Na Juma Khamis
WAZIRI wa Nchi (OR), Kazi na Utumishi wa Umma, Mhe.Haroun Ali
Suleiman, ametoa changamoto kwa wasomi kuandika machapisho mbalimbali ya
kitaalamu, akisema haiwezekani msomi mwenye shahada ya uzamivu (PhD) kukaa
miaka mitano bila kuandika chochote.
Alisema kutokuandika ni kasoro kubwa na msomi wa aina hiyo atakuwa
haitendei haki taaluma yake.
Alikuwa akizungumza katika fainali ya mashindano ya mdahalo kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi, yaliyofanyika
kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Vuga.
Aidha alipongea wazo la kuandaa mashindano hayo, akisema yanawajengea
wanafunzi uwezo wa kujiamini na kuwa viongozi wa baadae.
Alisema serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na
maslahi ya watendaji wakiwemo walimu hatua kwa hatua.
Hata hivyo, aliwataka walimu kuwajibika na kufundisha kwa ari kujenga
ustawi bora wa jamii ya kizanzibari.
Alichangia shilingi 300,000 kwa mshindi wa kwanza na kiwango kama
hicho kwa mshindi wa pili pamoja na kuahidi kuchangia shilingi 2,000,000 wakati
mashindano hayo yatakapoandaliwa tena mwaka 2014.
Mapema Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Idris Ahmada Rai, alisema mdahalo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu unawafanya wanafunzi wajiamini
wanapozungumza mbele za watu, hivyo
unapaswa kuendelezwa.
Alivipongeza vyuo vikuu vyengine kwa kuunga mkono wazo la kuandaa
mdahalo huo na kushiriki katika hatua zote.
Mdahalo huo ulivishirikisha vyuo vya SUZA, Chuo Kikuu cha Zanzibar
(ZU) Tunguu, Chuo cha Uongozi wa Fedha (ZIFA) na Chuo Kikuu cha Elimu Kishiriki
Chukwani, ambapo SUZA kimeshinda kwa kupata asilimia 84 dhidi ya asilimia 74.8
za ZIFA.
No comments:
Post a Comment