Na Mwandishi Wetu
MKE wa Rais wa Zanzibar,
Mama Mwanamwema Shein, amewataka Vijana wa Chama cha Mapinduzi, kuibua mambo
mapya ya maendeleo yatayoifanya Zanzibar kuwa nchi yenye mafanikio na kukuza
soko la ajira kwa vijana.
Mama Shein, aliyasema
hayo jana wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya muziki kwa bendi ya Vijana wa
Chipukizi wa Chama cha Mapinduzi, huko katika uwanja wa Gombani Wilaya ya
Kusini Kisiwani Pemba.
Mama Shein, alisema Chama
cha ASP, wakati kinaanzisha kiliona umuhimu wa kuwaunganisha vijana kwa kuweka
utaratibu maalum wa kuwaandaa vijana kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao na
kuweza kuwa warithi wa taifa hili hapo baadae.
Alisema ni laziama vijana
wathamini jitihada za Chama cha CCM, kwa kuwaandaa ili waweze kukabiliana na
soko la ajira pamoja na kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao .
Alisema utaratibu huo kwa
kiasi kikubwa uliweza kusaidia serikali kuweza kupata vijana walio na uzalendo
wa nchi yao, pamoja na waaminifu na walinzi shupavu wa nchi yao.
Alisema bila ya kuwaandaa
vijana nchi inaweza ikayumba kwani wanahitaji kuona wanaandaliwa kiakili,
elimu, kinidhamu, kimaadili na kupewa mafunzo yatayoweza kuwajengea uzalendo.
Alisema serikali inapenda
kuona vijana wa Zanzibar, wanakuwa ni wenye uwezo wa kuibua mambo mapya
ya kimaendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa yataweza kuwafanya kuwa washupavu zaidi
katiuka shughuli zao.
Hata hivyo, Mama Shein,
aliwataka vijana hao kuona umuhimu wa kuyathamini Mapinduzi ya Zanzibar kwa
vile ndio yaliowakomboa vijana kuweza kufanya shughuli zao chini ya Jemedari wa
Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Nae Mke wa Makamu wa Pili
wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, akitoa maelezo yake, alisema vijana nchini wa
kila sababu ya kuhakikisha hawayumbishwi katika kukitetea chama chao.
Alisema Chama cha CCM,
kimeona umuhimu wa kuwaunganisha vijana na ndio maana kimeamua kuwaundia
Umoja wa Vijana.
Kutokana na hali hiyo,
Mama Asha, aliwataka kuona haja ya kuwajenga kuwa wamoja iliu waweze
kufanya kazi kwa ushirikiano na kuufanya umoja wao kuwa tegemeo kwa vijana
wengine.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Shaka Hamdu, amewataka vijana kuona haja ya kutunza amani ya nchi kwa
kutambua kwamba uhuru wa nchi haupatikani mara mbili.
Alisema inasikitisha
kuona baadhi ya vijana kuingizwa katika vitendo vya vurugu vinavyotokea katika
maeneo mbalimbali duniani, jambo ambalo limekuwa likisababisha kupotea kwa
uhuru wa nchi zao.
Alisema hali hiyo,
imeanza kiuonekana katika mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Sudani ya Kusini
ambapo hivi sasa baadhi ya wananchi wao wamekuwa katika mazingira magumu
kutokana na amani kuharibika.
Kutokana na hali hiyo,
Shaka alisema viongozi wa Jumuiya hiyo, watahakikisha kuona vijana wanakuwa
katika mazingira bora ya maisha yao.
Nao viongozi wa Bendi
hiyo, walishukuru kwa msaada walioupata kwa vile utaweza kuifanya bendi hiyo
kuendeleza ajira yao.
No comments:
Post a Comment