Na Khamisuu Abdallah
HUKU mataifa duniani yakiendelea na
siku 16 za kupinga udhalilishaji wa kijinsia, mambo yamegeuka Zanzibar ambapo wanawake wanadaiwa
kuwanyanyasa wanaume.
Kwa ilivyozoeleka wanawake ndio
waathirika wakubwa wanaokabiliwa na vitendo vya udhalilishaji, lakini hapa Zanzibar kibao
kimewageukia wanaume ambao kwa mujibu wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi
zipo kesi kadhaa zilizoripotiwa.
Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili
huko Ofisini kwake Muembemadema, Mkuu wa Dawati hilo Staff Sagenti Zahor Faki, alisema
kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wenye tabia ya kuwanyanyasa
waume zao ikiwemo kuwapa vipigo.
Alisema dawati lake limepokea
kesi tisa za wanawake kuwadhalilisha wanaume na kwamba kesi hizo zimeripotiwa
kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi Oktoba.
Alisema wanawake wengi wenye kufanya
vitendo vya udhalilishaji hasa vya kuwapiga waume zao, hufanya kwa kuvizia hasa
wakiwa wanaume hao wamelala.
Mkuu huyo alisema sababu kubwa
zinazopelekea waume hao kupigwa na wake zao zinatokana na wanawake wengi kuwa
na wivu wa kupindukia katika ndoa zao pamoja na migogoro ya kugombani mali .
Aidha akizitaja sababu nyengine alisema
zinatokana na watoto wakati wazazi wao wanapoachana huku mwanamke akizuia hati
ya nyumba ambayo si haki yake bila kukaa kulitatua tatizo hilo .
"Sababu hii inatokana na mume
alieachana na mke wakati wakiwa wameshazaa mwanamke huanza vurugu na kuzuia
hati ya nyumba wakati si haki yake na husema hatoi mpaka apewe kitu fulani bila
ya kukaa pamoja na kulitatua tatizo hilo ",
alifafanua Mkuu huyo.
Alifahamisha kuwa wanawake wengi
wamekuwa wakiwavizia waume zao wakati wakiwa usingizini na kuwajeruhi sehemu
mbalimbali za miili ikiwemo sehemu ya siri huku wakiwapa maneno makali.
Zahor alifahamisha kuwa mbali na
malalamiko hayo lakini wanaume wengi wamekuwa hawaripoti katika Dawati hilo kutokana na mambo ya aibu jambo ambalo linawakosesha
haki zao za msingi kama vile wanawake.
Hata hivyo Mkuu Zahor alisema hakuna
hata lalamiko moja lililofikishwa mahakamani bali mengine huyatolea uamuzi na
mengine bado yanaendelea na upelelezi.
Akizitaja changamoto zinazowakabili ni
pamoja na wanawake wanaofanya vitendo hivyo kuja na hukumu zao mikononi jambo
ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Hivyo aliwataka wanandoa kujua wajibu
wao kwani ndoa ni hidaya huku akiwasisitiza kuacha tabia ya kuishi kwa chuki na
kusikiliza fitna za watu ambao hawawatakii mema.
Pia aliwashauri wanaume hao kutoona
tabu kufika katika vituo vinavyohusika ili viweze kuwatetea kama wananawake
ambao hupaza sauti zao na kusikika haraka kutokana na kuundwa kwa tasisi
mbalimbali kama vile Zafela, Tamwa na Dawati
la kijinsia.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mtendaji
wa Jumuiya ya Maimam Zanzibar, Sheikh Khamis Yussuf Khamis akizungumzia saula hilo alisema ni kweli malalamiko hayo huwa yanaenda katika
jumuiya yao .
Aidha alifahamisha kuwa jumuiya yao kesi hizo
zinapotokezea huwa wanasuluhisha kwa kutumia njia za kidini hasa kuwapa wanandoa
elimu ya kujua wajibu wao.
Hivyo aliwataka wanandoa hao kupata
elimu ya kutosha kabla hawajafunga ndoa ili kuondokana na matatizo mbalimbali
ya hapa na pale.
Sambamba na hayo aliwashauri vijana wa
kiume kufuata mawazo ya busara kutoka kwa wazazi wao na sio kufuata utashi wa
marafiki ambao hawawatakii mema katika ndoa zao.
No comments:
Post a Comment