hatua kali wale wote
watakaothibitika kufanya vitendo hivyo, imetolewa hapa na Waheshimiwa Wajumbe,
mifano mingi mingine ni ya aibu na ya kutisha.
Hatuwezi kuvumilia kuwa na watu wa aina hiyo ndani ya jamii yetu. Napenda nimpongeze sana Mjumbe aliyetuletea hoja hiyo hapa
Barazani.
24.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena
nichukue nafasi hii kukupongeza tena wewe binafsi, wasaidizi wako pamoja na
watendaji wote wa Baraza kwa kuhakikisha kwamba shughuli za Baraza zilizopangwa
zote zinatekelezwa chini ya maelekezo na busara zako Mheshimiwa Spika.
25.
Mheshimiwa Spika, vile vile niwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe
wa Baraza hili kwa jinsi wanavyojadili hoja mbali mbali zinazowasilishwa kwenye
Baraza kwa umakini wa hali ya juu. Michango na hoja wanazoziibua zinatusaidia
kuweza kufanya kazi kwa upeo mkubwa.
26.
Mheshimiwa Spika, Mwisho kabisa
navishukuru vyombo mbali mbali vya habari, radio, television na magazeti kwa
kuwa nasi kwa kipindi chote cha Baraza hili.
Pia nawashukuru, wakalimani wa alama kwa kazi yao nzuri waliyoifanya ya kuwawezesha
wananchi wenye ulemavu wa kusikia kujua nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya
Baraza hili.
Pia, nawashukuru Wajumbe wote kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa
utulivu na umakini mkubwa kwa muda wote wa Baraza hili. Ninawatakia safari ya salama kurudi Majimboni
mwao kuwatumikia wananchi wao.
27.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo,
sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi tarehe 22
Januari, 2014 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment