Na Amina Omari,Tanga
WATU sita wamefariki dunia papo hapo na wengine 26 kujeruhiwa baada ya
daladala kuligonga lori la mizigo,
katika eneo la Kange barabara kuu itokayo
Tanga mjini kwenda Muheza.
Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Costantine
Massawe alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana na ilihusisha gari la
abiria lenye namba za usajili T909 ATV lililokuwa likiendeshwa na Gadiel
Elikaeli na lori la mizigo aina ya Volvo lenye namba za usajili T260 DYM.
Alisema chanzo cha ajali ni mwendo kasi baada ya dereva wa daladala
ambaye alifariki kutaka kulipita gari
jingine bila kuchukua tahadhari na kujikuta anajiingiza kwenye lori lililokuwa limeharibika.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Raymond Mapunga (28),Halima Shaka
(28),Marrya Chilongoi (37),Glory Kidenya (1),Femida John (38) na dereva wa basi
hilo Gadieli Elikaeli (44) wote wakazi wa Kange.
Hata hivyo, alisema majeruhi 21 walipelekwa hospitali ya rufaa ya
Bombo kwa matibabu zaidi huku majeruhi wanne wakitibiwa katika hospitali ya
wilaya na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Nae Muuguzi wa zamu katika
hospitali ya rufaa ya Bombo, Alice Mkande alisema walipokea majeruhi 21 kati
yao 6 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa ambapo majeruhi 17 wanaendelea na
matibabu.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Charles Kiluwa, alisema ajali hiyo
ingeweza kuepukika kama dereva wa daladala
angekuwa makini.
No comments:
Post a Comment