Na Othman Khamis Ame. OMPR
Mradi mpya wa ujenzi wa Chumba cha chini ya Bahari uliofanywa na Hoteli ya Manta Resort iliyopo katika Kijiji cha Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba umeiweka Zanzibar katika ramani mpya ya Dunia katika harakati za kuimarisha sekta ya Utalii unaobeba nafasi kubwa ya Uchumi katika Mataifa mengi Ulimwenguni.
Chumba hicho cha chini ya Bahari kilichopo Makangale ambacho ni cha pekee Barani Afrika kimeiwezesha Zanzibar kuwa ya tatu kwa kuwa na mradi kama huo Duniani ikitanguliwa na Nchi za Puerto Riko,Sweden, Kisiwa cha Fiji na ikifuatiwa na Dubai mradi uliyoko katika Matengenezo unaotarajiwa kuwa na vyumba takriban 220.
Jengo hilo lenye huduma kamili anazostahiki kuzipata mwanadamu ni pamoja na chumba cha kulala,huduma za maji safi,Choo, umeme, sehemu ya Mapumziko, na eneo maalum la juu kwa ajili ya kuotea jua.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae ndiye aliyeweka Nanga ya Msingi ya mradi huo wa Makangale Miezi 12 iliyopita Tarehe 25/12/2012 akakizindua tena rasmi chumba cha mradi huo kilichoko umbali wa mita Nne chini ya Bahari.
Uzinduzi huo uliojumuisha mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Makangale pamoja na majirani zake ulishuhudiwa pia na Viongozi kadhaa wa Serikali, vyama vya Siasa pamoja na watendaji wa Sekta ya Utalii wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake Mh. Bihidndi Hamad.
Akizungumza mara baada ya kuuzindua Mradi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba uwepo wa mradi huo wa chumba cha chini ya Bahari ni kielelezo muhimu kitakachokuwa kivutio kwa wageni katika harakati za kukuza utalii hapa Zanzibar.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale kwa kuamua kuwekeza mradi huo wa kipekee Barani Afrika ambao utaleta maendeleo makubwa katika Sekta ya Utalii.
“ Nimeshuhudia uzuri wa chumba hichi ambapo yapo mazingira mazuri ya mapumziko na kulala, samaki wa kuvutia. Natarajia wakaazi wanaonguuka eneo hilo watashirikiana vyema na uongozi wa Hoteli hiyo katika kukilinda chumba hicho kinachotarajiwa kuongeza ushawishi kwa watalii kutembelea Zanzibar “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alielezea matumaini yake kwamba Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort Makangale utaendelea kutoa huduma bora na za uhakika ili kuongeza idadi ya wageni na watalii kutembelea Pemba.
Katika kuunga mkono jitihada hizo za wawekezaji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwapa mashirikiano ya karibu wawekezaji wa sekta hiyo ili waendeshe shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
“ Sisi Viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais na mimi mwenyewe tunapofanya ziara nje ya nchi hutumia fursa ya kuwabembeleza wawekezaji kuwa kuwekeza Nchini mwetu hasa katika sekta ya utalii na Viwanda. Bahati nzuri wanatuitikia na wanakuja na ndio maana leo Zanzibar ina vitega uchumi vingi vya sekta ya utalii na mfano hai ni huu mradi wa chumba cha chini ya Bahari hapa Makangale “. Alifafanua Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya uwekezaji katika sekta ya utalii lakini bado Serikali pamoja na Wananchi wanahitaji kuendelea kuwa na matumaini ya kuongezeka kwa idadi ya watalii hali ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Taifa.
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba watalii na wageni hao hawataingia nchini iwapo jamii haitojikita katika kuendeleza amani na utulivu ndani ya maeneo yao hasa sehemu zenye vitega uchumi hivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wananchi hawanabudi kupania kuiweka nchi katika hali hiyo ya amani na usalama ili wageni hao washawishike kupenda kuendelea kutembelea Nchini na kuishi bila ya wasi wasi.
“ Tuwe wanyenyekevu kwa wageni wetu, tuwaonyeshe bashasha za Kizanzibari kama ilivyo tabia na desturi yetu, tusiwabughudhi wakiwa ufukweni au katika matembezi yao. Tunataka wafurahie ukaazi wao katika visiwa vyetu vya karafuu na Viungo “. Alieleza Balozi Seif.
Mapema Meneja Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa Nini “ alisema utafiti wa mradi huo ulifanyika kwa karibu miaka sita ambapo wataalamu wa kimazingira na mambo ya bahari walilazimika kupima mwenendo wa maji ya bahari ya eneo hilo ili kuwa na uhaika wa kuanzisha mradi huo.
Bwana Methew Saus alisema mazingira ya Kisiwa cha Pemba yamepelekea kuanzishwa kwa mradi huo wa majaribio wa chumna cha chini ya Bahari uliogharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Laki Tano { U$ 500,000 } sawa na fedha za Kitanzania Milioni Mia 758,000,000/-.
Meneja huyo wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wizara inayosimamia Sekta ya Utalii kwa ushirikiano iliyompa kuweza kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mradi huo kwa kiasi kikubwa umeanza kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya utalii wa Daraja la juu duniani.
Waziri Mbarouk aliwaasa wananchi na hasa wavuvi wanayoizunguuka hoteli hiyo kujiepusha na uvuvi pembezoni mwa mradi huo jambo ambalo litaondoa sifa na mazingira halisi ya kuwepo kwa samaki wanaokizunguuka chumba hicho.
Alikemea tabia iliyoanza kujichomoza ya baadhi ya wavuvi wa maeneo hayo ya kuvua kwa kutumia nyavu ndogo nje ya chumba hicho kwani inaweza kumvunja moyo muwekezaji huyo ambae ameshajitolea kusaidia maendeleo ya Vijiji jirani na Hoteli hiyo.
Mradi wa mwanzo wa ujenzi wa vyumba vya chini ya Maji Jules Undersea Lodge umeanza Nchini Puerto Rica mwaka 1970, Utter In Vasteras Sweden Mwaka 2000,Poseidon Undersea Resort Fiji na Mwengine Crescent Hydropolis unaendelea kujengwa Nchini Dubai.
No comments:
Post a Comment